Header Ads

Wakali hawa watabaki Kibongobongo sana ni Jux, Ben Pol, Nay na wengine wengi

MUZIKI wa Bongo Fleva kwa miaka ya hivi karibuni umekuwa na mafanikio makubwa kiasi kwamba kwa baadhi ya wasanii umekuwa ni ajira rasmi inayowafanya kupiga mkwanja mrefu na hata kuajiri wasanii wenzao pamoja na vijana wengine wanaotafuta mkate wao wa kila siku. Mbali na mafanikio hayo na kuwa chimbo la kutengeneza mkwanja, muziki huu umekuwa na ushindani mkubwa, ndiyo maana wasanii kila kukicha wanakomaa kuandaa kazi nzuri na bora, ikiwemo audio na video ili ziweze kuchezwa mpaka kwenye vituo vya nje, tena vikubwa kabisa na kuonekana ulimwenguni kote. 

Hiyo ndiyo sababu akina Joh Makini, Diamond Platnumz, Ali Kiba, Vee Money na wengine wengi wanaofanya vizuri wamewashirikisha akina Chidinma, A.K.A, KO, Mr Flavour, Davido, P Square na wengine wengi wenye majina makubwa ili tu kufanya kazi zao zipenye zaidi nje ya mipaka ya Bongo, Afrika Mashariki na Kati hata kutikisa Afrika Magharibi na ughaibuni kwa jumla. 

Kwa wapenzi wa burudani watakumbuka moja ya vitu vilivyompa sifa AY ilikuwa ni kutoka na kutafuta wasanii wakubwa wa kufanya nao kazi akiwemo Sean King Stone, jambo lililomfanya pia kuwa miongoni mwa wasanii wa mwanzo kabisa kutoka Afrika Mashariki kuorodheshwa kwenye baadhi ya tuzo kubwa.
 
 Pamoja na jitihada hizo, lakini vipi kwa wasanii hawa? Kwa nini wamekubali kuwa wa hapahapa? Wengine wana zaidi ya miaka mitano kwenye gemu na wanafanya vizuri Bongo, kwa nini hawasogei? Kiukweli kwa mwendo walionao watasugua sana. 

BELLE 9 
Mpenda burudani gani asiyemjua mkali huyu kutoka Moro kutokana na kipaji alichonacho? Kiukweli jamaa anajua sana na wapo watu wengine hufikia hatua ya kusema hakuna kama yeye Bongo kwa upande wa wasanii wa kuimba. Kwa upande wa kolabo, Belle 9 amefanya nyingi sana za ndani na amekuwa daraja la mafanikio kwa baadhi ya mastaa wanaomshirikisha ili kukuza majina yao. Vipi kwa upande wake, kwa nini anashindwa kutafuta watu wa nje wanaomzidi ‘status’ na kupiga nao kazi ili wamsogeze mbele zaidi? Kila mara amebaki kuwa mtu wa ahadi tu kuwa atafanya kazi za kimataifa lakini utekelezaji unakuwa ziro.

 BEN POL 
Kolabo yake kubwa ya nje, Ben Pol amefanya na wasanii kutoka Kenya, Avril na Nameless, kama kuna nyingine basi zitakuwa kapuni. Kwa upande wa uwezo, ukweli ni kwamba Ben Pol ana uwezo mkubwa sana ndiyo maana amefanya kazi na wasanii wengi wakubwa Bongo. Lakini ndiyo hivyo tena, bado kwa wasanii waliotusua na wenye mafanikio, jamaa anaonekana ‘underground’ kwa sababu tu, hajajichanganya na kuupeleka muziki wake kimataifa. 

BARNABA 
Ni kati ya wasanii wenye muda mrefu kwenye gemu la muziki Bongo maana anakaribia kufikisha miaka kumi akifanya Bongo Fleva. Kwa waliomfuatilia kuanzia mwanzo, watakubaliana nami kuwa Brnaba wa Wimbo wa Njia Panda si huyu wa sasa, kila mara uwezo wake umekuwa ukipanda na kufanya ngoma kali zinazopendwa na kila mtu
Bongo. 


Ni miaka kadhaa tu iliyopita, mwanamuziki wa dansi mwenye jina kubwa ulimwenguni, Fally Ipupa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) alipokuja Bongo alisifia uwezo wake na kuhitaji kupiga naye kazi lakini uongozi wake ukambania. Pamoja na kufanya kazi na Jose Chameleone wa Uganda lakini Barnaba amebaki kuwa wa hapahapa na ukweli ni kwamba kama anahitaji kupiga hatua zaidi ya hapo alipo anatakiwa kujitengenezea ‘network’ ya mashabiki, ikiwemo kupiga kolabo na wasanii wakubwa kutoka nje ili tu, apate mashabiki wapya watakaomsikiliza kupitia wasanii atakaofanya nao kazi. 

NAY WA MITEGO 
Kwa upande wa muziki wa kibiashara, jamaa anajua. Amefanya mengi kwenye gemu la Muziki wa Bongo Fleva, amerap na kuimba mpaka Mchiriku ili tu kuonesha kuwa muziki kwake mbali ya kuwa ni kazi lakini anauweza. Hata hivyo, mafanikio ya Nay yameishia kugota kwenye kingo za kuta za Afrika Mashariki, amebaki kuwa mtu wa maneno kuwa atafanya kolabo na wasanii wakubwa lakini hatimizi ahadi. Kiukweli kwa mtindo huu, Nay atasugua sana na anafeli kwa sababu ili kufika mbali ni lazima afanye kazi na wasanii ambao watamtanulia ‘fun base’ yake.

 JUX 
Hayuko mbali na wasanii waliowekwa kwenye orodha hii, jamaa anaweza muziki. Wimbo wake wa Wivu unafanya vyema kwenye media na ni kama wimbo wa taifa kwa akina dada wengi.  Kwa namna moja au nyingine unaweza kusema Jux tayari soko la muziki Bongo analo mkononi na ili kufanikiwa zaidi ya hapo alipo, anatakiwa kufanya kitu cha ziada ambacho hajawahi kufanya, mojawapo ikiwa kupiga kolabo na wasanii wa nje ili kumtengenezea jina zaidi. Mbali na hivyo, wasanii hawa wote wataendelea kusugua na kuwa wasanii wa ndani tu na kushindwa kutikisa kimataifa.

No comments