Header Ads

Ibrahim Ajibu: Naondoka Simba SC

MSHAMBULIAJI wa Simba, Ibrahim Ajibu amefunguka kuwa hadi sasa hajui iwapo ataendelea kuitumikia klabu hiyo msimu ujao  ama lakini akasisitiza ana asilimia kubwa za kuondoka Msimbazi. Staa huyo amesisitiza kuwa hana mpango wa kuendelea kucheza soka la Bongo kwa sasa. Ajibu ni miongoni mwa wachezaji wenye viwango vizuri wanaotegemewa na Kocha wa Simba,
Joseph Omog.
 
Hata hivyo, mshambuliaji huyo amebakiza miezi michache ili kukamilisha mkataba wake wa miaka mitatu aliosaini mwaka 2014 ambao unaelekea ukingoni mwishoni mwa msimu huu. Lakini juzi amedai ana asilimia kubwa ya kutoendelea kucheza soka Bongo. Akizungumza na Championi Jumatatu,

Ajibu amesema anachokihitaji yeye kwa sasa ni kusonga mbele na kucheza soka la kimataifa, hivyo amepanga kufanya hivyo mara baada ya kukamilisha mkataba wake na Simba na kudai kuwa mara baada ya kufikia tamati, ndipo atakapojua aamue kucheza wapi. “Ndiyo, nimebakiza muda mchache kuweza kumaliza mkataba wangu na Simba lakini sijajua itakuwaje ila nasubiria hadi pale utakapofikia tamati ndipo nitakapojua wapi pa kwenda kucheza. “Kwa sasa sina mpango wa kucheza soka la Bongo kwani mikakati yangu ni kuona nafanikiwa kwenda mbele zaidi kisoka na si kuishia hapa tulipo hivi sasa.

 “Kuna mipango yangu ambayo naendelea kuifanya hivi sasa ya kusaka timu nje na pindi itakapokamilika, ndipo nitajua nifanye maamuzi gani kwani nahitaji kuwa wa kimataifa zaidi,” alisema Ajibu. Ajibu ni miongoni mwa mastaa wa Yanga na tayari msimu huu ameshaifungia timu hiyo mabao mawili.

Ajibu ni miongoni mwa wachezaji wanaong’aa Msimbazi tangu msimu uliopita na ni mmoja wa mastaa wanaopendwa na mashabiki klabuni hapo. Mwishoni mwa msimu uliopita, staa huyo alikwenda kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini, muda mfupi baada ya kupewa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Mwadui uliomalizika kwa Simba kufungwa bao 1-0. Alikwenda nchini humo bila kuuaga uongozi na akafanya majaribio katika kikosi cha Kaiser Chiefs lakini akafeli, baadaye akaenda Golden Arrows, ikaelezwa kwamba amefaulu lakini Simba wakashindwa kukubaliana na klabu hiyo.

No comments