Header Ads

SITALIA TENA-10


NYEMO CHILONGANI
Saida alikuwa ndani ya chumba kile akitetemeka, mapigo yake ya moyo yalikuwa juu na hakujua ni kwa namna gani angeweza kutoka salama ndani ya chumba kile. Watu waliokuwa nje bado waliendelea kuufungua mlango ule kwa ajili ya kuingia ndani.
Alichokifanya hata kabla watu hao hawajaingia ni kulifungua pipa moja, aliliona likiwa na maji yaliyokuwa na chokaa. Hakutaka kujiangalia ni kwa jinsi gani alikuwa msafi, harakaharaka pasipo kupoteza muda akaanza kuingia ndani ya pipa hilo, tena taratibu ili kuzuia maji yasimwagike chini.
Wakati amelifunga tu pipa hilo kwa mfuniko, mlango ukafunguliwa na watu hao kuingia ndani. Hakukuwa na mtu yeyote yule, waliangalia huku na kule, nyuma ya mapipa tena kwa haraka sana, lakini hakukuwa na kitu.
“Humu kuna nini?”
“Chokaa..”
Kwa kuwa yalikuwemo mapipa mengi, hawakutaka kufungua yote na kuangalia ndani, walifungua matatu tu, wakajiridhisha na hivyo kutoka ndani ya chumba hicho pasipo kujua kwamba mtu waliyekuwa wakimtafuta alikuwa ndani ya pipa moja humo stoo.
Mule ndani ya pipa alimokuwa, Saida alikuwa na presha kubwa, alizama kabisa ndani kwa kuziba pua yake kwani hakutaka kupumua akiwa humo. Yalikuwa mateso makubwa kuyavumilia lakini kwa jinsi alivyokuwa na pumzi kubwa, alishangaa akikaa humo kwa sekunde ishirini nzima ambapo watu hao wakatoka.
Hakutaka kuibuka kwa fujo, alipohisi kwamba watu hao wameondoka, akaufungua mfuniko wa pipa kidogo sana na kuchungulia, hakukuwa na mtu yeyote ndani ya chumba kile, akaanza kujitoa huku mwili mzima ukiwa umejaa chokaa.
Wakati polisi walipomkosa Saida ndani ya chumba kile, wakaondoka na kuelekea nje, huko, wakakutana na mwanamke ambaye kazi yake ilikuwa ni kufanya usafi ndani ya meli hiyo siku ambayo meli ilitakiwa kuondoka, kama ilivyo siku nyingine, akawa anafanya usafi huku akiwa amefunika kichwa chake na uso kwa kutumia nikabu.
Polisi wale walipomuona, wakahisi kwamba mwanamke huyo alikuwa Saida, hawakutaka kumuacha, walichokifanya ni kumsogelea, kabla ya kumuuliza chochote wakamchukua na kuanza kutoka naye huku wakiwa na uhakika kwamba mwanamke huyo alikuwa Saida.
“Niache niondoke,” alisema mwanamke huyo huku akipiga kelele.
Mara ya kwanza aliposikia sauti hiyo, Kareem alihisi kwamba alikuwa Saida, alijiandaa kufanya kile alichotaka kufanya lakini alipoisikia sauti hiyo mara kwa mara akagundua kwamba hakuwa Saida bali mwanamke mwingine kabisa.
“Na huyu ni nani?” aliuliza mkuu wa polisi.
“Anaitwa Nurhat...”
“Ni nani?”
“Mfanyakazi wa meli hii, huwa na kazi ya kusafisha meli kila inapotaka kuondoka,” alijibu Yusuf Al Sadiq.
Kwa kuwa hakukuwa na sheria ya kumvua juba au kitambaa kichwani bila ridhaa yake, wakamuomba kufanya hivyo, naye akafanya. Hakuwa Saida kama walivyofikiria bali alikuwa mtu mwingine kabisa.
Polisi wakachoka, walichokifanya ni kukubaliana nao kwamba msichana huyo hakuwepo ndani ya meli hiyo hivyo wakaondoka huku wakimuacha Kareem akiwa na furaha tele, hatimaye mpenzi wake angeweza kufika Dubai salama kwani mji huo haukuwa na sheria zozote kile, Waarabu waliishi kama Ulaya kwani ndiyo kilikuwa kitovu cha biashara na hata Wazungu walikuwa wengi sana.
“Wameondoka! Imekuwaje tena huko ndani? Si umesema kwamba waliingia katika stoo aliyokuwepo Saida?” aliuliza Kareem.
“Ndiyo!”
“Sasa iweje wasimuone?”
“Hata mimi nashangaa! Hebu niende kumwangalia!”
Yusuf Al Sadiq akaelekea huko, alitaka kuona ni kitu gani kilikuwa kimetokea, alipofika huko, akamkuta Saida huku mwili wake wote ukiwa umejaa chokaa. Alishtuka, alipomuuliza kilichotokea, Saida akaanza kumwambia kila kitu kilichotokea hivyo Yusuf Al Sadiq kurudi nje na kumwambia Kareem.
“Ni msichana mwelevu sana. Naomba unisaidie Yusuf, afike Dubai tu, nitakwenda huko kuonana naye,” alisema Kareem.
“Hakuna tatizo!”
Saa mbili usiku safari ikaanza, Saida alikuwa ndani ya chumba kile, tayari alikwishachukuliwa na kupelekwa sehemu iliyokuwa salama kwa ajili ya kuoga na kubadilisha nguo. Hakuamini kama huo ndiyo ungekuwa mwisho wake wa kukaa nchini Oman, alimuomba Mungu sana ili anusurike kuuawa na hatimaye alinusurika.
Safari iliendelea. Kutoka Oman mpaka Dubai hakukuwa mbali sana lakini kwa usafiri wa meli, ilitakiwa kutumia wiki nzima kwani ilikuwa ikizunguka sana. Wakati safari ikiendelea, tena usiku wa manane, meli ikaanza kupita katika eneo lililoitwa almawt ikimaanisha kifo.
Hilo ndilo lilikuwa eneo hatari kama ilivyokuwa nungwi katika Bahari ya Hindi. Meli nyingi zilizama kwani kulikuwa na mzunguko mkubwa wa maji mahali hapo. Meli nyingi zilikuwa zikipita mbali kabisa na almawt na zile ambazo zilikuwa zikipita hapo ni zile zilizokuwa na mashine kubwa.
Meli hiyo ilikuwa na mashine kubwa, kutopita hapo ilimaanisha kwamba wangezunguka sana. Katika maisha yao yote tangu meli hiyo ianze kufanya kazi ilikuwa ikipita njia hiyo mara kwa mara.
Waliiamini kutoka na injini yake ya Kijerumani. Wakati inapita katika eneo hilo siku hiyo, injini ambayo walikuwa wakiitegemea, haikuwa ikifanya kazi kama ilivyotakiwa na ugumu ukaongezeka kwani siku hiyo kulikuwa na mzunguko mkubwa wa maji eneo hilo ambalo ulisababishwa na kuchafuka kwa bahari.
Meli ikaanza kupelekwa huku na kule, Yusuf Al Sadiq alijitahidi kuitoa katika eneo hilo lakini ilishindikana, maji yalikuwa na nguvu kubwa. Meli ikapelekwa huku na kule, kutokana na mawimbi kupiga sana, meli ikaanza kukaa upandeupande, ikapigwa na mawimbi mazito na hatimaye maji kuanza kuingia ndani kupitia madirishani.
Kila mtu aliyekuwa ndani ya meli hiyo alijua fika kwamba meli ingezama kama tu nahodha asingetumia kazi ya ziada kuiondoa meli hiyo mahali hapo. Alipambana na kupambana ila kilichotokea, injini ikaanza kuzima kwani maji yale ya chumvi yakaingia ndani kabisa mpaka sehemu ambayo ilizibwa na kufanya uharibifu mkubwa.
“Vipi tena? Mbona injini imezima?” aliuliza jamaa mmoja huku akionekana kushtuka.
“Hata mimi nashangaa...nafikiri maji yameingia kwenye injini!” alijibu Yusuf Al Sadiq ambaye ndiye alikuwa nahodha mkubwa humo melini.
“Kwa hiyo bosi?”
“Ni lazima tupunguze mizigo kwanza, meli haitakiwi kuwa na mizigo mingi. Nendeni mkapunguze mizigo ili meli isizame. Baada ya hapo, tutaondoa maji yaliyokuwepo humu,” alisema Yusuf Al Sadiq.
Wafanyakazi wake wakaondoka mahali hapo, kitu cha kwanza walichokifikiria kilikuwa ni kutoa mizigo iliyokuwa stoo, waliamini kwamba humo ndipo kulipokuwa na mizigo mizito. Wakaenda huko.
Wakati meli ikianza kuyumbayumba, Saida alikuwa akitetemeka, aliogopa kwani hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Alibaki akiwa amesimama ndani ya chumba kile. Wakati akiwa anashangaa, mapipa yakaanza kuanguka, lile pipa lililokuwa na mfuko ambao aliutoa nalo likaanguka, mapipa yote yakaanza kumwaga chokaa ile.
Wakati akishangaa, mara akasikia vishindo vya watu wakija kule alipokuwa, hakutaka kusubiri, akalichukua pipa moja na kisha kuingia humo ndani, akachukua mfuniko na kujifunika.
Watu wale walipofika, wakaangalia mapipa yote, chokaa ilikuwa chini, walichanganyikiwa, ilikuwa ni lazima kupunguza mizigo ya meli hiyo, walitakiwa kutoa chokaa yote iliyokuwa humo na mapipa hayo, hawakutaka kuchelewa, kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kuyaondoa mapipa hayo na kuyatupa baharini.
Mapipa yalikuwa mazito, waliyabeba wawiliwawili na kuanza kulitupa moja baada ya jingine. Hawakuambiwa kuhusu Saida, walichojua ni kwamba ndani ya chumba kile hakukuwa na mtu yeyote yule. Wakalishika lile pipa alilokuwemo Saida kisha kulitupa baharini pasipo kuwa na habari yoyote ile.
Injini ilizima, alichokifanya Yusuf Al Sadiq ni kuanza kuishtuashtua kifundi, mara ikawaka kipindi ambacho kwa kiasi fulani bahari ilianza kutulia. Aliamua kutumia nguvu sana kuiondoa meli hiyo katika eneo hilo, akafanikiwa na meli kuanza kuondoka kwani hata haikuwa na mizigo mikubwa kutokana na mapipa yale na mizigo mingine kutupwa baharini kuziokoa nafsi zao.
“Afadhali! Asante Allah! Tumenusurika,” alisema Yusuf Al Sadiq huku akinyanyua mikono yake kama mtu aliyekuwa akiomba dua.
“Hakika yeye ni muweza,” alisema kijana mwingine.
Hakuwa na habari na Saida, meli iliendelea kwenda mbele, alimsahau kabisa Saida. Asubuhi iliyofuata ndipo akakumbuka kuhusu Saida, harakaharaka akaelekea kule stoo ili kumwangalia na kumjulia hali.
Alipofika huko, akaingia ndani, kilichomshtua, hakukuwa na pipa lolote lile. Akaanza kumuita Saida, aliita na kuita lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyesikia. Akaondoka na kuwafuata vijana wake, alitaka kujua kama mapipa yote yalitupwa au la.
“Mlitupa mapipa yote?” aliuliza Yusuf Al Sadiq huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Ndiyo! Yalikuwa mazito lakini yote tuliyatupa baharini usiku huohuo,” alijibu kijana mmoja huku akionekana kutabasamu.
“Unasemaje?”
“Tuliyatupa yote mkuu!” alijibu kijana huyo. Yusuf Al Sadiq akashika kichwa na kukaa chini. Hakuamini alichokisikia kwani aliamini kwamba Saida alikuwa ndani ya pipa mojawapo.
Je, nini kitaendelea?

No comments