Header Ads

Mtu Hatari Adaiwa Kuuwa Watu Hadharani Dar!

DAR ES SALAAM: Ni tukio la kutisha! Mwanaume anayesemekena kuwa ni hatari kwa kuua watu hadharani, Salim Salum Mpepe maarufu kwa jina la Scorpion, anadaiwa kutekeleza jaribio la mauaji ya mfanyabiashara aliyetambuliwa kwa jina la Said Ali kufuatia kumchoma visu sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kumtoboa macho na kumwachia kilema cha maisha cha upofu. Tukio hilo la kushangaza huku kumbukumbu zikidai kuwa, Scorpion amewahi kufanya vitendo kama hivyo siku za nyuma, lilijiri hivi karibuni maeneo ya Buguruni –Sheli jijini hapa. 

ANA KWA ANA NA MANUSURA 
Katika mahojiano ya ana kwa ana na Wikienda akiwa nyumbani kwa mama mkwe wake, Mabibo Hostel, Dar, mfanyabiashara huyo ambaye ni manusura wa kifo kutoka kwa Scorpion, alisimulia mkasa mzima wa tukio hilo la kutisha lililojiri maeneo hayo kwenye njiapanda ya Buguruni –Kwamnyamani. Kwa mujibu wa maelezo ya Said, Scorpion ni mtu hatari ambaye alielezwa kuwa anaogopwa kutokana na historia ya matukio ya mauaji aliyowahi kuhusishwa nayo mara kwa mara jijini Dar. Huku akiugulia maumivu, Said alisimulia: “Kama sijakosea ilikuwa wiki mbili zilizopita, nilikuwa nikitokea kazini kwangu maeneo ya Tabata-Senene (Dar). Ilikuwa muda wa saa nne na nusu hivi usiku.


” ANGECHEZWA NA MACHALE ANGESHTUKA! “Mimi naishi Ubungo-External (Dar). Hakukuwa na daladala hivyo nilichukua bodaboda, nikaelewana naye anipeleke hadi Tabata-Relini ili nikifika pale nichukue daladala za Ubungo nishuke External, niingie nyumbani. “Yule dereva wa bodaboda aliniambia sehemu rahisi ya kupata daladala ni BuguruniSheli, nilimkatalia lakini baadaye alipolazimisha nilimkubalia. 

“Kweli, alinishusha pale Buguruni-Sheli na nikamalizana naye. Hapo ndipo tatizo langu lilipoanzia na kama machale yangenicheza tangu awali kwenye bodaboda, ningeshtuka na kuamua kwenda Tabata Relini, nisingekutana na Scorpion. “Pale Buguruni, kuna sehemu panauzwa kuku hivyo niliona
nichukue kitoweo hicho kwa ajili ya familia yangu. Nilisogelea eneo hilo ambapo kila muuza kuku aliniitia kwake lakini nilikwenda kwa mmoja. Akaniambia kuku ni shilingi elfu saba. Nilimwambia nina elfu sita hivyo nilimpa shilingi elfu kumi na moja ili anirudishie elfu tano kamili.


” SCORPION HUYU HAPA! “Dakika chache kabla ya kuletewa kuku na chenji nilishtuka nyuma yangu kuna mtu amesimama ananiongelesha begani. Alikuwa akiniomba nimsaidie kwani ana shida. Sikujua kama ni mtu hatari, hivyo nilimwambia aseme shida yake haraka. “Cha kushangaza, wale wauza kuku na akina mama wanaouza vyakula walikuwa wakiniangalia sana na nilijiamini kuwa, hakuna mtu anayeweza kuniibia kwa sababu kulikuwa na watu wengi.

” KISU CHATUMIKA “Kabla hajasema shida yake, ghafla nilishtuka amenichoma kisu hapa begani (akionesha sehemu aliyochomwa). Kabla sijageuka akanichoma tena kingine mgongoni kisha alipitisha kisu kwa mbele akawa ananichomachoma nacho tumboni. “Niliomba msaada kwa watu wengi waliokuwa wakishuhudia nikichomwa visu na bisibisi pia, lakini hawakunisaidia wala kunisogelea kwa maelezo kwamba jamaa anaogopeka na atakayesogea atauawa.

” MACHO YA MWISHO “Baadaye nilianguka, nikawa natokwa damu nyingi. Lakini kabla sijapoteza fahamu na kutobolewa macho, nilimtazama jamaa huyo. Ni mrefu na mwenye mwili kama baunsa. Nasikia alikuwa bausa wa baa maeneo ya Kimboka (Buguruni). “Alichokifanya ni kunisachi, akachukua shilingi laki tatu kwenye waleti na nyingine lefu ishirini nilizokuwa nazo mfukoni. Kisha alikata cheni yangu shingoni na mkononi. Hapo nilijua amemaliza lakini bado aliendelea kunichoma visu na bisibisi huku watu wakishuhudia!” 

AMBURUZIA BARABARANI AKANYAGWE NA GARI 
“Baadaye aliniburuza hadi barabarani na kuongoza magari yanikanyage ili nife. Nadhani lengo lake apoteze ushahidi kwani inasemekana ndiyo kawaida yake. Kwa bahati nzuri waliokuwa na magari
waligoma kutii agizo lake la kunikanyaga hivyo alinitoa pembeni, akachomoa tena kisu na kuanza kunichoma machoni nikiwa nimelala chali. “Kwa kweli maumivu niliyoyapata ni makali sana. Sitaki hata kukumbuka. Siamini kama kuna binadamu hawamjui Mungu kiasi kile. Lakini mimi naamini Mungu alimuona Scorpion! “Kufikia hapo Scorpion aliondoka, nadhani aliamini amemaliza kazi yake ya kuniua. Huku nyuma, mimi nilipoteza fahamu. Nilipokuja kuzinduka nikasikia sauti ya mtu kwa mbali akiniuliza nimepatwa na nini! Nilimjibu nimevamiwa na kuchomwa visu.


” WENGINE WASEMA NI FUMANIZI “Sasa wakati msamaria mwema huyo akinihoji, nilimsikia mtu mwignne akisema eti nimefumaniwa, nikasema sijafumaniwa. Watu wote hao wawili nilikuwa siwaoni kwa sababu nilishatobolewa macho. “Huyo mtu ambaye si mwenyeji wa eneo lile alikuwa mpita njia, ndiye aliyeshirikiana na watu wengine kuchukua simu yangu ambayo Scorpion aliiacha na kuanza kuwasiliana na ndugu zangu kuwapa taarifa.

” AFIKISHWA KITUO CHA POLISI “Baadaye walinipeleka Kituo cha Polisi Buguruni, nikaandikiwa PF-3 kisha wakanipeleka Hospitali ya Amana. Pale ishu ilionekana ni kubwa hivyo nikatafutiwa Ambulance na kukimbizwa Hospitali ya Muhimbili. “Muhimbili walinipa matibabu, ikiwemo kufanyiwa operesheni kuona kama kisu kilibaki ndani. Walipomaliza nililazwa siku kadhaa kabla ya kuruhusiwa na kuja hapa.

” HABARI MBAYA KWAKE NI HII “Lakini habari mbaya ni kwamba, madaktari pale Muhimbili waliniambia kuwa mishipa ya macho inafanya kazi lakini macho yaliharibika kabisa na hayataona tena! Niliwauliza kama kuna uwezekano wa kuwekewa macho ya bandia, wakasema wanaweza kuniwekea lakini bado hayataona. “Pia niliporuhusiwa Muhimbili, nilikwenda Hospitali ya CCBRT (Msasani),
nikapimwa lakini nako waliniambia sitaweza kuona tena! Yaani mimi nimekuwa kipofu hivihivi jamani. Mtu wa mwisho kumwona na ufahamu wangu ni yule niliyekuwa nanunua kuku kwake. “Nawaomba Watanzania, serikali, viongozi au hata wasanii wanisaidie kupata msaada wa kuona tena, ikiwezekana niende nje nikawekewe macho mengine kwa mtaalam yeyote duniani.


” MAMA YU TAYARI KUTOA JICHO! “Mama yangu amesema yupo tayari kunitolea jicho lake moja hivyo kama tutapata daktari wa kumtoa hilo jicho moja na kuniwekea mimi, hakuna shida kwani mimi ndiye mhimili wa familia yetu. Ninamlea mama na wadogo zangu, mimi ni mtoto wa kwanza.

” HUYU HAPA MAMA MZAZI  
Pia Wikienda lilizungumza na mama mzazi wa Said, Halima Omar aliyekuwa akilia kwa uchungu ambapo alisema kuwa, yupo tayari kumtolea mwanaye jicho moja ili apate kuona tena na kuendelea na shughuli zake. 

KUHUSU SCORPION 
Aliongeza kuwa, wakati wa kumsaka Scorpion waliambiwa kwamba, kawaida yake akishafanya tukio kama hilo au mauaji huwa anavaa nguo nyeusi mwili mzima na kweli alipokamatwa na polisi alikuwa na mavazi hayo. Likiwa eneo lilipojiri tukio hilo, Buguruni, Wikienda lilikuta habari ya Scorpion kudaiwa kumfanyizia Said ukatili huo ni gumzo. Baadhi ya watu walikiri kushuhudia tukio alilofanyiwa Said lakini walishindwa kutoa msaada kwa sababu jamaa huyo ni ‘mtu hatari’ hivyo walihofia uhai wao. Walisema kuwa, Scorpion alikamatwa kwa msaada wa askari wa kutoka Kituo cha Polisi Sitaki-Shari ambao walitinga BuguruniKwamnyamani anapoishi kisha kumtia mbaroni. 

KAMANDA WA POLISI AKIRI 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, ACP Salum Hamdani alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba, mtuhumiwa yupo selo akisubiri upelelezi ukamilike ili sheria zaidi ifuate mkondo wake.

No comments