Header Ads

YANGA YAIPIGA BAO SIMBA, KOCHA WA SAMBA YANGA WATABEBA UBINGWAYANGA imeipiga bao Simba kiulaini kabisa na kocha wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm amechekelea kwa kusema, msimu huu atabeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwani ana kikosi kipana.

Iko hivi, Simba imecheza mechi mbili za ligi kuu na kushinda moja kisha ikatoka suluhu nyingine, hivyo ina pointi nne wakati Yanga imecheza moja tu na kushinda.
Katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Simba ilishinda mabao 3-1 wafungaji wake wakiwa ni Laudit Mavugo, Fredric Blagnon na Shiza Kichuya.

Kwenye fowadi ya Simba, Mavugo raia wa Burundi, Blagnon wa Ivory Coast na Mtanzania Kichuya ndiyo tegemeo kwa sasa, lakini hawakuweza kufurukuta katika mechi iliyofuata dhidi ya JKT Ruvu.

Kocha wa Simba, Joseph Omog aliwaanzisha Mavugo na Blagnon dhidi ya JKT Ruvu, lakini hawakuweza kufurukuta hadi akasalimu amri na kumtoa Blagnon kisha kumuingiza Ibrahim Ajib ambaye hata hivyo hakuweza kuisaidia timu yake kupata bao.
Baada ya Simba kucheza mechi mbili na kufunga mabao matatu na kufungwa moja, imeonyesha wazi kwamba Omog raia wa Cameroon ana kazi ngumu ya kufanya ili aweze kufanya vizuri katika mechi zinazofuata ikiwemo dhidi ya Yanga Oktoba Mosi, mwaka huu.
Awali ilionekana wazi Omog ana imani na ‘kombinesheni’ ya Mavugo na Blagnon, lakini kushindwa kufurukuta kwao mbele ya JKT Ruvu, kumemfanya abadili mambo kidogo kikosini.

“Baada ya sare ile nimewaambia wachezaji wapambane kuhakikisha tunashinda mechi zetu zilizobaki za nyumbani ili tuwe katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa,” alisema Omog.
Katika mazoezi ya Simba kabla ya kwenda Dodoma, Omog alionekana akiwasisitiza wachezaji wake kucheza soka la pasi na kuepuka kupiga chenga zisizo na msingi pia akikataza pasi za kurudi nyuma.
Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi nne katika mechi mbili, ina mabao matatu na imefungwa moja, Azam FC ipo kileleni ikiwa na pointi nne pia lakini ina mabao manne na imefungwa bao moja. Yanga ni ya sita ikiwa imecheza mechi moja na ina mabao matatu, haijafungwa.

PLUIJM ANACHEKELEA
Hali ni tofauti kwa Yanga, kwani Kocha Pluijm anaonekana kuchekelea kwa kusema: “Wanaotubeza kutolewa kwetu Kombe la Shirikisho Afrika, watakoma na tutafanya vizuri kwenye ligi kuu.”

Pluijm aliongeza: “Sitegemei mchezaji mmoja au wawili katika ufungaji hata nafasi yoyote ile, vijana wangu wamechoka lakini nimeweka mzunguko maalum wa kucheza ili wengine wapumzike.”
Katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilishinda mabao 3-0, wafungaji wakiwa Deus Kaseke, Simon Msuva na Juma Mahadhi.

Tegemeo kubwa la ufungaji kwa Yanga lilionekana kuwa kwa Donald Ngoma na Amissi Tambwe, hata hivyo hawakuweza kufunga mbele ya African Lyon. Pia beki ya kati ya Yanga, haikuwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani badala yake walicheza Andrew Vincent ‘Dante’ na Vincent Bossou. 

“Nina kikosi kipana sana, tazama wamefunga Kaseke, Msuva na Mahadhi, hawa walipata nafasi wakafanya vizuri pia Ngoma na Tambwe wana uwezo huo.
“Ikipigwa kona utaona nimewandaa Dante na Bossou kupiga vichwa ili wafunge pia Ngoma na Tambwe, hiki ni kikosi kipana sana, kumbuka nina Cannavaro na Kelvin,” alisema Pluijm, raia wa Uholanzi.

UGUMU KWA OMOG
Ukiwatoa Ngoma na Tambwe, Yanga ina mastraika wengine ambao ni Malimi Busungu na Matheo Anthony, hao wanaweza kucheza na kina Msuva na mambo yakaenda.
Simba ukiacha Mavugo na Blagon inaweza kuwatumia Ajib na Danny Lyanga, ambao bado inaonekana kocha hajawaamini kuwatumia kwa pamoja kikosini.
Tayari Yanga inao Dante na Bossou katika beki ya kati wanaocheza nafasi za Cannavaro na Yondani, Simba mambo bado kwani sasa wanacheza Novalty Lufunga na Method Mwanjale raia wa Ivory Coast, ukiwatoa hao anaweza kuwatumia Emmanuel Semwanza na Juuko Murshid.

Omog anajenga kikosi, hivyo hajawahi kuwatumia kwa pamoja Murshid na Semwanza aliyetokea Mwadui FC. “Bado naendelea kutengeneza kikosi changu na kombinesheni ya ushambuliaji haijakaa sawa, hata ile ya beki ya kati haijakaa sawa,” alisema Omog.
Habari zinasema, kuna uwezekano mkubwa kwa Murshid kurejeshwa kikosi cha kwanza ili acheze na Mwanjale.

No comments