Header Ads

Simulizi ya Msamaha wa Mama - 04

MWANDISHI/MTUNZI: SEID BIN SALIM
Ilipoishia asubuhi……
“Bibi naomba nikuulize swali nisamehe lakini kabla ya kukuuliza.” Nilijihami.
Alinyanyua jicho lake na kunitazama akanambia Uliza kisha akaendelea kusuka mkeka.
“Bibi tangu nizaliwe sijawahi kumuona baba, na sijawai kuambiwa kama amefariki au lah naomba unambie bibi kama unajua chochote kuhusu baba yangu.
Bibi baba yangu yuko wapi?
Sasa endelea……..
Baada ya kumuuliza nilikaa kimya nikashikilia tama nikiwa nimekunja miguu huku nikimuangalia bibi anavyokazana na mkeka. Hakujibu swali langu, alikaa kimya ndani ya dk moja, aliachia pumzi kisha akauweka pembeni mkeka.
“Kweli mjukuu wangu umekuwa mpaka unauliza kuhusu baba! Aya nambie unataka ukweli gani?
“Wowote bibi ikiwezekana unambie tu aliko baba.
“Usijali mjukuu wangu, ukweli utaujua tu kwa kuwa umeuhitaji, ni Stori ndefu na inataji moyo kuisimulia, hasa mama yako ngumu sana kukwambia, anajisikia uchungu sana pale alipo ila anavumilia ili kuhakikisha anakulea vizuri na kukupatia Elimu na kwa kuwa umeuitaji ukweli mimi nitakusimlia yale ninayoyajua ujue kila kitu kwa sababu mama yako ukimuuliza chochote kuhusu baba yako anaweza kufa kutokana na yaliyomkuta. Ila njoo kesho asubuhi ndiyo nitakuambia leo sikuambii.”
“Aaaaagh bibi kwa nini usinambie sasa  hivi? hujui kiasi gani nateseka bibi, nikishaujua ukweli hata nikiteseka poa tu, naumia kwa kuwa naona yanayonikuta kisha sijui chochote naomba unambie sasa hivi tu.” Nilisema.
 Alinipiga jicho la sekunde kadhaa kisha kuniuliza.
“Baba yako unamjua anaitwa nani?
Kiukweli lilikuwa ni swali gumu sana kwangu kwa sababu sijawai kuambiwa baba yangu anaitwa nani, kumbukumbu ambazo nilikuwa nazo ni kumbukumbu za jina la Sharif ambalo niliambiwa ni la babu yangu na ndiyo jina ninalotumia shuleni.
“Bibi! mama hajawai kunambia jina la baba yangu, tokea nlipoanza shule niliandikishwa kwa jina la Said sharif, nilipokuja kumuuliza sharif ndiyo jina la baba alisema la Babu.
“Ni kweli mjukuu wangu, Sharif ni babu yako,  Mwanangu najma hakuitaji utumie jina la baba yako kwa sababu anamchukia sana kwa vitendo alivyo mfanyia.
Bibi alitoa kikombe kilichokuwa juu ya jagi nikamsaidia kumimina maji ya kunywa. Alikunywa taratibu alipomaliza alirudishia kikombe, akasogea nyuma kidogo kwa ajili ya kuegamia kwenye mti, alitoa sauti ya “E, e, e, e akiashiria uchovu wa mgongo baada ya kuukalisha bila kuuegemesha sehemu muda mrefu, aliachia pumzi kisha akaanza kunipa ukweli kuhusu baba, huku na mimi nkikaa makini kumsikiliza.
“Mjukuu wangu, waswahili wanasema Usichokijua ni sawa na usiku wa kiza.
“Pia kilichoko nyuma ya pazia huwezi kukijua mpaka liondoshwe au uambiwe.”
Nilijikuta nadakia maneno yake, na kumbakiza akicheka.
“Kweli umekuwa inabidi unioe tu sasa hivi, alisema kiutani akaendelea kunipa stori…  nakumbuka ilikuwaaaaaa! Tarehe 05/02/1990 Wazee wa baba yako ambao ni babu zako, walipiga hodi kwenye nyumba yangu hii na kuleta barua ya kumuoa mama yako, kutokana  na mila za hapa kijijini kwetu niliipokea vizuri na mimi hapo nguvu bado zilikuwemo hata macho yangu yalikuwa mazima, niliisoma, nilipomaliza nikawauliza.
“Ni nani mmekuja kumtolea hii posa?
walijibu kwa kusema “mtoto wetu Suudy japo bado anasoma lakini anaitaji kuoa, na tumeona tuoe katika ukoo wako mama kwa sababu ukoo wako una heshima zote.
Mjukuu wangu mama yako ndiyo alikuwa amemaliza darasa la tisa, sikuweza kukataa, niliongea nao muda mrefu tukapanga mambo ya mahari, Najma mama yako nilimueleza akakubali na baada ya wiki mbili ndoa ikapita.
Masoudy ambae ndiyo baba yako mzazi. Wakati huo alikuwa amemaliza kidato cha sita anasubiri majibu yake.
Waliuanza ukurasa wa ndoa baada ya ndoa kupita na walikuwa wanapendana sana sana zaidi ya sana. kila mmoja aliiangalia ndoa yao kwa jicho la tatu kutokana na mapenzi mazito waliyokuwa wakioneshana.
wakienda shamba wanaenda wote, kisimani kuchota maji wote, sokoni wote, kiufupi kila sehemu.
Baba yako wapo waliomuita mume bwege kwa alivyokuwa akishugulika kumsaidia mama yako, mara anafua nguo na watu wanamuona, mimi mwenyewe niliwai kumkuta anaosha vyombo nilipomuuliza akasema namsaidia mke wangu kachoka leo, siku nyingine anapika, na kufanya vingine vingi kama kumsaidia mkewe.
katika shamba lao walipanda mpunga mwingi pamoja na mahindi, wakiamini vitawasaidia sana mbele kiuchumi.
Walifanya mengi ndani ya miezi michache ya ndoa yao, na kupata mafanikio mengi ambayo kila mtu wa hapa kijijini aliyatamani.
Baada ya miezi sita kupita. masoudy alipata furaha mpya katika maisha yake alipopata matokeo ya masomo na kukuta  alama zake ni za kuendelea, wiki kadhaa zilipopita  akajiunga na chuo cha Suza (University of Zanzibar).
Najma alimjali kwa kila kitu mumewe,
Masoudy unene ulianza kuuandama mwili wake kutokana na maanjumati  aliyokuwa akiyapata kwa mkewe na kumfanya aridhike. Ila alama ya kuuliza ilianza kupita pande zote mbili yaani kwangu na familia ya Masoudy baada ya kuona  mwaka umeisha wakiwa katika ndoa hata dalili ya Najma kubeba mimba haipo, ndipo kikao cha familia zote kilifanyika ikabidi tulazimike kuwaweka chini kuwauliza, walichotujibu ilitulazimu tuwe wapole na kuridhika kwa majibu yao.
“waliwajibu nini? Niliingilia tena maongezi ya bibi baada ya kuona sijaelewa vizuri.
“Swali zuri, walituambia wamepanga wasizae mpaka Masoudy amalize chuo.
Maisha yalisonga mbele, siku na miezi ikakatika, mapenzi yao yakionekana kuwa marudufu kila siku.
Mjukuu wangu! mwaka 1992 wakiwa tayari wana miaka miwili  ndani ya ndoa yao, lilitokea tukio ambalo sitolisahau katika maisha yangu yote ya duniani, na hicho ndiyo kitu ambacho nahisi Najma ataendelea kulaani juu ya babaako japo yapo mengi mabaya aliyomfanyia na Najma kuyavumilia, ila kwa hilo tukio! Kama baba yako atakaa siku moja chini na kulifikiria, basi naamini siku moja atarudi kwa mama yako akiwa amepiga magoti chini akiitaji msamaha, kwani ni wanawake wachache sana wanaweza kujitolea kwa jinsi alivyojitolea mwanangu Najma ili kuokoa maisha ya mumewe!

No comments