Header Ads

PIQUE: SHAKIRA NI STAA AKIWA KAZINI TU


Saleh Ally aliyekuwa Barcelona
MAHOJIANO kati ya beki Gerard Pique wa Barcelona, yanaendelea. Championi likiwa jijini Barcelona, Hispania lilizungumza na beki huyo kwa ufupi kutokana na muda wake.
Pique ambaye pia ni beki wa timu ya Taifa ya Hispania, alieleza mengi kuhusiana naye, ushindani wa ligi, namna ambavyo anaweza kucheza wakati wa mechi ya watani maarufu zaidi, yaani El Clasico ambayo huwakutanisha Barcelona dhidi ya wapinzani wao wakubwa Real Madrid.
Lakini alielezea kuhusiana na anavyoamini unapotaka kumlinganisha nyota Lionel Messi dhidi ya mshambuliaji Cristiano Ronaldo ambaye ni nyota wa Madrid.
Hiyo ilikuwa ni jana na kama unakumbuka tuliishia wakati Pique alipoulizwa swali kuhusiana na Shakira ambaye ni mpenzi wake na wana watoto wawili.
Pique na Shakira wanaishi jijini Barcelona katika moja ya maeneo ambayo wanaishi watu maarufu au matajiri.
Wamekuwa kivutio kikubwa cha jiji hilo kwa kuwa Shakira ambaye ni mwanamuziki kutoka Colombia, pia ni maarufu sana.
Kitu kizuri zaidi, historia yao inaanzia barani Afrika, mwanzoni mwa mwaka 2010 walipokutana nchini Afrika Kusini kabla ya michuano ya kwanza ya Kombe la Dunia kufanyika barani humo.


Championi: Mpenzi wako Shakira ni mtu maarufu kama wewe, bahati nzuri mlikutana kwetu Afrika maisha kabla yake na baada ya kuwa naye, yakoje?
Pique: Nafikiri muda umekwisha…

Championi: Sasa ni dakika 12, tunaweza kumalizia haraka hizi dakika tatu.
Pique: Sawa (anaangalia saa), halafu anakaa kimya.

Championi: Nakusikiliza…
Pique: Amini Shakira ni mama bora, ni mlezi wetu sote. Watoto na mimi. Kumbuka kazi ya soka kila wakati unakuwa ‘busy’ mazoezini, mikutano na kadhalika, lakini najitahidi sana kuwa karibu na familia.
Championi: Haikupi shida kwa kuwa mpenzi wako ni mtu nyota?
Pique: Ninaishi maisha ya kawaida kabisa, watu wanaona hilo, Shakira ni staa kwenye kazi yake, kama ilivyo mimi. Lakini baada ya hapo, sisi ni watu wa kawaida kabisa.

Championi: Ungependa siku moja asimame kuimba, zaidi akae na familia?
Pique: Huo ni uamuzi wake, siwezi kulifafanua zaidi.

Championi: Ungependa watoto wako hata kama ni mabinti siku moja wawe wanasoka?
 Pique: Huo pia ni uamuzi wao.

Championi: Kukutana kwenu Afrika unakuzungumzia vipi, maana ilikuwa ni kurekodi video ya wimbo wake, lakini mkaenda mbali zaidi?
Pique: Afrika napakumbuka, tulifanikiwa kubeba Kombe la Dunia, lakini ilivyokuwa na Shakira, si ishu ya watu wote.

Championi: Hapa Ferguson, hapa Guardiola unaambiwa uchague kocha bora, utaweka wapi turufu yako?
Pique: Sitajibu hilo.

Championi: Unafikiri siku moja unaweza kuhama FC Barcelona na kuchezea timu nyingine, mfano Real Madrid?
 Pique: Real Madrid?

 Championi: Ndiyo, Real Madrid.
 Pique: Unaijua historia yangu vizuri?

 Championi: Kuhusiana na soka zaidi, au unazungumzia kuhusiana na mambo mengine?
 Pique: Familia ninayotoka, wazazi wangu?

 Championi: Hapana, 
vizuri uweke vizuri.
Pique…..
 Pique ni mchezaji wa timu ya taifa ya Hispania ambayo ameichezea 78 na kuifungia mabao matano.
 Akiwa na kikosi cha timu ya taifa, amefanikiwa kushinda Kombe la Dunia na Kombe la Euro, yaani mabingwa wa Ulaya.
Makocha mbalimbali waliopita Barcelona ukianzia na Pep Guardiola, timu ya taifa kama kocha maarufu zaidi, Vicente Del Bosque wamekuwa wakimuamini kwa asilimia kubwa pia.
Hakuna ambaye amewahi kukubali kumuacha Pique abakie nje katika kikosi chao. Lakini bado watu wengi wamekuwa wakitupa lawama nyingi kwake.
Kutokana na kutokuwa na makeke, Pique amekuwa ni mlinzi ambaye ameshinda karibu kila taji katika upande wa klabu na inaonekana anawa-shinda wachezaji wengi sana.
Maana yake, chini yake, Barcelona imekuwa chini ya uangalizi sahihi na kupata uwezo wa kushinda kila ilichohitaji.
Pamoja na hivyo, watu wengi wamekuwa wakionekana kutovutiwa na mwendo wake. Kutofurahia anavyocheza, lakini ni mtu ambaye hupenda kuwa alivyo au kuamua kubadilika ghafla.
Katika sehemu ya mwisho, keshokutwa Jumatatu, Pique ataeleza namna ambavyo amekuwa akijisikia kuonekana hana thamani licha ya kazi kubwa. Pia ataeleza namna ambavyo amejifunza kupitia matatizo ambayo amekumbana nayo hasa kushambuliwa na watu ambao anaamini ndiyo walinzi wake. USIKOSE.

No comments