Header Ads

Hukumu ya Yanga SC, Kessy kesho


KESHO Jumapili itakuwa aidha siku ya furaha au huzuni kwa Simba inayosubiri jibu la mwisho la Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ambayo inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi yao dhidi ya Yanga na beki wao wa zamani, Hassan Kessy.

Simba ilifungua kesi hizo wakimtuhumu Kessy kuanza kuitumikia Yanga wakati akiwa na mkataba wao, kesi inayowabana pia Yanga kwa kuingia mkataba na mchezaji mwenye mkataba kwingine.

Championi Jumamosi lilifanikiwa kunasa nakala ya malalamiko ya Simba ambayo inataka Kessy kuwalipa kitita cha Sh bilioni 1.3 kwa mujibu wa kipengele cha mkataba wake Msimbazi.

Kesi hizo ndizo pekee ambazo hazikupatiwa ufumbuzi kati ya kesi 25 zilizosikilizwa Jumatatu wiki iliyopita na kutolewa uamuzi, hiyo ni kutokana na upande wa Yanga kutohudhuria, hivyo kusogezwa mbele kwa wiki moja.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema kamati hiyo inatarajia kuketi tena kesho kusikiliza kesi hiyo na zile ambazo walizitaka pande mbili kumalizana nje ya kamati.

“Ya Yanga ilishindikana kutokana na wao kutofika kusikiliza shauri lao, lakini tumeshawapa barua ya kuwataka Jumapili kuwepo na ndipo yatatolewa maamuzi juu ya kesi ya Kessy.
“Pia malalamiko yote ambayo yalitakiwa kumalizwa nje ya kamati kwa makubaliano ya pande mbili kufikia kesho (leo) na kutakiwa kutoa mrejesho, kesi zao zitarudi mezani tena,” alisema Lucas.

No comments