Header Ads

Askali Magereza

 Askari wa Jeshi la Magereza Tanzania (jina lipo) wa Gereza la Ukonga jijini hapa ameingia kwenye skendo nzito kwa madai ya kumshambulia kwa kipigo mfungwa aitwaye Hamza Ally Mponda na kusababisha kifo chake huku mkuu wa gereza hilo, akitoa ufafanuzi.

Kifo hicho kilichoacha majonzi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, kilijiri usiku wa Septemba 9, mwaka huu gerezani hapo. Akizungumza kwa huzuni na gazeti hili, shemeji wa familia ya marehemu aitwaye Hassan Mabuyu alisema kifo cha mpendwa wao kimewasikitisha sana. Mabuyu aliongeza kuwa, marehemu Hamza ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Lupilo, Mahenge, Ulanga mkoani Morogoro na ndugu zake, Uwezo Mponda na Hassan Mponda walihukumiwa kifungo kwa kosa la kumpiga roba na kumvunja mkono mtu mmoja.

Alisema hukumu hiyo ilitolewa mwaka 1998 katika Mahakama ya Wilaya ya Ulanga, Mahenge lakini kutokana na watuhumiwa kukata rufaa mara kadhaa na kushindwa, miaka ya kutumikia adhabu iliongezeka ambapo wanapaswa kutoka mwaka 2018.

 Akielezea tukio la kifo cha shemeji yake huyo, Mabuyu alisema: “Septemba 10, mkewe alipigiwa simu na kaka yake Inspekta Aziz aishiye Kondoa, Dodoma aliyefahamishwa na rafiki yake askari magereza wa Morogoro kwamba, Hamza amefariki dunia  kwa kupigwa na askari.” Aliongeza kuwa, kuhofia kuwa angemwambia moja kwa moja dada yake kwamba Hamza amefariki dunia angechanganyikiwa sana, inspekta huyo akamficha na kumweleza alipewa taarifa kwamba, Hamza ni mgonjwa sana hivyo waende wakamwangalie.

 “Baada ya kuambiwa hivyo, aliwafahamisha ndugu wengine, ndipo yeye, shemeji yake aitwaye Hassan na kijana mwingine walielekea gerezani Ukonga kumuona lakini wakiwa njiani, mke wangu alipigiwa simu na mtu aliyesema ni askari magereza na kumwuliza kama ni  ndugu wa Hamza, akasema ndiyo.” Mabuyu aliongeza kuwa, mtu huyo alimwambia Hamza alifariki dunia. Ndipo naye alimfahamisha mumewe huyo
ambaye aliondoka kuelekea gerezani kujua undani wa kifo. “Tulipofika na k u j i t a m b u l i s h a tulipokelewa na afisa mmoja wa magereza, akatupeleka ofisini kwake akiwa na wenzake. Huko tuliambwia kifo cha Hamza kilitokana na ugonjwa wa kifafa uliokuwa ukimsumbua.” Mabuyu alisema, walishangazwa na taarifa hiyo kwani marehemu hakuwa akisumbuliwa na maradhi hayo na hawakuwahi kupewa taarifa kwamba alikuwa akiumwa kifafa, hivyo waliomba kuonana na Uwezo anayetumikia kifungo chake katika gereza hilo.

 “Tukiwa kwenye mazungumzo kuhusiana na kifo cha ndugu yake, mbele ya maafisa wa magereza, Uwezo alisema si kweli kwamba Hamza alifariki kwa ugonjwa wa kifafa isipokuwa ni kipigo. “Uwezo alisema yupo tayari kuelezea tukio hilo popote kwa sababu alilishuhudia. Alisema ilikuwa siku ya Jumatano, yeye Uwezo alitoka kwenda kufanya kazi za nje.

 “Kwa mujibu wa Uwezo, aliporejea gerezani aliitwa na askari huyo na kumwambia anywe dawa kwani alihisi alimeza madawa ya kulevya. “Uwezo alimwambia askari huyo yeye hakumeza kitu chochote, ndipo akamzaba makofi na kwenda kumfungia kwenye chumba kimoja gerezani humo.” Mabuyu aliendelea kusema kuwa, Uwezo aliwaambia wakati wa chakula ulipofika, Hamza
alimfuata yule askari magereza kwa lengo la kumuomba ampatie chakula.

Cha kushangaza akamwambia alikwenda kumletea fujo na kuanza kumshambulia. Mabuyu alidai kuwa, Uwezo alisema askari huyo alimpiga teke Hamza kwenye ubavu wa kushoto, kichwani, mgongoni na sehemu mbalimbali za mwili kisha kwenda kumfungia chumbani huku akiwa hoi ambapo wafungwa wenzake walilaumu kwa nini apelekwe humo wakati ameumia? “Uwezo akatuambia ilipofika usiku, marehemu alipiga kelele kuomba msaada kufuatia hali yake kuwa mbaya, ndipo wenzake walikwenda kumwambia askari
aliyekuwa zamu.”

 Aliongeza kuwa, Uwezo aliendelea kudai, ilipofika asubuhi waligundua Hamza amefariki dunia, lakini askari wakawaambia wafungwa wengine kwamba alizidiwa kwa ugonjwa hivyo wanampeleka kutibiwa kwenye Zahanati ya Magereza kisha wakaupeleka mwili wake  Hospitali ya Taifa Muhimbili. Mabuyu alisema, Septemba 12 walikwenda kuonana na Mkuu wa Gereza la Ukonga, ACP Stephen Mwaisabila  ili kujua kiini cha kifo cha shemeji yake ambapo aliwaambia ni kweli ilitokea hali ya kutoelewana baina yake na askari huyo lakini hakufariki kwa sababu ya kipigo. Mabuyu aliongeza kuwa, wakati wa uchunguzi
wa mwili wa marehemu (postmortem) uliohudhuriwa na yeye mwenyewe, Inspekta Aziz Mshamu  ambaye ni mdogo wa marehemu, Hassan, daktari, Bakari ambaye ni askari wa Kituo cha Polisi cha Salenda, Adam aliyekuwa msimamizi wa kazi siku hiyo mochwari na mhudumu, yeye aliweza kuona jeraha la marehemu lililotoa damu utosini na alikuwa na michubuko mgongoni na walipohoji daktari hakuwapa jibu badala yake alitoka nje ambapo mpaka leo hawajapata majibu. Baada ya kusikia madai ya upande wa ndugu, Septemba 17, mwaka huu, Uwazi lilifika ofisini kwa mkuu huyo wa Gereza la Ukonga, ACP  Mwaisabila ili kuzungumza naye kuhusu madai hayo. Kwanza alikiri kifo hicho kutokea lakini akisema si kwa sababu ya kipigo. “Ni kweli kifo cha Hamza kilitokea Septemba tisa, lakini hakikusababishwa na kipigo kama ndugu wanavyodai, ila kilitokana na ugonjwa wa kifafa uliokuwa ukimsumbua,” alisema Mwaisabila na kuongeza: “Tarehe sita tulipata taarifa Uwezo ambaye ni kiongozi wa wafungwa (nyapala) alikuwa na madawa ya kulevya hivyo, alipoingia mlangoni huyo askari wanayedai alimpiga Hamza alimwambia Uwezo japo ni kiongozi alitakiwa kukaguliwa ili kubaini kama alikuwa na madawa ya kulevya au simu, vitu ambavyo wafungwa huvificha njia ya  haja kubwa, akagoma. “Ilibidi ampeleke kwenye chumba kinachotumika kufanyia ukaguzi, alivua nguo na kutakiwa achuchumae ajisaidie.

Wakati akiwa katika hali hiyo alitokea Hamza, aliyekuja kumuuliza Uwezo chakula chake amuachie nani lakini akamuuliza askari kwa nini anamdhalilisha ndugu yake, wote wakaanza kumshambulia askari, ndipo walipokamatwa. “Walipelekwa kwa msaidizi wa mkuu gereza ambaye aliwaambia siku iliyofuata angewaleta kwangu. Siku hiyo sikuweza kuonana nao kwa sababu nilikuwa bize na wageni,  lakini tarehe nane nilikutana nao, nikazungumza nao kisha kuwaonya wasifanye  fujo tena, nikawatenganisha vyumba vya kulala. “Akiwa amelala na wenzake watatu, Hamza usiku alizidiwa na ugonjwa wake, wakamleta akiwa kachoka sana. Ndipo tukampeleka kwenye zahanati yetu kisha kumkimbiza Muhimbili alikofariki dunia,” alisema Mwaisabila.

Mwandishi wetu alipomuuliza kama waliwafahamisha ndugu zao kuhusu kupatwa na maradhi hayo ya kifafa akiwa gerezani, alisema kwa kuwa hali hiyo ilikuwa ikitokea mara chache hawakufanya hivyo kwani walipokuwa wakimtembelea kumjulia hali aliwaambia alikuwa mzima lakini  gereza lina kumbukumbu zinazoonesha alikuwa anaumwa kifafa na alikuwa akitumia dawa. Hata hivyo, mkuu huyo wa gereza alisema uchunguzi ulifanywa ili kubaini kama marehemu alipigwa ambao uliwahusisha ndugu,  askari magereza, polisi wa Kituo cha Salenda na daktari ambapo ilithibitika kuwa, hakupigwa na ndugu kuridhia kisha kuuchukua mwili kwa mazishi.

No comments