Header Ads

Meya: Temeke Inakabiliwa Na Ongezeko La Watu (Video)meya-temeke-2  Wahariri wetu Elvan Stambuli (kushoto) na Sifael Paul (kulia) wakihojiana na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Temeke, Abdallah Jaffar Chaurembo ambaye ni Diwani wa Kata ya Charambe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCC).
Sifael Paul na Elvan Stambuli
Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Temeke ni miongoni mwa halmashauri tano za Jiji la Dar. Nyingine ni Ilala, Kinondoni, Ubungo na Kigamboni. Pia Temeke ni miongoni mwa manispaa tatu za jijini Dar. Nyingine ni Ilala na Kinondoni. Ubungo na Kigamboni bado hazijapandishwa kwa vigezo kuwa manispaa.

Wiki hii kwenye sehemu ya kwanza ya mahojiano haya ya Uwazi Live tunaye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Temeke, Abdallah Jaffar Chaurembo ambaye ni Diwani wa Kata ya Charambe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCC).
Katika mahojiano yake na Uwazi Live hivi karibuni ofisini kwake, alifunguka mambo mengi kuhusiana na changamoto alizokutana nazo, mipango na mikakati ya kuwaletea wananchi wake maendeleo, masuala ya utumbuaji majipu na mengine mengi, ungana naye;

meya-temeke-1
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Temeke, Abdallah Jaffar Chaurembo akiendelea kufunguka.
TEMEKE YAKABILIWA NA ONGEZEKO LA WATU
Swali: Manispaa ya Temeke ina changamoto nyingi, je, ni changamoto zipi kubwa ulizokutana nazo tangu ukabidhiwe ofisi?
Jibu: Changamoto kubwa ni ongezeko la watu kwa kasi kubwa. Kwa sasa Temeke ni kimbilio la watu wengi ambao wanakuja kutafuta maisha kutoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania.
Kila anayetaka kutoka kimaisha anakimbilia Temeke kwa sababu tumeweka mazingira mazuri yanayowavutia watu kuja kujitafutia maisha. Kwa mfano kuna ongezeko kubwa la watu hasa Mbagala. Ukifika pale Mbagala, Rangi-Tatu, Maji-Matitu hadi Chamazi, unaweza kujiuliza mara mbilimbili kuwa watu wale wote wanaoonekana pale kila siku wanatokea wapi?
Lakini ukweli ni kwamba ile ni sehemu ndogo tu ya wakazi wa Temeke ambao wote wanaamini watapata maisha kwenye manispaa hii.
Sasa changamoto kubwa ni kuwahudumia kielimu kwa kuhakikisha wanapata elimu, maji safi, kuweka miundombinu mipya na kuboresha iliyokuwepo, masoko, namna ya kupata mikopo na zaidi sana katika afya.

meya-temeke-4
Elvan Stambuli (kulia) na Sifael Paul (kushoto) wakiendelea kumsikiliza Meya (hayupo pichani).
Ukweli ni kwamba Hospitali ya Temeke kwa sasa imezidiwa. Mbali na kupokea wagonjwa wa Temeke pia inalazimika kuhudumia watu kutoka Mkuranga na Rufiji, Pwani na hata mikoa mingine ya kusini.
TEMEKE YAKUBALI KULIPA FIDIA YA VIWANJA
Swali: Halmashauri ya Temeke inakabiliwa na tatizo kubwa la migogoro ya ardhi, je, kama Meya umelitafutia muarobaini gani?
Jibu: Kwenye manispaa hii hakuna migogoro mikubwa. Iliyokuwepo ni kama ile ya maeneo ya Kigamboni ya Pemba-Mnazi, Kimbiji na maeneo mengine. Tulichokifanya ni kuanzisha na kuimarisha miradi ya kupima viwanja.
Tulichukua ardhi ya watu ambao wanatudai zaidi ya Sh. bilioni 3 lakini ndiyo tumefungua njia na sasa mapato ni makubwa. Baraza limekubaliana kuwalipa watu wote tuliowachukulia ardhi yao maeneo ya Kimbiji, Geza-Ulole na mengineyo. Changamoto kubwa ipo kwa watu binafsi kupima viwanja wenyewe, cha msingi tumeweka sheria ndogo Kigamboni na baraza linaisimamia.

TEMEKE YAKABILIWA NA ONGEZEKO LA MACHINGA
Swali: Kuna tatizo la kusambaa kwa wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) maeneo mbalimbali kwenye halmashauri yako, kinachoonekana kila mmoja anajipangia eneo lake, je, hili likoje?
Jibu: Ni kweli, miongoni mwa watu wanaohamia Temeke kwa kasi, wengi ni wafanyabiashara ndogondogo kwa sababu ya mazingira mazuri wanayoona yanafaa kwa ajili ya biashara zao. Tuliwaita mimi na Sophia Mjema (Mkuu wa Wilaya ya Temeke).
Walengwa walikuwa ni wale wa barabarani, masokoni na wale waliovunjiwa vibanda vyao. Tulianza kwa kuwatengea maeneo na kuwapeleka kwa ajili ya shughuli zao. Lipo eneo kama Toangoma Stand, Kigamboni. Tunachokifanya ni kuhakikisha tunapeleka huduma stahiki kwa wafanyabiashara wadogowadogo.
Pia kuna eneo la Mbagala, Rangi-Tatu lenye wafanyabishara wadogowadogo wengi tumewatengea eneo zuri kule Charambe na Nzasa na tumeshawapa barua ya kuhamia pale. Wafanyabiashara ndogondogo ni wenzetu hivyo ni lazima tuwatengenezee mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao.
Katika hili shukrani ziende kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Pia tupo mbioni kutekeleza agizo la Rais Dk John Pombe Magufuli la kutenga siku maalum kwa ajili ya soko la pamoja ili wafanyabiashara kwa kushirikiana wajenge utaratibu wa kulipa kodi.

meya-temeke-3
Abdallah Jaffar Chaurembo akieleza ongezeko la watu katika  wilaya yetu.
UTUMBUAJI MAJIPU TEMEKE NI ENDELEVU
Swali: Vipi kuhusu utumbuaji wa majipu kwa watumishi wa halmashauri yako wasiowajibika, je, utumbuaji majipu umeisha?
Jibu: Suala la utumbuaji majipu siyo la mpito au la kusema sasa limekwisha hivyo watu wasifanye kazi. Ni suala endelevu na si kwa watumishi wa zamani tu, hata wa sasa wasipowajibika lazima watatumbuliwa tu.
Serikali ya Awamu ya Tano inataka watu wawajibike katika kila nafasi. Yeyote anayefanya kazi chini ya kiwango atatumbuliwa tu.
Tusieleweke vibaya lakini yeyote anayezembea au anayeshindwa kwenda na kasi yetu aondoke kwani ni sehemu ya watu wachache. Ninachosisitiza hapa ni watu kuwajibika na kuwa waadilifu kwenye ofisi na maeneo yao ya kazi.

TEMEKE HAKUNA MPASUKO WA KISIASA
Swali: Sasa hivi kwenye baraza lako kuna mchanganyiko wa madiwani kutokana na vyama vyenye itikadi tofauti, Je, hilo halikupi shida kiutendaji?
Jibu: Ni kweli kwenye baraza langu kuna mchanganyiko wa madiwani kutoka CUF, Chadema na CCM. Sisi tulichokifanya ni kukubaliana kwamba tuweke misingi imara ya utendaji kazi kwenye halmashauri na manispaa yetu na hakuna mpasuko wa kisiasa.
Tulikubaliana tuweke siasa pembeni na kufanya kazi. Hakuna matukio makubwa ya kiutendaji. Baraza pia lilisimamia kikamilifu suala la kugawana mali kihalali bila tatizo.
Tulikubaliana kwa pamoja kuwa tunatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kuhakikisha tunawahudumia watu, wapate barabara, maji, huduma za afya na kuwaletea maendeleo wananchi.

TEMEKE WAPANGA KUJENGA BARABARA ZENYE MIFEREJI
Swali: Barabara nyingi za halmashauri zimejengwa chini ya viwango na huwa zinaharibika hata kabla ya kukabidhiwa, je, hili baraza lako la madiwani mnaliwekea suala hilo mikakati gani?
Jibu: Ukweli ni kwamba kwa zile barabara za halmashauri hakuna zilizojengwa chini ya kiwango. Upo mradi wa CIUP ambao barabara zake zimedumu hadi leo. Tunasimamia sana kuhakikisha barabara zetu hazina upungufu. Kama kuna upungufu si wa kiutendaji au kiusimamizi ila kuna suala la mapato kidogo.
Pia ujenzi wa barabara zisizo na mifereji, tumeamua kwa pamoja kwenye baraza letu kuhakikisha tunajenga barabara zenye mifereji. Pia barabara zimekuwa nyembamba na si kwamba hazina ubora hivyo lazima tuzipanue ili kuondoa misongamano na kuharakisha maisha ya watu wetu.

No comments