Header Ads

Mmeoana ili mgawane vyumba au Vitanda

KARIBU tena jamvini mpenzi msomaji wangu wa makala za XXLove kwa ajili ya kupata chakula cha ubongo ili uelimike na kudumisha uhusiano wako wa kimapenzi na maisha yako ya kila siku. 


Mada yangu ya wiki mbili mfululizo zilizopita juu ya ulazima wa kulifanya penzi lako kuwa hai (up date) iliibuka mjadala mkubwa. Wengi walionipigia simu na kunitumia SMS walikiri kukosea katika vitu vidogovidogo lakini pia waliwatupia lawama wenza wao.

 Nilichowashauri ni kwamba wafanye wanachokiamini kwa vitendo ili kulinda uhusiano wao na kuwaachia wenzi wao wakijitathimini. Ipo siku wenzi wao nao watajishtukia kuwa kuna kitu wanakosea. Siyo vema mmoja anapojisahau na mwingine naye ajifanye amejisahau kwani wote mtatumbukia shimoni.

 Baada ya kusema hayo, turudi kwenye mada ya leo ambayo nitawazungumzia baadhi ya wapenzi au wanandoa wenye tabia ya kulumbana, kupigana, kuchuniana mara kwa mara hadi kufikia hatua ya kulala mzungu wa nne, kutengana vitanda au hata vyumba vya kulala (kama Mungu amewabariki kuwa navyo). 

Hebu tujiulize, hivi inakuwaje wapenzi mnagombana na kuanza kutengeneza mipaka ya kugawana vyumba au vitanda? Hivi mlioana ili mgawane vitu hivyo? Msema kweli ni mpenzi wa Mungu kama anavyosema Rais John Pombe Magufuli, nami nasema kweli, kufanya hivyo si sahihi hata kidogo. 

Hata kama mmekwazana, si sahihi kugawana vitanda au vyumba kwani kwa kufanya hivyo ni kutengeneza au kuhalalisha uchepukaji miongoni mwenu. 

Jifunze kuwa na hasira za muda. Hasira ambazo baada ya muda, utazifuta na mwenzako atajua umezifuta na maisha yanaendelea kwa vicheko kama kawaida na hata chakula cha usiku mnaendelea kulishana kama kawaida. Jamani tukubaliane kuwa ndoa ni tamu. 

Ila kama mtashindwa kusomana na kujuana tabia zenu, basi mtaiona chungu kama shubiri. Kikubwa ni kila mmoja kumjua mwenza wake hapendi nini na anapenda nini. Lakini pia wapenzi au wanandoa mnapaswa kuvumiliana kwenye shida na raha kama ambavyo mliapa.

 Sasa kwa nini mshindwe kuvumiliana kwa sababu ya misukosuko ya hapa na pale ambayo inapita? Usikubali kumkimbia mpenzi wako au kuhama kitanda. 

Kama unaona umemkwaza au amekukwaza, basi jitahidi kufanya juu chini kusawazisha mambo, kumfanya mwenzi wako awe na amani, upendo na furaha kama mwanzo. Siku zote hakikisha uhusiano wako unakuwa wa amani na furaha. 

Tumia nguvu na akili yako yote kumshawishi na kumridhisha mwenzako kuwa kile ulichokifanya ni kosa na kwa kuwa unampenda, hauko tayari kumuudhi kwa kurudia kosa kama hilo. 

Mkiwa na tabia ya kugawana vitanda au vyumba, mnaweza kujikuta mnashindwa kujizuia baadhi ya mambo na yawezekana ikawa ni rahisi kwa kuchepuka kwa sababu hali hiyo inatoa nafasi ya kutengeneza mazingira ya usaliti. Haipendezi, mnadhani mnatoa picha gani kwa watoto wenu wa kizazi hiki cha sasa ambao wanafahamu kila kitu kinachoendelea, tofauti na watoto wa kizazi cha miaka ya nyuma? Ni matumaini yangu nimeeleweka na makala hii utaitumia kama tiba ya tabia hiyo kama inakuhusu wewe au mwenza wako. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine murua.

No comments