Header Ads

Simba SC yakwepa hujuma za Yanga SC

UONGOZI wa Simba upo makini kuelekea mchezo wao ujao dhidi ya Yanga baada ya kuwadhibiti wachezaji wao vilivyo ili wasiingie kwenye mtego wa kuhujumiwa na wapinzani wao hao. Simba wamekuwa na kawaida ya kila wakimaliza mechi kuwaruhusu wachezaji wao kwenda kusalimia familia zao, lakini juzi Jumamosi haikuwa hivyo, kwani baada ya mchezo wao dhidi ya Majimaji, moja kwa moja wakaenda kambini Ndege Beach. Simba ambayo juzi Jumamosi iliichapa Majimaji mabao 4-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara
 

uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar, Jumamosi hii itacheza dhidi ya Yanga uwanjani hapo. Katika maandalizi yao kuelekea mchezo huo, jana Jumapili kikosi hicho kiliondoka kwa basi kuelekea mkoani Morogoro huku kikitarajiwa kurudi siku moja kabla ya kuwavaa Yanga. Mmoja wa watu wa benchi la ufundi la timu hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake, ameliambia gazeti hili kuwa, baada ya mchezo wao wa juzi, walijifungia kwenye vyumba vya uwanja huo na kuwa na kikao kizito na viongozi wao ambacho kilidumu kwa takriban nusu saa.
“Jana (juzi) tulikuwa na kikao na viongozi ambapo leo (jana) tumesafiri kwenda Morogoro kuweka kambi ambapo tunatarajia kurudi siku moja kabla ya mchezo wetu huo. “Hii ni vita na lazima tujipange kwa mashambulizi, ndiyo maana utaona wachezaji hawakupewa hata ruhusa za kwenda kuaga familia zao kwa kuhofia kuhujumiwa kwani unajua mchezaji anaweza akapewa nafasi hiyo, wapinzani wetu nao wakautumia mwanya huo kutuhujumu. Hatutaki itokee hivyo na mpaka sasa vita hiyo tumeishinda,” alisema mtu huyo.

No comments