Header Ads

TATHMINI YAKINIFU KUELEKEA PAMBANO LA SIMBA NA YANGA KESHO

Na Ahmada Mwariko
Ukiwa umesalia usiku mmoja tu kuelekea  mpambano wa watani wa jadi katika ligi kuu soka ya Tanzania Bara homa ya mpambano wa Simba na Yanga inazidi kupamba moto huku kila upande ukitoa tambo kuwa wataibuka na ushindi.

Bila ubishi pamabano hili ni miongoni mwa Derby kubwa kabisa barani Afrika linalovuta hisia za mashabiki wengi hata wale ambao si mashabiki wa mpira lakini mwisho wa siku hutaka kujua matokeo ya mwisho ya mpambano huo.

Safu hii inakuletea tathmini ya mpambano huo kuanzia safu ya ulinzi mpaka ushambuliaji.

NAFASI YA GOLIKIPA
Agban vs Mustapha
Katika nafasi hii bila shaka Mustapha anaonekana kuwa na kiwango kizuri kuliko Agban, mpaka sasa ameruhusu goli 1 tu tangia ligi ianze huku Agban akiwa amesharuhusu magoli 2, japo hiyo haitoshi kumpa credit Mustapha au Agban lakini makosa ya mara kwa mara yanayofanywa na Agban akiwa golini kama ya kuwa na maamuzi yasiyo na uhakika wakati anakwenda kucheza mpira, kutema mipira hovyo na sio mzuri kwenye kucheza krosi, endapo udhaifu huu utajitokeza basi goli la Simba halitakuwa Salama.
NAFASI YA ULINZI
Hapa tathmini inaonyesha Timu zote kuwa na ukuta bora lakini swala la uzoefu linaweza kuleta tatizo kwa upande wa Simba kwani wana maingizo mapya katika safu hiyo ambayo ni kwa mara ya kwanza wanacheza katika pambano la kesho
Beki ya Yanga inayoundwa kwa sasa na Bossou na Dante imekuwa imara na haipitiki kirahisi na mpaka sasa ikiruhusu goli 1 tu, Mwinyi Haji anaitendea vyema nafasi ya ke ya ulinzi wa kushoto huku Juma Abdul akisimama vyema upande wa kulia na hawa ni miongoni mwa mabeki wanaopandisha mashambulizi mara kwa mara.

 Kwa upande wa beki ya Simba muunganiko wa Mwanjale na Lufunga umekuwa ukitumika zaidi na kocha Omong na umeonekana kutoa matunda mazuri japo bado akipangwa Mwanjale na Juuko wanaweza pia kumaliza shughuli pale katikati, mwajale ameonekana kuwa mpambanaji na anacheza kwa kujituma na bila shaka kesho Donald Ngoma atakuwa chini ya Ulinzi wa Mzimbabwe mwenzake.

SEHEMU YA KIUNGO
Nafasi hii ni dhahiri kabisa Simba imeimeza Yanga kwa kuwa na mafundi wengi kuliko wenzao wa Yanga. Simba wanachagizwa na viungo wengi vijana ambao wanacheza kwa nguvu na wajanja zaidi ya wale wa Yanga ambao kwa kiasi kikubwa wanamtegemea Kamusoko katika eneo hilo na endapo atazidiwa basi ni dhahiri hali itakuwa mbaya kwa upande wa Yanga

Mpira wa sasa unategemea sana safu ya kiungo kupandisha Timu na kutengeneza nafasi za kufunga..Roation ya kikosi kwa Timu ya Simba kutaisaidia kufanya vyema katika safu hii.

NAFASI YA USHAMBULIAJI
Yanga wamekuwa na safu bora ya ushambuliaji ikiongozwa na Amis Tambwe na Donald Ngoma huku ikichagizwa na Simon Msuva, wameskuwa ni wepesi kufanya maamuzi kwenye lango la mpinzani na katika msimu uliopita Tambwe na Ngoma walifanikiwa kuwafunga Simba katika mechi zote za ligi walizokutana na tayari safu hii imeshafunga magoli 8.

Kwa upande wa Simba ni kama hawatabiriki yani hujui nani wa kuchunga zaidi, vijana kama Kichuya na Mnyate wamekuwa moto wa kuotea mbali wakati unaendelea kumchunga Ajib na Mavugo vijana hawa wanawez kukudhuru wakati wowote, wamekuwa na jitihada binafsi kutafuta magoli kwa hivyo safu ya ushamuliaji wa Simba imejaa vipaji na haitabiriki nani atafunga wachezaji wote wanne pale mbele wamekuwa hatari langoni mwa wapinzani tayari safu hii imeshafunga magoi 12.

MAJUMUISHO
Ukomavu na uzoefu wa wachezaji wa Yanga unaweza ukawa chachu ya ushindi katika mechi ya Kesho lakini uchovu wa kucheza mechi nyingi bila kupumzika na kutokuwa na Rotation ya Wachezaji katika kikosi cha Yanga inaweza kuwagharimu na kupoteza mchezo huo.

Uchanga wa kikosi cha simba na ugeni wa mpambano huu kunaweza kuigharimu timu ya Simba na kupoteza mchezo lakini utimamu na utimilifu wa vipaji walivyonavyo wachezaji wengi wa Simba, Rotation ya wachezaji wanayoifanya katika mechi walizocheza inaweza kuwa chachu ya ushindi katika mchezo huo.
 Mwisho wa siku dakika 90'' ndio zitaamua nani ni nani kati ya Simba na Yanga

No comments