Header Ads

Kikwete Atunukiwa Tuzo Ya Uongozi Wa Kisiasa Na Utetezi


unnamed-59
Rais  mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete,  akipokea Tuzo ya  Uongozi wa Kisiasa na  Utetezi kutoka kwa  Mkurugenzi Mtendaji wa  Speak Up Africa  Bi Kate  Campana,  katika hafla iliyofanyika siku ya Alhamisi  New York Marekani. Tuzo hiyo  ni kutambua jitihada na juhudi zake za kufikisha huduma za jamii hususani  afya kwa   kwa wanawake na watoto.
jk...Baada ya kupokea tuzo yake.
jk-1
 ...Akitoa hotuba baada ya kukabidhiwa tuzo  ambapo alisema tuzo hiyo ni kwa watoto wote wa Afrika ambao ndiyo  walimwezesha kuipata.
jk-3
Watu waliohudhuria katika hafla hiyo wakimsikiliza.
Na  Mwandishi Maalum, New York
Shirika lisilo la  Kiserikali    la Speak  Up for Africa    limemtunuku tuzo, rais mstaafu, Jakaya Kikwete, kutokana na uongozi wake wa kisiasa na utetezi wake  kwa  makundi ya jamii yaliyo katika mazingira magumu hususani wanawake na watoto.
Utoaji wa  tuzo hiyo  ya  uongozi wa kisiasa na utetezi , umekwenda sambamba na   hafla ya  miaka mitano ya kuanzishwa kwa  Taasisi ya Speak up  Africa. Hafla  hiyo iliyofanyika jana Alhamisi Jijini New York   ilikuwa  pia  ni sehemu ya kuhamasisha uchangiaji   wa shughuli za  taasisi hiyo.
Mchango ambao umetambuliwa na  Speak Up  Africa,   taasisi ambayo imekuwa ikifanya kazi  kwa karibu na Kikwete, ni  katika maeneo ya  upelekaji na usambazaji wa huduma za msingi za afya hususani afya ya mama na mtoto,  udhibiti wa  ugonjwa  wa malaria kupitia kampeni  ya Malaria Haikubaliki, usambazaji wa vyandarua  vyenye viatilifu, kampeni ya  lishe bora, na  kampeni ya   chanjo kwa watoto.
Pamoja  na  kutambua  juhudi zake katika  kuyasemea maeneo hayo,  taasisi hiyo kupitia  Mkurugenzi wake  Mtendaji Bi. Kate Campana pia imemtambua  kama kiongozi ambaye    amekuwa mstari wa mbele  wa kulisema Bara la Afrika kila  mara alipopata  fursa  ya  kufanya hivyo wakati akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu.
Kikwete ameelezwa katika hafla hiyo iliyowashirikisha  wadau wa kada mbalimbali, kama kiongozi wa kisiasa ambaye amezigusa nyoyo za watu wengi kujitolea kwa ajili ya watu wenye mahitaji ya kupata huduma za msingi za kijamii ambazo  au wameshindwa kuzipata kutokana na kipato kidogo au haziwafikii kabisa.
Akipokea  tuzo hiyo, amesema tuzo hiyo ni ya watoto wote  Waafrika ambao ndiyo  waliomfanya asimame   mbele ya wageni waalikwa.
“Ni kwa sababu yenu ndiyo sababu nimetenga muda wangu  baada ya kustaafu kusukuma mbele agenda ya  kuboresha maisha yenu. Ninafanya hivyo kwa sababu makuzi yangu yalikuwa kama  ya mtoto yeyote yule wa  Kiafrika, nimeyaishi maisha  wanayoishi. Na kwa hiyo ninaelewa fika  hamu na kiu yao ya kuwa  na maisha bora na afya njema,” akasema Kikwete na kushangiliwa na wageni waalikwa.
Akaongeza kuwa,  mafaniko ambayo ameyapata katika  juhudi hizo  za kufikisha huduma za msingi  za kijamii kwa makundi  yenye mahitaji  yametokana na mambo mawili makubwa moja ni   aina ya uongozi  alioutumia kusukuma harakati hizo. Na pili  uhamasishaji uliofanyika katika  kupiga vita malaria kupitia Speak Up Africa na    kampeni yao ya  malaria haikubaliki.
“Nisingeweza kuyafanya niliyoyafanya   bila uungwaji mkono na  ushirikiano  wa karibu nilioupata  na ninaoupata kutoka taasisi za kimataifa  ikiwamo hii ya  Speak Up  Africa. Ndiyo maana, kwa mfano,  tumeweza kupunguza  malaria kwa   theluthi mbilli,  tumefanikisha  upatikanaji wa chanjo kwa asilimia 96 kwa watoto wote na kupunguza vifo vitokanavyo na  malaria kwa   nusu,” alisisitiza Kikwete na kushangiliwa  tena.
Alisema anamini katika ushirikiano na wadau mbalimbali  kama akina Ray Chambers kupitia kampeni ya  Hakuna Tena Malaria, Taasisi ya  Billy na Melinda Gates na Gavi Vaccination   Alliance ambayo anashirikiana  nayo kwa karibu katika  kampeni ya chanjo kwa wote.
Kikwete amewahakikishia   watendaji wa Speak  Up Africa kwamba  ataendelea kufanya kazi nao kwa karibu  kutokana  kile alichosema amejionea mwenye kazi nzuri wanayoifanya.
 Aliwasihi  wadau mbalimbali  kuichangia taasisi hiyo  kwa kile alichosema, inafanya kazi kubwa  na siyo tu kufikisha huduma za kijamii pale zinapotakiwa lakini  pia imekuwa ni kipaza sauti cha Afrika.
Wengine waliopewa tuzo kwa kutambua michango yao kwa jamii ni  pamoja na   Professa Awa Marie Coll- Seck, Waziri wa Afya  wa Senegal, Bibi Toyin  Saraki,  mwanzilishi wa Taasisi ya  Wellbeing  Afrika ambayo  pia imekuwa ikitoa  elimu na misaada kwa wanawake na watoto pamoja na elimu  kwa wakunga na kutambua kazi nzuri, kubwa na ngumu  ya kuwahudumia wanawake wenzao wanapojifungua.  Pia alikuwemo Kabirou Mbodje ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa  Taasisi ya  Wari.
Taasisi ya  Speak  Up  Africa  imeanzishwa  na wanawake na inaongozwa na wanawake. Ni taasisi ambayo imejijengea uwezo na sifa kubwa ndani  ya kipindi cha miaka mitano tangu  kuanzishwa kwake.   

No comments