Header Ads

Mshindi Chemsha Bongo Na Amani Apewa Zawadi YakeMshindi wa tatu wa Chemsha Bongo na Amani, Jimmy Kisanga akiwa ameshikilia zawadi yake ya Sh. 500, 000 mara baada ya kukabidhiwa.
amani-mshindi
Mshindi wa tatu wa Chemsha Bongo na Amani, Jimmy Kisanga (kushoto) akikabidhiwa zawadi yake ya Sh. 500,000 na wakala wa Global jijini Mwanza, Alex Mabula. Makabidhiano hayo yalifanyika Jumamosi iliyopita katika ofisi za Global.
Na Idd Mumba, Mwanza
MSHINDI wa tatu wa Chemsha Bongo ya kwenda Dubai inayotolewa na Gazeti la Amani, Jimmy Kisanga mkazi wa Igoma jijini hapa, amekabidhiwa zawadi yake, Sh.500,000.
Akizungumza na mtandao huu mara baada ya kukabidhiwa zawadi yake hiyo, Jimmy alianza kwa kuishukuru Kampuni ya Global kwa kuweza kuwajali wasomaji wake kwani amekuwa mshiriki na shuhuda wa zawadi nyingi zitolewazo katika chemsha bongo mbalimbali.
“Kwanza namshukuru Mungu kwa zawadi hii na pili niishukuru Global kwa kweli, hii ni mara ya tatu tangu nimeanza kushiriki chemsha bongo hii hivyo kila toleo nilikuwa nasoma swali na kulijibu huku nikisubiri huenda nami nikashinda. Kweli Mungu ameonesha njia na leo hii (Jumamosi iliyopita) nimeshinda na kukabidhiwa zawadi yangu ya shilingi 500,000.
“Kiukweli najiona ni mtu mwenye bahati ya hali ya juu, ujue haipiti siku bila kusoma haya magazeti ya Global yaliojaa hadithi na habari mbalimbali za kufunza. Niwaombe wale wengine ambao hawajashiriki ama wamekata tamaa, wasikate tamaa na wala wasiwe na imani kwamba zawadi hizi zina watu wake maalum wanaowajua wao, hapana!” alisema Jimmy ambaye pia ni mfanyakazi Bodi ya Pamba kitengo cha kuendeleza zao la pamba jijini hapa.
Jimmy aliongeza kuwa zawadi hiyo aliyoshinda imemsaidia kwa kiasi kikubwa kumalizia ada ya mtoto wake aliyokuwa akidaiwa.
“Nina mke na watoto watatu, mmoja yupo darasa la kwanza mwingine la tatu na wa mwisho hasomi. Sasa huyu wa darasa la tatu anasoma shule ya Olimpio na alikuwa akidaiwa ada, niwe mkweli zawadi hii imekuja muda muafaka,” alimaliza Jimmy.
Jimmy anakuwa mshindi wa tatu wa chemsha bongo hii baada ya awali kuwapata wawili, Godwin Deodath Katiali mkazi wa Njia Panda Machame, Moshi na mwingine, Bakari Omar Omunga mkazi wa Manzese jijini Dar.
Chemsha Bongo hii bado inaendelea katika Gazeti la Amani. Kushiriki ni rahisi sana, unachotakiwa kufanya ni kununua gazeti lako la Amani kila Alhamisi na kujibu swali kiufasaha linalopatikana ukurasa wa pili. Kumbuka mshindi pia anaweza kupata safari ya kwenda kwenye jiji la maraha duniani, Dubai kula bata kwa siku tatu.

No comments