Header Ads

Saida Karoli afunguka ngoma mpya ya Diamond

Msanii mkongwe wa nyimbo za asili, Saida Karoli aliyepotea katika jukwaa la muziki kwa muda mrefu, amefungukia wimbo wake wa Maria Salome, wenye kibwagizo cha Chambua kama karanga, ambao umerudiwa na mkali wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz. Akizungumza na Risasi Mchanganyiko mwanzoni mwa wiki, Saida alisema Diamond alimfuata na kumweleza juu ya nia yake ya kuurudia wimbo huo, kitu ambacho alikipokea kwa mikono miwili na kumpa ruhusa. “Aliniuliza anataka anipe shilingi ngapi, nikakataa, sikutaka anilipe hela kwa sababu mimi ni sawa na nimeshapotea, yeye kuimba wimbo wangu ni sawasawa na kunirudisha tena kwenye muziki, nikamwambia sihitaji hela, ila ninataka kufanya naye nyimbo ikiwa ni pamoja na kurudia baadhi ya kazi zangu akitaka,” alisema mkongwe huyo. Saida ambaye enzi zake alikuwa chini ya uangalizi wa FM Studio ya Felician Muta, alisema baada ya kukubaliana na Diamond, alimpeleka kwa meneja wake huyo kwa makubaliano rasmi ya kisheria yaliyomwezesha nyota huyo wa muziki barani Afrika kwa sasa kuucheza upya wimbo huo, akimshirikisha mmoja wa wasanii wa lebo yake ya WCB, Raimond. Aina ya muziki wa asili uliofanywa na Saida, aliyeibuka akitokea mkoani Kagera, ulimfanya kuwa miongoni mwa wasanii maarufu zaidi katika miaka ya 2000, huku kazi zake zikipigwa katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki, hasa Uganda.

No comments