Header Ads

YANGA wamfuata Kipre Tchetche Ivory CoastUONGOZI wa Yanga hivi karibuni ulikutana kwa lengo la kupitia ripoti ya kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm iliyohusiana na mechi iliyopita ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Medeama ya Ghana na kukubaliana kumfuata Kipre Tchetche.
Katika kikao hicho, pia viongozi hao walitumia nafasi hiyo kujadiliana ni namna gani watafanya ili waweze kuipata saini ya  mshambuliaji huyo wa Azam FC, ambaye kwa sasa yupo kwao nchini Ivory Coast.
Inadaiwa kuwa, Tchetche amegoma kurudi nchini kuendelea na majukumu yake ya kuitumikia timu hiyo.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa baada ya majadiliano hayo, uongozi ulikubaliana kumtuma mwakilishi nchini humo kwa ajili ya mazungumzo na mchezaji huyo ambaye wamekuwa wakimwinda kwa muda mrefu.
 “Ni kweli kabisa Tchetche tulimjadili na tupo kwenye harakati za kumtuma mtu ili akafanye naye mazungumzo ikiwa ni pamoja na kumtangazia ofa yetu tutakayompatia kwani tunataka tumsajili katika kipindi cha dirisha dogo.
“Hatujakurupuka kufanya hivyo ila tumejiridhisha kabisa kuwa mchezaji huyo kwa sasa hayupo tayari kurudi Azam, kama tofauti na hivyo basi tusingefikia uamuzi huo wa kumtuma mtu ili akazungumze naye.
“Tunataka kumsajili aje kuziba pengo la  Donald Ngoma ambaye amekuwa akiomba kutaka kuondoka zake akacheze soka huko Afrika Kusini,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit alikanusha kuwepo kwa mpango huo: “ Hakuna kitu kama hicho kwani sisi tumeshamaliza usajili wa wachezaji wa kigeni na hatutarajii kusajili mchezaji mwingine tena.”

No comments