Header Ads

UFAFANUZI KADI NYEKUNDU YA AJIBU MSIMU ULIOPITA, ILIMZUIA KUCHEZA DHIDI YA NDANDA?

Ajib-red-card
Baada ya mshambuliaji wa Simba Ibrahim Ajib kuitumikia klabu yake kwenye mchezo wa kwanza wa ligi msimu wa 2016/17 dhidi ya Ndanda FC, umezuka mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii kama nyota huyo alikuwa na uhalali wa kucheza game hiyo baada ya kupata kadi nyekundu mwishoni mwa msimu uliopita.
Ajib alioneshwa kadi nyekundu wakati Simba ikicheza dhidi ya Mwadui FC Jumamosi May 7, 2016 kwenye uwanja wa taifa mechi iliyomalizika kwa Simba kuchapwa na Mwadui bao 1-0. Ajibu alimkanyaga Hassan Kabunda wa Mwadui FC dakika chache kabla mechi hiyo haijamalizika na kujikuta akioneshwa kadi nyekundu na mwamuzi wa mchezo huo Anthony Kayombo.
Utata uliozuka ni kwamba, je Ajib alimaliza adhabu ya kutumikia kadi nyekundu aliyooneshwa na mwamuzi Anthony Kayombo?
Baada ya kadi hiyo, Ajib alikosa mechi tatu mfululizo za mwisho za ligi kuu Tanzania bara, mechi alizokosa ajibu ni Majimaji 0-0 Simba (11-05-2016), Mtibwa Sugar 0-1 Simba (15-05-2016) na mchezo wa mwisho wa ligi Simba 1-2 JKT Ruvu (21-05-2016).
Jedwali linaloonesha mechi nne za mwisho za Simba katika msimu huliopita. Baada ya Ajib kutolewa kwa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Mwadui, hakucheza mechi tatu za mwisho zilizosalia kwenye ligi
Jedwali linaloonesha mechi nne za mwisho za Simba katika msimu huliopita. Baada ya Ajib kutolewa kwa kadi nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Mwadui, hakucheza mechi tatu za mwisho zilizosalia kwenye ligi
Kwa mijibu wa kanuni za ligi, kanuni ambayo inahusu udhibiti na adhabu kwa wachezaji, kuna kipengele kinasema kwamba, mchezaji atakayetolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja (straight red card) atakosa michezo miwili inayofuata.
Kifungu kingine cha kanuni hiyohiyo kinaongeza, mchezaji atakaeolewa kwa kadi nyekundu kwa kosa la kupiga au kupigana, atasimama kushiriki michezo mitatu inayofuata ya klabu yake na atalipa faini ya shilingi laki tano (500,000).
Kanuni hiyohiyo katika kipengele kingine kinasema kwamba, mchezaji atakaeoneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa ligi kuu au atakaemaliza msimu wa ligi kuu akiwa na adhabu ambayo haijaisha muda wake, ataendelea kutumikia adhabu hiyo katika msimu unaofata isipokuwa adhabu inayotokana na kadi za njano.
Kulingana na takwimu hizo, Ajib alistahili kucheza mchezo wa ufunguzi wa ligi msimu wa 2016/17 dhidi ya Ndanda FC.

No comments