Header Ads

CCM ina mkono sakata la mgawanyiko CUF

DAR ES SALAAM: Wakati  sakata la mgawanyiko likiendelea kushika kasi katika Chama cha Civic United Front (CUF) baina ya mwenyekiti aliyejiuzulu ambaye sasa anataka kurejea katika nafasi yake, Profesa Ibrahim Lipumba na Baraza la Uongozi la chama hicho, minong’ono imesambaa mitandaoni kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kina mkono wake. Katika mitandao mbalimbali ya kijamii, wachangiaji wengi wanaozungumzia suala la kujiuzulu na kurejea kwa  Profesa Lipumba, wanasema kiongozi huyo mchumi, anatumiwa na CCM ili kupunguza nguvu za upinzani, hasa kupitia umoja wao wa Ukawa. 
 
KUTOKA MITANDAONI 
Katika mitandao hiyo, kumekuwa na mijadala mingi kuhusu sakata hilo, wengi wakiamini kuondoka kwa Profesa Lipumba katika nafasi yake mwaka jana, kulichagizwa na ushawishi wa chama tawala, hasa baada ya kuwepo kwa dalili za kuimarika kwao, baada ya kujiunga na upinzani kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Wachangiaji hao walihoji iweje mchumi huyo atake kurudi katika nafasi yake, wakati sababu alizotoa wakati akijiuzuru zikiwa bado zipo. “Profesa aliondoka Cuf kwa sababu ya kupinga kupokelewa kwa Lowassa (Edward), lakini mbona huyu bwana bado yupo? Ina maana akirejea anataka afukuzwe? Sasa kama siyo kutumika ni kitu gani,” alihoji mchangiaji mmoja katika mtandao mmoja maarufu. Mchangiaji mwingine alisema chama tawala kiliamini baada ya kuondoka kwa Lipumba na aliyekuwa
 

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa, upinzani ungekosa nguvu, lakini kwa kuwa bado ni tishio, CCM imeamua kumtumia kiongozi huyo ili kuuvuruga Ukawa. “Ukitazama mazingira yote ambayo yapo nyuma ya madai ya Lipumba kutaka uenyekiti wake, unaona kabisa baraka za CCM. Tangu lini mtu aliyeandika barua ya kujiuzulu akataka nafasi yake, tena baada ya mwaka mzima kupita?” alihoji mchangiaji mmoja anayejiita Jobson katika Mtandao wa Facebook. Hata hatua ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kutoa waraka wenye kuonesha uhalali wa Profesa Lipumba katika nafasi yake ya uenyekiti, unaelezwa na wachangiaji hao kuwa ni mwendelezo wa kutumika kwa chama tawala kuhakikisha kinakivuruga chama hicho ambacho ni cha pili kwa ukubwa visiwani Zanzibar. 

UWAZI KAMBI YA LIPUMBA Ili kupata maelezo ya kina juu ya madai hayo, Uwazi lilimtafuta Profesa Lipumba kwa siku mbili mfululizo kupitia simu yake ya mkononi, lakini mara zote, iliita bila kupokelewa.
Baadaye lilifanikiwa kumpata Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano, Abdul Kambaya ambaye pia amesimamishwa uanachama na Baraza la Uongozi la chama hicho.


 KUHUSU YEYE KUSIMAMISHWA “Hilo halinipi tabu kwa sababu tunachofanya sisi ni kufuata katiba ya chama na siyo utashi wa mtu. Sisi tunaheshimu maamuzi ambayo tayari yameshafanywa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania. “Tunachokataa ni kuwa uamuzi batili unabaki kuwa batili hata kama utachukuliwa na kikao halali. Kikao kilichofanyika Zanzibar ni halali, lakini maamuzi yaliyochukuliwa ni batili.

” KWAMBA PROFESA LIPUMBA ANATUMIWA NA CCM? “Ukisema Profesa Lipumba anatumiwa na CCM, je Chadema wanatumiwa na nani? Kwa sababu unaona sasa hawa jamaa wanazungumza mambo ya Cuf kitu ambacho siyo sahihi. “Ukisema Chadema wanazungumza kwa sababu ya Ukawa siyo kweli, Ukawa siyo chama, mbona wao walipomfukuza Zitto (Kabwe Zuber)
mbona hata siku moja sisi hatukuwahi kumzungumzia? “Kama wanasema Profesa Lipumba anatumika, mbona katibu hakumzuia asiingie ukumbini wakati wa mkutano mkuu wa Agosti 21 pale Ubungo Plaza? Angesema pale kuwa huyu amechukua hela na anatumika na wapinzani wetu, mbona hakusema? “Wao ndiyo wanatumiwa na Chadema, ndiyo maana unaona leo mambo ya Cuf yanazungumzwa na Mbowe (Freeman), Lissu (Tundu), Mbatia (James) na wengine. Wao ndiyo wamekuwa wasemaji wa Cuf Zanzibar. “Haya mambo yalitakiwa yajadiliwe ndani ya vikao vyetu vya ndani, sasa kama kuna mtu anasema profesa anatumiwa na CCM, mtu huyo anatakiwa athibitishe maneno yake, vinginevyo ni upuuzi.


” UWAZI KAMBI YA CCM 
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye alipoulizwa na mwandishi wetu juu ya madai hayo alikuwa na haya ya kusema: 

“Mwaka jana mwandishi uliponiuliza nini maoni yangu kuhusu Ukawa nilikuambia kwamba nawatahadharisha wapinzani kuwa hilo ndilo litakuwa kaburi lao. “Baada ya habari ile kutoka katika gazeti lako nilianza kurushiwa maneno mengi nikiambiwa mimi siyo mtabiri lakini leo mambo ni yale yale niliyoyasema yanatokea na nakwenda mbele zaidi kwa kuwaambia kuwa siyo Cuf tu,  bali Ukawa ni kaburi la Chadema pia. 

“Chadema itafia humohumo Ukawa na Cuf pia kaburi lao ni Ukawa. 

Nilifafanua kuwa Ukawa  siyo chama, hivyo hawawezi kuwa kitu kimoja hata mara moja, wasitatufe mchawi. 

“Niwaambie tu kwamba migogoro yao wasituhusishe sisi CCM kwa sababu tuna kazi nzito ya kuhakikisha tunatekeleza ahadi zetu kwa wananchi waliotuchagua na ndiyo kazi ambayo tunaifanya kwa sasa. 

CHANZO: UWAZI GAZETI

No comments