Header Ads

Kama kweli unampenda, usiombe likakukuta hili!

LEO nataka kuzungumza na wewe rafiki yangu, ambaye umejitolea kwa moyo wako wote kumuonesha mwenzi wako kwamba unampenda na kumthamini kwa moyo wako wote lakini unachoambulia ni mateso na maumivu kila kukicha! Kabla sijaendelea na mada yetu, ningependa kukushirikisha kisa cha dada yetu mmoja ambaye ameomba nisimtaje kwa jina gazetini lakini ni mkazi wa Temeke jijini Dar. 


Kama kawaida yangu, huwa napenda kubadilishana mawazo na wasomaji wangu wanaosumbuliwa na matatizo mbalimbali ya kimapenzi, siku chache zilizopita dada huyu akawasiliana nami na kunieleza mkasa wake akiomba ushauri kutoka kwangu. Alijitambulisha kwamba yeye ni dada ambaye ametokea kumpenda kwa dhati kijana mmoja wanayeishi naye mtaa mmoja, akaniambia kwamba japokuwa kijana huyo hana shughuli yoyote inayomuingizia kipato, anampenda hivyohivyo na yeye ndiye anayemuwezesha kimaisha, kwamba akiwa na mahitaji madogomadogo, huwa anamtimizia kwa sababu anajishughulisha na biashara Kariakoo inayomuingizia kipato cha kutosha. 

“Tatizo linalonisumbua, huyu kaka japokuwa mimi nampenda kwa moyo wangu wote lakini yeye haoneshi kuwa ‘serious’, ananifanyia vituko vingi sana ila navumilia. Kwanza huwa hawezi kunitafuta kwenye simu, mimi ndiyo kila
siku nimpigie au kumtumia SMS. Nikikaa kimya, inaweza hata kupita wiki hajanitafuta japo tunaishi jirani kabisa. 


“Kingine, hata tukikutana mtaani, anataka mimi ndiyo nimchangamkie na kumsalimu. Nikisema nijaribu kunyamaza, unaweza kukuta tunapishana kimyakimya kama hatujuani. Muda pekee ambao anaweza kunichangamkia ni akiwa na shida ya pesa au kimapenzi. Kama ana shida ya kukidhi haja zake za kimwili, basi ataniitaita na kunitania, akishamaliza haja zake basi, hana habari tena na mimi. Au akiwa na shida ya pesa ndiyo utamuona ananitafuta na kujifanya ananipenda. “Mbaya zaidi, namuona kama akili zake hazijapevuka kwa sababu licha ya kujua kwamba nampenda, haoni hatari kupita na wanawake wengine mbele za macho yangu. 

Siku moja alifikia hatua ya kunitambulisha kwa mwanamke mwingine kwamba eti ndiyo mpenzi wake anayempenda, jambo ambalo liliniuma sana. “Nikimuuliza kwa nini ananifanyia hivi, ananiambia eti hao wengine anawaongopea tu ila ananipenda mimi, japokuwa kiumri nimemzidi lakini nampenda sana, kuna wakati huwa najaribu kuachana naye lakini kila nikimuona au nikisikia sauti yake, moyo wangu unadunda kwa nguvu na kujikuta nikimsamehe hata kama hajaniomba msamaha! “Nateseka sana lakini siwezi kumuacha, nikijiangalia umri nao unasonga mbele nahitaji kuwa na mtu wa kuanzisha naye familia lakini mwenzangu ndiyo hivyo tena, naomba unisaidie, nifanye nini?”

 Hayo ni maelezo machache kati ya mengi aliyonieleza dada huyo, najua wapo wengi wanaopitia matatizo kama haya kwenye mapenzi! Kwamba unampenda sana mtu fulani, na yeye anajua kwamba unampenda lakini badala ya kuuthamini upendo wako, anakufanyia vituko vya kuutesa moyo wako kila kukicha, akiamini kwamba kwake ndiyo umefika na huna ujanja! Je, ni sawa kucheza na moyo wa mtu anayekupenda? Je, mpenzi wako akikuonesha kwamba anakupenda kwa dhati na kwako hafurukuti ndiyo kigezo cha kumnyanyasa kimapenzi? Kutokana na watu wenye tabia kama hizi, siku hizi kuna kasumba ipo mitaani, kwamba hata kama mtu unampenda kiasi gani, eti usimuoneshe kwamba unampenda kwa sababu akishajua, ni lazima atakutesa! Je, hii ni sawa? Tukutane wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii.

No comments