Header Ads

Mahiga: Jumuiya ya kimataifa isaidie kukabili rushwa

ANZANIA imebainisha kuwa juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kukabiliana na vitendo vya rushwa, hazitafanikiwa endapo hazitaungwa mkono na Jumuiya ya kimataifa.

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga

Aidha, imezitaka nchi zilizoendelea kuwawajibisha wawekezaji wao, zikiwemo kampuni za mafuta ili zilipe kodi. 

Hayo yalisemwa jijini New York nchini Marekani jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga alipozungumza katika Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la 71 la Umoja wa Mataifa. Alitumia fursa hiyo kuelezea vipaumbele vya Serikali ya Tanzania.

Alisema lengo namba 16 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGS) linatambua kuwa, rushwa inakandamiza juhudi za kupambana na umaskini na usawa wa jinsia, inazuia fursa na inakuwa na kama kodi kwa familia maskini pale wanapotafuta haki.

Balozi huyo alisema Tanzania imeamua kuanzisha vita dhidi ya rushwa kwa kuhuisha uwazi, uwajibikaji na usahihi katika utoaji wa huduma kwenye taasisi za umma.

Alisisitiza kuwa serikali imeweka misingi mizuri ya uwajibikaji, inayomtaka mtumishi wa umma kutambua kwamba wajibu wake wa kwanza ni kutoa huduma bora na kwa wakati kwa umma.

“Juhudi hizi za serikali za kupambana na rushwa hazitaweza kuzaa matunda bila ya kuungwa mkono wa jumuiya ya kimataifa. Nchi zilizoendelea zinatakiwa kuwawajibisha wawekezaji wao pamoja na kampuni za mafuta ili ziweze kulipa kodi stahiki. Ni lazima wawe tayari kurudisha mali na fedha zilizoibwa kutoka nchi zinazoendelea na kuzificha katika nchi zao ili mali na fedha hizo ziweze kusaidia maendeleo yetu,” alisema Balozi Mahiga.

Akizungumzia fursa za jinsia na uwezeshwaji wa wanawake, Waziri Mahinga alisema juhudi mbalimbali zimefanywa na serikali katika kuwawezesha wanawake ikiwemo kushika ngazi za juu za maamuzi kuanzia serikali kuu hadi bunge na uwezeshwaji wa kiuchumi.

Katika kuthibitisha kuwa Tanzania inazingatia usawa wa jinsia katika uteuzi wa ngazi mbalimbali za maamuzi, alisema kwa mara ya kwanza wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Rais John Magufuli aliteua mwanamke kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wa vijana, waziri huyo alisema serikali imeanzisha mfuko wa maendeleo wa vijana ambao hadi kufikia Machi mwaka huu jumla ya Sh bilioni 1.6 zilipelekwa kwa vikundi 284 vya vijana.
Akizungumzia elimu, alisema serikali inatekeleza bila kuchoka kuhakikisha kwamba watoto wote wa kike na wa kiume, wanapata elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, ikiwa ni pamoja na kuboresha mitaala yake kwa kuzingatia mahitaji ya karne ya 21.

“Alipoingia madarakani, Mheshimiwa Dk Magufuli alitangaza kuwa kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari itakuwa bure. Serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 263 ili kuhakikisha elimu inatolewa bure kwa wote,” alisisitiza Balozi Mahiga.

Aliainisha vipaumbele vingine vya Tanzania mbele ya mkutano huo kuwa ni pamoja na mikakati ambayo serikali imejiwekea katika utekelezaji wa mkataba wa mabadiliano ya tabia nchi, utekelezaji wa malengo ya SDGs, mapambano dhidi ya dawa haramu za kulevya na kukabiliana na ugaidi.

Kwa upande wa migogoro inayoendelea katika nchi za Burundi na Sudan Kusini, Mahiga alizitaka pande zote zinazopingana, kutambua kwamba majadiliano ambayo ni jumuishi kwa pande zote ndiyo njia sahihi ya kutatua matatizo ya nchi yao.

Alifafanua kuwa Tanzania ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iliitisha kikao kwa ajili kuzungumzia hali ya kisiasa ya Burundi na Sudan Kusini.

CHANZO; HABARI LEO

No comments