Header Ads

Kuiona Yanga vs Simba buku saba

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetangaza viingilio vya mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga dhidi ya Simba unaotarajiwa kupigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ambapo kiingilio cha chini ni Sh 7,000.

Mchezo huo ambao rasmi mashabiki wa soka wataanza kutumia tiketi za elektroniki, utakuwa na viingilio vya aina tatu huku kadi maalum za mfumo huo mpya zikitarajiwa kuanza kutolewa bure leo Jumatano mpaka siku ya mchezo wenyewe.


Akizungumza na Championi Jumatano, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, alisema: “Viingilio vitakuwa ni Sh 30,000 kwa viti vya V.I.P A, V.I.P B na C ni Sh 20,000 na mzunguko ambapo ni viti vya rangi ya bluu kijani na chungwa ni Sh 7,000.


“Tumewaondolea mzigo mashabiki wa soka kwani zile kadi za elektroniki kwa kawaida zinauzwa Sh 3,000, lakini kwa sasa watazipata bure kwenye mawakala mbalimbali wa Selcom, unachotakiwa ni kulipia kiingilio chako kati ya hivyo vitatu, kisha utapewa kadi yako bila ya gharama zingine.”


Wakati huohuo, Meneja Miradi wa Kampuni ya Selcom ambayo inasimamia mchakato huo wa tiketi za elektroniki, Gallus Runyeta, alitaja sehemu zitakazopatikana kadi hizo kuwa ni vituo vyote vya mafuta vya Total, Village Supermarket iliyopo Mbezi Beach, vituo vya mafuta vya Puma na katika matawi yote ya Samaki Samaki. Hiyo ni kwa wakazi wa Dar pekee.


Lakini pia alitaja sehemu zote zenye mawakala wa Selcom Tanzania zinapatikana kadi hizo, ambapo baadhi yake ni Buguruni Sheli, Ilala Bungoni, Vingunguti, Tandika, Buza, Kiwalani na Sinza Afrika Sana.

No comments