Header Ads

TFF yapata buku mbili mgao Ligi Kuu Bara


HIVI karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipigwa na butwaa baada ya kupata mgao wa Sh 2,000 tu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliozikutanisha African Lyon na Mbao FC, Uwanja wa Uhuru, Dar.


Habari za kuaminika kutoka ndani ya TFF, zilidai kuwa katika mchezo huo uliopigwa Septemba 12, mwaka huu na Lyon kuibuka na ushindi kwa bao 3-1, mapato yaliyopatikana yalikuwa ni chini ya Sh 50,000.
“Baada ya kufanyika kwa mgawanyo wa mapato ambao ulifanyika kwa kukata asilimia 18 ya Vat zilibakia fedha kidogo ambazo pia ziligawanywa pande zote zilizokuwa zikihusika na mchezo huo.


“Asilimia 15 ya fedha hizo zilizokua zimebakia baada ya kukatwa Vat, zililipia uwanja, asilimia nane zililipia gharama ya mchezo, asilimia tano zilienda TFF, asilimia tisa zilienda Bodi ya Ligi, asilimia tatu zilienda FA, asilimia 40 ya fedha hizo ilichukuliwa na African Lyon na asilimia 20 ilichukuliwa Mbao FC.


“Kutokana na mgawanyo huo TFF iliambulia shilingi 2,000 tu, huku Mbao FC wakiondoka na fedha kiduchu ambayo haizidi hata Sh 10,000,” kilisema chanzo hicho cha habari.


Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo Ofisa Habari wa TFF, Alfred  Lucas alisema: “Ni kweli katika mchezo huo mapato yalikuwa kidogo sana lakini hizo zote ni changamoto ambazo tumekuwa tukikumbana nazo, hivyo viongozi wetu wanaposema shirikisho halina fedha inabidi tukubaliane na ukweli.”

No comments