Header Ads

SITALIA TENA - 02


NYEMO CHILONGANI
Saida alikuwa kwenye wakati mgumu, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya. Ni kweli alikuwa kwenye mahusiano mazito na mwanaume ambaye hakuwahi kuonana naye, walijuana kwenye mitandao na kuweka uhusiano mkubwa, ukaribu uliokuwa ambao ulimfanya kila mmoja kuwa karibu na mwenzake.
Akaombwa kuwa mpenzi wake na hivyo kuolewa lakini bado kwake kulikuwa na mtihani mgumu. Alimpenda Kareem zaidi ya mwanaume mwingine yeyote yule, na hakuwa radhi kumuona akiondoka mikononi mwake lakini suala la kumkubalia na kuwa wapenzi, kwake ulikuwa mtihani mwingine mgumu.
Alikaa na kujifikiria kwa kipindi cha siku mbili na ndipo akamwambia Kareem kwamba alikubali kuwa mpenzi wake. Huo ndiyo ukawa mwanzo wa uhusiano wa kimapenzi baina ya watu wawili hao.
Mawasiliano yakachanganya na kila mmoja akamuona mwenzake kuwa muhimu katika maisha yake. Siku zikakatika huku mapenzi ya mtandaoni yakiendelea kunoga. Baada ya miezi sita mingine, Kareem akamwambia Saida kwamba alitaka kumfuata nchini Tanzania, aende akajitambulishe kwa wazazi wa msichana huyo.
Hilo halikuwa tatizo, Saida akawaambia wazazi wake. Kwanza wakashtuka, walishangaa, hawakuamini kile walichoambiwa na binti yao. Ilikuwa vigumu kumwamini mwanaume huyo kwani kulikwishawahi kutokea wanaume wengi ambao walianzisha uhusiano wa kimapenzi na wasichana kwenye mitandao lakini mwisho wa siku, kulikuwa na mambo mabaya yaliyowatokea.
“Una uhakika huyu ni mtu mwema?” aliuliza baba yake.
“Baba! Siwezi kulijibu swali hilo, ila nahisi ni mtu mwema kwani kwa jinsi tunavyowasiliana, anaonekana ni mtu mzuri sana,” alijibu Saida.
“Halafu yeye akija atataka na wewe uende kwao, ndiyo?” aliuliza mama yake.
“Ndiyo mama! Tumelizungumzia hilo pia. Ananipenda na ninaomba mumkubali,” alisema Saida.
“Mmh!”
“Nawaombeni jamani! Nataka niolewe na Kareem,” alisema Saida.
Kwa jinsi alivyokuwa akizungumza, machozi yalikuwa yakimlenga, moyo wake ulimpenda sana mwanaume huyo na hakuwa radhi kumuona akiondoka mikononi mwake.
Wazazi wake hawakuwa na jinsi, binti yao alipenda, tena kitu kizuri ni kwamba alimpenda mwanaume wa dini yake hivyo suala la kuoana halikuwa tatizo kabisa. Wakamkubalia na kumwambia kwamba huyo Kareem alikaribishwa kwenda Tanzania na kujitambulisha.
“Nashukuru sana,” alisema Saida.


“Usijali binti yetu. Ila utatakiwa kuwa makini! Hutakiwi kumwamini kila mtu kwenye mtandao,” alisema baba yake.
Saida akamwambia Kareem kilichokuwa kimetokea, ilikuwa ni furaha kwake na alimuahidi kwamba ndani ya wiki moja angekuwa nchini Tanzania. Hilo ndilo likafanyika, kama utani, Kareem akatua nchini Tanzania.
Kitendo cha kumuona Saida uwanja wa ndege kilimfurahisha, akamfuata na kisha kukumbatiana. Huyo ndiye alikuwa msichana wake, aliyempenda kwa moyo wa dhati na ndiye aliyemfanya kusafiri kutoka nchini Oman mpaka Tanzania kwa ajili yake.
“Karibu mpenzi! Siamini kama umekuja kuniona,” alisema Saida, alishindwa kuyazuia machozi yake.
“Nimekuja kwa ajili yako! Nyumbani wazima lakini?”
“Wazima!”
Wakaondoka na kwenda hotelini. Wakafika katika Hoteli ya Nyota Tano ya Caspean iliyokuwa Mikocheni B na kutulia huko. Wahudumu wa hoteli hiyo walipomuona Kareem, hawakuamini kama kwenye dunia hii kulikuwa na mwanaume aliyekuwa na sura nzuri kama alivyokuwa mwanaume huyo.
Kila mmoja alimpenda, walimuonea wivu Saida na kuona kama alikuwa mwanamke mwenye bahati kubwa, kuwa na mwanaume kama Kareem halikuwa jambo la kawaida hata kidogo.
Kareem akaenda kuoga huku akimwacha Saida chumbani. Alipomaliza, akatoka, akajifuta maji, baada ya dakika kadhaa, wote wakajikuta wakiwa watupu kitandani na ni sauti za mahaba ndizo zilizokuwa zikisikika chumbani humo.
Sauti hizo zilisikika kwa saa moja, wote wakainuka na kuelekea bafuni kuoga, baada ya hapo wakaondoka na kuelekea nyumbani kwa kina Saida.
“Ninatamani kuwaona wazazi wako, inaelekea ni watu wazuri sana mpenzi,” alisema Kareem huku wakiwa ndani ya teksi.
“Bila shaka utawafurahia, wao wenyewe wanatamani sana kukuona,” alisema Saida, hakutaka kuutoa mkono wake kwa Kareem.
Safari hiyo iliwachukua dakika thelathini, wakafika Magomeni Mapipa ambapo wakateremka na kuelekea ndani. Siku hiyo hata majirani walikwenda kwao kwani waliambiwa kuhusu Kareem, hivyo kila mmoja alitaka kumuona.
Kitendo cha kuingia tu, kila mmoja akaanza kupiga makofi. Kareem hakulizoea hilo, alishangaa lakini moyo wake ulikuwa na furaha mno kwani hakuamini kama angepokewa kiasi hicho.
Wazazi wakamfahamu siku hiyo, wakamkaribisha na kutoa baraka zote kwamba binti yao awe na mwanaume huyo. Kwa kuwa familia ya Saida haikuwa ya kitajiri na nyumba waliyokuwa wakiishi haikuwa nzuri, baada ya wiki moja kukaa nchini Tanzania, alichokifanya Kareem ni kuwanunulia nyumba nyingine iliyokuwa Mbezi Beach, nyumba kubwa na ya kifahari.
“Nitataka mke wangu aishi humu kwa sababu ni mkwe wa bilionea mkubwa,” alisema Kareem.
Ilikuwa ni bahati kubwa, maisha yake hayakuwa na mbele wala nyuma lakini ghafla yakabadilika na kuwa ya mtu fulani mwenye pesa nyingi. Kareem alipanga kuibadilisha familia hiyo kwa sababu tu alimpenda mno Saida.
Familia ikapewa hela nyingi na kufungua biashara. Wakatoka Magomeni Mapipa na kuelekea Mbezi Beach huku wakiyaendesha maisha yao huko. Kwa familia nzima, hawakuamini kilichokuwa kikiendelea, wakati mwingine walihisi kama maigizo ambapo baadaye ‘scenes’ zao zingeisha na kurudi Magomeni au kwenye ndoto ndefu nzuri na ya kusisimua na baadaye wangeamka na kujikuta wakiwa vitandani. Hiyo haikuwa filamu, haikuwa ndoto bali kilikuwa kitu halisi kilichokuwa kikiendelea.
Baada ya kukaa nchini Tanzania kwa wiki mbili, Kareem akaondoka na kurudi nchini Oman. Wakati huu baba yake hakutaka arudi na ndege ya abiria ila alichokifanya ni kumtumia ndege binafsi na kurudi nyumbani kwao.
Njiani, mawazo yake yalikuwa kwa Saida, alitokea kumpenda mno msichana huyo. Aliwahi kuwa kwenye uhusiano na wasichana wengine lakini kwa Saida, alikuwa tofauti, alikuwa msichana mwenye furaha mno, tabasamu pana ambaye alimjali kupita kawaida.
Hakutaka kuondoka, alitamani aendelee kubaki nchini Tanzania kwa kipindi chote kwani kuwa mbali na msichana huyo tayari ikaonekana kuwa kama mateso makubwa. Ndani ya ndege, kazi yake ilikuwa ni kuwasiliana na mpenzi wake kupitia WhatsApp. Kila mmoja alikuwa akimuonyeshea mwenzake jinsi alivyokuwa akimpenda.
“Hakika nitaishi na wewe mpaka kifo kitakapotutenganisha, na siku ya kufa, nitataka nife nikiwa mikononi mwako,” aliandika Kareem.
“Kama Romeo na Juliet...”
“Ndiyo mpenzi! Nitakupenda hata zaidi ya Romeo alivyompenda Juliet. Wewe ni mama wa watoto wangu, nisingependa kuona ukiteseka, katika maisha yako yote, nitakuwa nawe bega kwa bega. Nakupenda mpenzi,” aliandika Kareem.
Waliwasiliana mpaka ndege ilipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muscat nchini Oman ambapo akapanda ndani ya gari lililokuja kumchukua na kwenda nyumbani kwao.
Baada ya kulala siku hiyo, siku iliyofuata, Kareem akawaambia wazazi wake juu ya safari yake, aliwaambia namna alivyokutana na msichana huyo huko, alivyopokelewa mpaka kurudi nchini Oman.
Wazazi wake wakawa na furaha mno hivyo walichokihitaji ni msichana huyo afunge safari na kwenda Oman. Hilo halikuwa tatizo kabisa, baada ya wiki kadhaa, Saida akatumiwa tiketi na hivyo kupanda ndege kwa mara ya kwanza na kuelekea nchini Oman.
Alivaa kiheshima, juba jeusi huku kichwani akiwa amevaa ushungi uliozifunika nywele zake. Miguu yake hakuiacha wazi, alivalia soksi kwani alizijua sheria kali za nchi hiyo jinsi walivyokuwa wakikemea mwanamke kutokujisitiri.
Baada ya saa kumi na tano, akafika huko. Alipomuona mpenzi wake, Kareem, akamsogelea na kisha kusalimiana naye kwani alijua kabisa kwamba sheria za kidini za nchi hiyo zilikemea mambo mengi mpaka pale watu walipokuwa wameoana.
Kama alivyopokelewa Kareem nchini Tanzania ndivyo alivyopokelewa yeye nchini Oman. Wazazi wa mwanaume wake walifurahi kumuona na walimkaribisha kwa mikono miwili.
Kutokana na nchi hiyo kutotaka watu kujihusisha na mambo ya kimapenzi kwa kuishi pamoja na wakati hawakuwa wameoana, ilichokifanya familia hiyo ni kumtambulisha Saida kama mfanyakazi kutoka Afrika.
“Ila utatakiwa kuwa makini!” alisema baba yake Kareem.
“Hakuna tatizo baba!”
“Hutakiwi kufanya mapenzi na huyu msichana, si unajua unaweza kumpa mimba kwa bahati mbaya! Ukiona umempa mimba, jua kwamba atauawa kwa kupigwa mawe kama sheria yetu inavyosema,” alisema baba yake.


“Hicho kitu hakiwezi kutokea, siwezi kumpa mimba Saida.”
“Basi sawa. Nashukuru.”
Hicho ndicho alichokijua kwamba asingeweza kufanya mapenzi na Saida hivyo asingeweza kumpa mimba msichana huyo. Ukaribuni wao wa kimahaba ulikuwa ndani ya nyumba tu na wageni walipokuwa wakifika, ilikuwa ni vigumu kugundua kwamba watu hao walikuwa wapenzi kwa namna ambavyo walivyokuwa wakiishi, Saida alionekana kama mfanyakazi wa ndani nyumbani hapo.
Siku zikakatika na hatimaye wiki ya kwanza ikatimia. Hakukuwa na mabadiliko yoyote yale lakini kipindi hicho mwili wa Kareem ukaanza kumuhitaji msichana huyo. Alikuwa mpenzi wake na alikataliwa kufanya naye mapenzi, hakutaka kukubali tena kwani kila alipokuwa naye faragha, msichana huyo alimtamanisha kupita kawaida.
Alichokifanya ni kuanza kuelekea chumbani kwa Saida kila siku usiku. Hakukuwa na mtu yeyote aliyeligundua hilo, huko, walikuwa wakikumbatiana mpaka saa kumi alfajiri ambapo alikuwa akitoka na kwenda msikitini.
Hayo yakawa maisha yao, hakukuwa na siku ambayo Kareem hakuwa akitoka chumbani kwake, walifanya sana mapenzi kisiri, wazazi hawakugundua kitu chochote kile, hawakujua kwamba kila siku watu hao walikuwa wakikutana chumbani kitandani na kufanya mapenzi walivyotaka.
Baada ya mwezi mmoja kutimia tangu Kareem aanze kuelekea chumbani humo, hali ya Saida ikaanza kubadilika. Mwili wake ukaanza kuchoka, kichefuchefu kikamshika na hatimaye kuanza kutapika.
Mara ya kwanza walichukulia ni tatizo la kawaida ila baada ya kuendelea kutokea mara kwa mara Kareem akahisi kwamba mpenzi wake alikuwa na mimba. Akamchukua na kuanza kuzungumza nayye pembeni, alitaka kujua ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea.
“Unasemaje?” aliuliza Kareem kana kwamba hakusikia aliambiwa nini.
“Nina mimba mpenzi! Mimba imeanza,” alisema Saida, hapohapo Kareem akakaa chini. Hakuamini alichoambiwa.
“Unasema kweli?”
“Ndiyo!”
“Mungu wangu! Tumekwisha..” alisema Kareem huku kijasho chembamba kikianza kumtoka.
Aliikumbuka vilivyo adhabu ya kifo waliyokuwa wakihukumiwa watu wengine mara baada ya kupewa mimba. Hakutaka kuona hilo likitokea kwa msichana aliyekuwa akimpenda, tena aliyekuwa na mtoto wake tumboni.
Ilikuwa ni rahisi kumwambia Saida aondoke na kurudi nchini Tanzania lakini ugumu uliokuwepo ni kwamba kulikuwa na sheria ya kuwapima mimba watu wote waliokuwa wakitaka kuondoka nchini humo kwani kabla ya hapo, wengi walikimbia nchi hiyo baada ya kuona kwamba walikuwa wajawazito kwani mbali na kupima, kwa wale waliokuwa wameolewa, walitakiwa kuonyesha vyeti vyao vya ndoa kujua kama walikuwa ndani ya ndoa.
“Kwa hiyo?” aliuliza Saida huku akionekana kuogopa.
“Sijajua! Saida, ninachohofia ni kwamba utauawa kwa kupigwa mawe tu,” alisema Kareem huku akionekana kuwa na hofu moyoni mwake.
“Haiwezekani! Ni lazima niitoe.”
“Utaitoaje? Ukienda hospitali, daktari haruhusiwi, na akijua una mimba, kitu cha kwanza kitakuwa ni kuitaarifu serikali. Saida, nimechanganyikiwa,” alisema Kareem maneno yaliyomfanya Saida kukata tamaa ya kurudi nchini Tanzania, iwe isiwe ilikuwa ni lazima kuuawa kwa kupigwa mawe.

Je nini kitaendelea?

No comments