Header Ads

MBUNGE CATHY AFUNGUKA MAZITO

Toa ya moyoni! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mbunge wa Viti Maalum Arusha (CCM), Catherine Magige ‘Cathy’ kufunguka mazito na kukanusha kuhusu madai yaliyotapakaa jijini Arusha kwamba, amewahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mkuu wa mkoa (jina tunalihifadhi kwa kuwa hakupatikana hewani).

 TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo makini kilichopo mkoani humo kimedai kuwa, mbunge huyo yupo kwenye bifu zito na mkuu huyo wa mkoa kiasi cha kila mmoja kumuundia zengwe mwenzake ili aweze kuchafuka kisiasa kama si kuharibiana kazi. “Ubuyu wa motomoto ndiyo huo mimi nakupa, Arusha kwa sasa kila mtu anajua kwamba Cathy na mkuu wa mkoa haziivi, yaani ni kama paka na panya. Unajua iko hivi, wale inadaiwa walikuwa wapenzi, sasa kama unavyojua tena mambo ya mapenzi, ilifika mahali nasikia wakamwagana.

WAKAWA MAADUI
“Baada ya kumwagana ndipo hapo wakageuka maadui. Wakaanza kuwindana, kila mtu anamuwinda mwenzake kivyake. Mkuu wa mkoa akatumia mbinu zake kumchafua Cathy lakini Cathy naye akawa halali, anajibu mashambulizi katika namna ambayo naye aliona inafaa,” kilidai chanzo hicho.

YADAIWA CATHY ALIMJERUHI
Chanzo kikazidi kumwaga ubuyu kuwa, mvutano kati ya wawili hao ulizaa matunda kwa Cathy kwani alifanikiwa kumchongea mkuu huyo wa mkoa kwa wakubwa wake jambo ambalo lilimuathiri katika majukumu yake ya kazi. “Cathy alimpiga kombora moja matata
sana mkuu wa mkoa, alichanganyikiwa. Vita ya mbunge ni kali, alimchoma katika jambo fulani ambalo lilileta mtafaruku kwa mkuu wa mkoa.

MJADALA NI CATHY, MKUU WA MKOA “Yaani kwa sasa ukipita kwenye vilinge mbalimbali Arusha stori inayofukuta ndiyo hiyo. Kuna wengine wanamuunga mkono Cathy na wengine wanamsapoti mkuu wa mkoa. Lakini kama hiyo haitoshi, waungwana wanawashauri wamalize tofauti zao maana mabifu hayana maana,” kilidai chanzo hicho.

ILIANZIA KWENYE UCHAGUZI MKUU ULIOPITA
 Chanzo kilizidi kumwaga data kuwa, ishu ya mbunge huyo kudaiwa kutembea na mkuu huyo wa mkoa ilianza kwenye uchaguzi mkuu uliopita wakati ambao Cathy alikuwa kwenye harakati za ndani ya chama kutetea nafasi yake ya Ubunge wa Viti Maalum. “Kipindi hicho ndiyo watu wanasema penzi la Cathy na mkuu wa mkoa lilishamiri kwelikweli. Wengi walikuwa wanajua hilo, nashangaa nyinyi Global mlikuwa kimya kuripoti ishu hiyo,” kilidai chanzo hicho.

CATHY HUYU HAPA Akizungumza na Risasi Jumamosi  juzi kwa njia ya simu kwa takriban dakika 11, Cathy alikiri kuzisikia tuhuma hizo ambapo zilianza kupikwa kipindi cha uchaguzi mkuu uliopita na wapinzani wake kisiasa ili kumchafua na hakuna ukweli wowote kuhusu yeye kutembea na mkuu huyo wa mkoa.

LOWASSA ATAJWA “Sikia iko hivi; kwanza unapaswa utambue hayo mambo yalianza tangu kipindi kile cha kampeni za uchaguzi mkuu uliopita. Hakuna kitu kama hicho, sijawahi kutembea na huyo mkuu wa mkoa na hakuna kitu kama hicho.”

KAMPENI ZILIKUWA NGUMU
“Mimi kampeni yangu nilifanya katika mazingira magumu sana. Kumbuka Arusha yote ilikuwa ni Lowassa na kulikuwa na watu wake walikuwa wagombee na mimi. Nimegombea na watu wake ndani ya CCM. “Siku mbili kabla ya uchaguzi, nilikuwa Marekani kwenye sherehe ya Watanzania, alikuwepo rais Kikwete (Jakaya) na Membe (Benard), nikawa nimepiga picha na Membe. Wakaigoogle kwenye mtandao, waliituma kwa wapiga kura wote kunichafua, ile picha siku mbili kabla ya uchaguzi ilisambaa na ujumbe usemao; huyu ni mtu wa Membe nini?”

MAKUNDI YA URAIS YATAJWA
“Ni makundi tu ya urais. Na mimi siku ya uchaguzi watu wa Lowassa walikuja kwa kishindo lakini namshukuru Mungu uchaguzi ulitendewa haki na mimi nikawa namba moja, ndipo hapo walipoanza kusuka hayo mambo. “Baada ya ushindi watu walianza kusema mimi na huyo mkuu wa mkoa tunatoka. Ukiwaambia leteni ushahidi, hawana. Kwanza mimi siwezi kufanya kitu kama hicho. Mimi ni mke wa mtu jamani. Hayo ni mambo tu ya siasa wanaleta ili kunichafua, namshukuru Mungu wameshindwa. “Watu wanashindwa kufanya kazi na kuleta maendeleo wamekalia kuzushazusha mambo yasiyokuwa na kichwa wala miguu, mara utasikia hili mara utasikia lile yaani ili mradi tu wakuchafue,” alimaliza Cathy.

MKUU WA MKOA ATAFUTWA
Ili kutaka kusikia upande wa pili, mwanahabari wetu alimtafuta mkuu huyo wa mkoa kupitia namba yake ya simu kwa takriban siku mbili mfululizo lakini haikuwa hewani ila jitihada za kumtafuta zinaendelea

HABARI NA STORI:ERICK EVARIST/GPL, RISASI JUMAMOSI

No comments