Header Ads

First XI: Simba vs Azam Kesho hii hapa


AZAM (5)

Wachezaji wa timu ya Azam wakifanya mazoezi.

Nicodemus Jonas na Said Ally

KESHO Jumamosi Simba itakuwa mgeni wa Azam katika mchezo wa raundi ya tano ya Ligi Kuu Bara, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru lakini timu zote zikiingia zikiwa na nguvu sawa. Zina idadi sawa ya pointi, mabao ya kufunga na ya kufungwa na zinakabana koo kileleni mwa msimamo.

Katika mechi nne walizocheza kila moja, kila moja imeshinda mechi tatu, sare moja, pointi 10, zimefunga mabao saba, zimeruhusu mabao mawili tu, hali ambayo huenda mchezo wa leo ukabadili taswira ya sasa.

AZAM (1)

Wachezaji wa timu ya Azam wakiendelea na mazoezi.

Pamoja na kulingana kila kitu lakini hiyo haimaanishi kuwa zitafananisha hadi ubora na udhaifu wa vikosi. Pia wapo wachezaji wamekuwa kwenye ubora pande zote mbili na Championi inakuletea kikosi cha kwanza cha muunganiko kuelekea mchezo huo.

Kwenye uteuzi huo, kigezo tosha ni kiwango cha mchezaji kwenye mechi nne zilizopita pamoja na rekodi yake. Mfumo wetu ni wa 4-2-3-1 ambao ndiyo mfumo wa kisasa unaotikisa kwa sasa.

simba1

Wachezaji wa Simba wakishangilia kwa pamoja.

Ulaya, Jurgen Klopp wa Liverpool aliupendelea zaidi pindi akiwa Borussia Dortmund na ndiyo uliifikisha timu hiyo fainali ya Uefa dhidi ya Bayern Munich mwaka 2013 japo walipoteza.

Kwa mujibu wa Tovuti ya Soccerpilot.com, mfumo huu huonekana kama wa kujilinda zaidi (defensive formation) lakini kimajukumu, beki za pembeni hufanya kazi kama mawinga huku pia ikitegemeana na majukumu ya kiungo namba sita hasa pale mpira unapokuwa kwenye miliki yenu; aidha kuilinda ngome ama kupeleka mashambulizi, majukumu ambayo pia huweza kufanywa na namba nane.

Kikosi cha Championi hiki hapa;

Golikipa: Aishi Manula- Azam

Licha ya kuruhusu mabao mawili kama ilivyo kwa Vincent Angban wa Simba, lakini Manula anakaa hapa kutokana na ubora wake wa kujua kuwasoma wafungaji, umahiri wa kupangua penalti na ameiokoa Azam na Taifa Stars mara kibao pindi anapobakia na mfungaji. Juzi Kocha wa Stars, Charles Mkwassa alikiri kama asingekuwa Manula, Stars ingekula hata sita mbele ya Nigeria badala ya kufungwa bao 1-0.

Beki kulia: Shomari Kampombe

Ni nadra sana Azam kufungwa bao kutokea upande wa kulia. Kapombe mbali na ulinzi wake mkali, sifa ya kipekee ni ubora wake wa kupandisha mashambulizi, krosi murua na kufunga mabao pengine hakuna beki anayeweza kumfikia kwa kufunga mabao. Msimu uliopita alifunga jumla 11, tayari msimu huu amefunga moja (Ngao ya Jamii) na zaidi ni kasi yake uwanjani. Si Hamad Juma, Besala Bokungu bado hawamuwezi.

SIMBA DAY (19)

Mshambuliaji mpya wa Simba, Mrundi Laudit Mavugo.

Beki kushoto: Tshabalala-Simba

Ni kutokana na ubora wake, ametunukiwa zawadi ya gari. Beki huyo ambaye jina lake kamili ni Mohammed Hussein amekuwa nguzo muhimu kwa Simba, akiva sifa karibu zote za Kapombe. Mashambulizi mengi ya Simba hupitia kwake, kwa sasa amekabidhiwa jukumu la faulo kikosini hapo, achilia mbali ubora wa krosi za mabao.

Beki ya kati: Daniel Amoah: Azam

Mghana huyu pamoja na kuichezea mechi mbili Azam dhidi ya Prisons na Mbeya City, lakini tayari shughuli yake imeonekana. Gemu na Prisons akiachaza sambamba na David Mwantika alifanikiwa kumfunika fowadi Jeremiah Juma kabla ya kucheza sanjari na Himid Mao mechi na Mbeya City. Zaidi Amoah analindwa na shughuli pevu alivyowahenyesha mafowadi wa Yanga kwenye mchezo wa Kombe la Afrika akiwa na Medeama kwenye mechi zote.   

Beki ya kati: Method Manjale- Simba

Mzimbabwe huyu amemficha kabisa Juuko Murshid na tayari ameanza kusahaulika kwenye nafasi yake ya namba tano pale Msimbazi. Panga pangua amekuwa kikosini huku Kocha Joseph Omog akionekana hana mpango na Juuko ambaye msimu uliopita alikuwa nguzo ya Simba. Pengine kukosekana kwa Pascal Wawa pale Azam imechangia kwa sana kumpatia nafasi hii maarifu kama mkoba.

Kiungo: Himid Mao- Azam

Kwa mfumo wetu wa 4-2-3-1, Mao anafaa kusimama kama kiungo cha kukaba. Hii ni kutokana na soka lake la kibabe, kutibua mashambulizi na mara kadhaa amekuwa akicheza kama mlinzi. Mfano ni mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City alipocheza kama mkoba. Pia ni hodari kwa kupanga mashambulizi akicheza kama kiungo mchezeshaji (box-to-box).

Winga kulia: Shiza Kichuya- Simba

Ni kosa kubwa utakapotaja mastaa walio kwenye fomu usilitaje la kiungo huyu wa zamani wa Mtibwa. Achilia mbali chenga, kasi yake inayowapa wakati mgumu mabeki, Kichuya mpaka sasa ameifungia Simba mabao mawili; moja ligi (dhidi ya Ndanda) na jingine dhidi ya FC Leopard ya Kenya (kirafiki). Ana asisti tatu mpaka sasa; mbili dhidi ya Leopard kabla ya kutengeneza tena dhidi ya Ndanda.

Kiungo: Jonas Mkude- Simba

Kulingana na mfumo wetu, Mkude anafiti kucheza sanjari na Mao, jukumu zaidi likiwa ni kuilinda ngome, badala ya kupeleka mashambulizi, hata hivyo mmojawapo kwa kuelewana atalazimika kupanda na mwenzake kusimama kama kiungo mkabaji. Mkude ni panga pangua mkabaji wa Simba, majukumu ambayo kwa Azam aidha hupewa Michael Bolou ama Jean Mugiraneza ‘Migi’. 

Mshambuliaji wa Kati: John Bocco- Azam

Huyu ndiye atasimama kama mshambuliaji pekee kwenye mfumo huu, kazi yake kubwa ni kuangalia goli liko wapi kwa krosi, pasi za kutanguliziwa ama mipira atakayoletewa na mshambuliaji msaidizi (namba 10). Ubora wa Bocco unajulikana enzi na enzi na kila msimu ndiye rungu la Azam. Ameiokoa mara nyingi sana ndiye mchezaji aliyefanikiwa kufunga mabao matatu haraka msimu huu.

Mshambuliaji Msaidizi: Laudit Mavugo- Simba

Ni homa ya jiji kwa sasa. Ukiwa msimu wake wa kwanza Bongo, Mrundi huyo tayari ameifungia Simba mabao manne, matatu ligi kuu na moja mechi ya kirafiki. Katika mechi nne alizocheza, jamaa ameingia kambani mara tatu, kwa tafsiri nyingine amefunga katika kila mechi ambayo Simba imefanikiwa kufunga bao. Zaidi ya kufunga, Mavugo ni hodari wa kumiliki mpira, anakaba, mzuri kwenye pasi na zaidi zaidi kasi, sifa zinazompa nafasi ya kumsapoti Bocco kwenye kikosi chetu

Winga wa kushoto: Ibrahim Ajib- Simba

Kontroo zake, kumiliki mipira na ubora wa pasi zake kwenye mfumo huu zinampa nafasi ashambulie akitokea pembeni, achilia mbali anavyocheza namba 10 kwenye kikosi cha Simba, sambamba na Mavugo. Ajib anaweza kubalishana na Kichuya kwenye wingi ya kulia na kufanya majaabu.

Kocha: Joseph Omog- Simba

Ingawaje Zeben Hernandez wa Azam hajapoteza kama ilivyo kwa Omog lakini Zeben atabakia kuwa kocha anayejifunza mazingira ya soka la Kibongo. Ni mgeni kumlinganisha na Omog anayelijua fika pamoja na kuzifahamu timu zote, Simba na Azam.

MWISHOOOO. 

No comments