Header Ads

MZEE YUSUF APATA WAKATI MGUMU KUTOKA KWA WAKE ZAKE!

MIONGONI mwa matukio makubwa ya kukumbukwa kwenye ulimwengu wa Muziki wa Taarab nchini kwa mwaka huu ni pamoja na kitendo cha Mwanamuziki Mzee Yusuf kuachana na kazi hiyo kisha kumgeukia Mungu ila sambamba na hilo, amepata mtihani mzito, Ijumaa linakuhabarisha. Mzee Yusuf ambaye hivi karibuni alikwenda Makka kuhiji ikiwa ni moja ya nguzo za Uislam, alitangaza azma yake hiyo Agosti, mwaka huu katika msikiti mmoja uliopo Ilala jijini Dar huku akitokwa na machozi akieleza kuwa, amemkosea Mungu wake kwa muda mrefu hivyo anatubu na kuamua kujikita kwenye ibada pamoja na kuimba kaswida.

 
MASHEHE WAMZUNGUMZIA
Uamuzi huo mgumu aliochukua Mzee Yusuf licha ya kuwashtua wadau wa Muziki wa Taarab nchini, umepokewa kwa mikono miwili na waumini na viongozi mbalimbali wa Dini ya Kiislam huku wengi wakimpongeza ila wakaeleza kuwa, baada ya uamuzi huo, anao mtihani mzito unaomkabili kwa sasa. Akizungumza na Ijumaa hivi karibuni, shehe mmoja wa msikiti maarufu jijini Dar aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini alisema: “Kwanza ni jambo la kumshukuru Mungu sana kwa kumuonesha Mzee Yusuf Swiratwal mustakim (njia iliyonyooka) ila mtihani mzito alionao hivi sasa ni kuhusu wake zake.

 AWAZUNGUMZIA WA MZEE
“Ninavyojua ana wake wawili licha ya kwamba aliwahi kuoa, akaacha. Huyo mke mmoja, Chiku simfahamu vizuri ila mtihani alionao kwake ni kuhakikisha na yeye anakuwa kwenye mstari ulionyooka, kama tulivyoambiwa kuwa, wake zetu wako chini ya mamlaka ya wanaume, hivyo kwanza Mzee Yusuf kwa hilo atakuwa na mtihani mzito wa kuhakikisha na yeye anafuata vilivyo maamrisho ya Dini ya Kiislam. “Kwa huyu Leila, nimesikia mara baada ya mume wake kutangaza kuacha muziki, yeye amesema ataendelea na kazi hiyo, huu nao ni mtihani mzito kwa Mzee. Akiendelea na kazi hiyo atakuwa anamtibulia mwenzake kwa Mungu na ili kuushinda mtihani huo, ifike mahali kama yeye ameamua kuachana na muziki, basi amshawishi na mkewe naye aungane naye laa sivyo ibada zake zitakuwa na matundu,” alisema shehe huyo.


KUHUSU MALI, UTAJIRI ALIOPATA KWENYE MUZIKI
 Aidha, baada ya Mzee kutangaza kuacha muziki, wadau mbalimbali walihoji kuhusu uhalali wa mali na pesa alizochuma kupitia kazi hiyo huku wengine wakisema anatakiwa azigawe zote kwa watu wenye uhitaji. Kufuatia hoja hiyo, shehe huyo alisema kuwa, Dini ya Kiislam haina ugumu kiasi hicho na kwamba kama ameamua kuachana na muziki, alichokichuma kupitia kazi hiyo bado ni halali na akitumie katika misingi inayotakiwa. “Hilo la kwamba kwa kuwa ameacha muziki basi na mali zake azitelekeze siyo sawa, kama ni hivyo basi hata wake zake aliowaoa kupitia huo muziki awaache, aoe wengine, jambo ambalo siyo sawa. “Ni hivi, unapoamua kumrudia Mungu wako ni kama unaanza moja, tukianza kusema eti pesa alizochuma kupitia muziki ni haramu pamoja na mali zake pia, hapo tutawafanya hata wengine wanaotaka kufuata nyayo zake wasite. “Tunachotakiwa kufanya sasa ni kumuombea Mzee afe akiwa kwenye Uislam wake, lakini pia afaulu mtihani wa kuhakikisha wake zake nao wanaingia kwenye swiratwal mustakim na kwa uwezo wake Mungu atafanikiwa Inshaallah,” alisema shehe huyo.

SHEHE MKUU DAR ANASEMAJE? Ili kupata elimu zaidi, mwandishi wetu alimtafuta Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum ili kuzungumzia uhalali wa mali na utajiri alioupata Mzee Yusuf wakati alipokuwa akifanya muziki, mahojiano yalikuwa hivi: Ijumaa: Assalaam alaikum shehe, nilitaka kukuuliza juu ya mambo matatu yanayomhusu Mzee Yusuf, hivi dini inasemaje kuhusu yeye kumuacha mkewe aendelee kufanya muziki huo wakati yeye ameamua kuuacha? Shehe: Dini inasema usimkatishe mtu tamaa, yeye amejaaliwa basi tumtie moyo na huenda kwa kugeuka yeye na wake zake wakamfuata. Ijumaa: Je, kwa upande wa mali na pesa alizopata wakati anaimba ni halali kuendelea kuzitumia? Shehe: Kidini huenda siyo kila kitu kikaenda sawa lakini kwa kuwa amebadilika basi tusiangalie upande wa kumkatisha tamaa. Ijumaa: Je, iwapo akikosa hela ya matumizi na mkewe akamhudumia kwa pesa aliyoifanyia kazi ya muziki itakuwa ni sawa? Shehe: Kibusara naomba maswali mengine nisiyajibu, dini haiko kwa ajili ya kuwakatisha tamaa watu, nakusisitizia mwandishi, iwapo amebadilika basi kila kitu kitabadilika taratibu, wote hatujui mipango yake huenda kwa kuanza yeye akajaaliwa kuwabadilisha na wengine. Mambo ya mali, pesa Mwenyezi Mungu ndiye anajua.

 MZEE YUSUF ANASEMAJE? Jitihada za kumpata Mzee kuzungumzia mtihani huo mzito alionao baada ya kumrudia Mungu ziligoma baada ya taarifa kuwa alikuwa hajarudi kutoka Makka. Kutoka meza ya Ijumaa Gazeti hili linamtakia kila la heri Alhaj Mzee Yusuf katika maisha yake mapya na linamuombea kwa Mungu aweze kushinda mtihani huo unaomkabili na mingine ili aweze kuwa na maisha mazuri ya hapa duniani na kesho akhera

No comments