Header Ads

SITALIA TENA -14


NYEMO CHILONGANI
Hakukuwa na mtu aliyekuwa akiumia moyoni mwake kumuona msichana Saida mahali hapo kama Ahmed. Kila alipomwangalia msichana huyo, alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake, ni kweli aliwekwa bondi mahali hapo, ni kweli bosi wake alikuwa ametoa kiasi kikubwa cha fedha lakini kitendo cha Saida kuwepo mahali hapo, aliona kabisa hakukuwa na haki.
Alipanga kumuokoa ndani ya jumba hilo, hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kumtoa kwani yeye na jamaa mwingine ndiyo waliopewa kazi ya kumlinda msichana huyo na kuambiwa kwamba hakutakiwa kuondoka.
Hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kumshawishi mwenzake akubaliane naye ili kumtorosha msichana huyo, aliamini kwamba isingekuwa rahisi hata mara moja, hivyo ilikuwa ni lazima afanye kazi peke yake.
“Saida...” alimuita.
“Abeee..”
“Unaona raha kuwa hapa?” alimuuliza.
“Hapana. Ninapakumbuka nyumbani, ninahitaji kurudi nyumbani kuwaona wazazi wangu,” alisema Saida huku akitokwa na machozi.
“Naomba usilie. Nipo tayari kukurudisha nyumbani kwenu,” alisema Ahmed Said huku akimwangalia msichana huyo machoni. Saida akashtuka kwani huyo alikuwa mmoja wa watu walioagizwa kumlinda msichana huyo.
“Naomba uniamini! Nitakutorosha mahali hapa,” alisema jamaa huyo.
Hicho ndicho alichotaka kukifanya, alidhamiria moyoni mwake kwamba iwe isiwe ilikuwa ni lazima kumtorosha msichana huyo mahali hapo. Muda mwingi alikuwa akijifikiria ni kwa namna gani angeweza kumtorosha Saida ndani ya jumba hilo kubwa.
Wakati akijifikiria hilo, akamkumba msichana aliyeitwa kwa jina la Samira ambaye mara kwa mara alikuwa akifika nyumbani hapo kwa ajili ya kuleta matunda na kuondoka. Huyo ndiye ambaye alitakiwa kutumiwa, yaani yeye abaki na Saida aondoke nyumbani hapo.
Alichokifanya ni kumsubiri Samira, baada ya siku mbili akafika nyumbani hapo kama kawaida yake, alikuwa na kikapu cha matunda, alifika hapo kama siku nyingine kuleta matunda. Alichokifanya Ahmed ni kumuita na kisha kuzungumza naye.
“Naogopa,” alisema Samira.
“Hutakiwi kuogopa. Naomba unisaidie!”
“Mmh! Sawa!”
Walipanga kwamba ni lazima baada ya siku mbili Samira arudi nyumbani hapo huku akiwa amevaa mavazi yake vilevile, yaani juba jeusi pamoja na nikabu iliyoyafanya macho yake tu kuonekana, baada ya hapo, aingie ndani ambapo humo, Ahmed angefanya kila liwezekanalo Saida avae mavazi kama hayo na kisha kuondoka ndani ya jumba hilo.
Hilo halikuwa tatizo. Alichokifanya Ahmed ni kumwambia Saida kile ambacho kilitakiwa kufanywa na msichana huyo kukubali hivyo kuanza kufanya mipango mapema kabisa.
Akatafutiwa mavazi hayo, akawa anavaa kuanzia siku hiyo na kwa siku mbili ambazo msichana Samira alitakiwa kurudi nyumbani hapo. Hakukuwa na aliyejua kilichokuwa kikiendelea zaidi ya Ahmed tu.
Siku ya tukio ilipofika, msichana Samira akafika nyumbani hapo huku akiwa na kapu lake, akakaribishwa mpaka ndani. Kwa sababu kila kitu kilikuwa kimepangwa, Samira akaomba kwenda chooni, alipokwenda huko, naye harakaharaka Ahmed akaelekea chumbani na kumwambia Saida aende chooni huku akiwa amevaa mavazi yale, akaelekea huko.
Alipofika, akakutana na Samira, wakasalimiana na kuambiwa atoke haraka sana, akifuate kikapu kilichokuwa sebuleni, akichukue na kuondoka nacho. Hilo halikuwa tatizo, harakaharaka huku akiwa na juba pamoja na nikabu mwilini mwake, akaondoka kulifuata kikapu kile cha matunda, japokuwa alikuwa na hofu lakini hakutaka kuionyesha kabisa kwani hiyo ilikuwa nafasi yake pekee.
Akakichukua na kuanza kuondoka, alipofika nje, walinzi wote hawakutaka kujali kwani walijua kwamba yule alikuwa msichana Samira, hivyo wakaachana naye, akatoka nje na kuanza kuondoka kwa mwendo wa kasi na Samira kurudi katika chumba kile.
Hakujua angekwenda wapi, hakujua sehemu yoyote hapo Iran, alikuwa na hofu kwamba angepotea, kwani hakujua baharini kulikuwa wapi, uwanja wa ndege ulikuwa wapi.
Siku hiyohiyo usiku wanajeshi wakavamia ndani ya jumba hilo, wakaua walinzi na kuingia ndani, walichokuwa wakikitaka ni msichana huyo tu. Wakaingia mpaka katika chumba cha siri, huko wakamkuta msichana Samira akiwa amekaa chini huku amejiinamia zake.
Wakamchukua na kumvua nikabu, hakuwa mwenyewe. Walichanganyikiwa, hawakujua mahali msichana huyo alipokuwa. Wakawachukua baadhi ya walinzi ambao hawakuwaua na kuwauliza kuhusu msichana huyo.
“Yupo ndani!” alijibu mlinzi mmoja.
“Siyo yule.”
“Mimi nilikuwa najua ni huyo. Hakuna msichana mwingine humu zaidi ya huyo,” alisema jamaa huyo.
“Na wewe unajua nini?” aliuliza mwanajeshi mmoja, alikuwa akimuuliza Ahmed.
“Mimi najua aliyekuwa chumbani ndiye msichana pekee humu ndani,” alijibu Ahmed huku akikiinamisha kichwa chake.
Hawakutaka kukubali, walijua fika kwamba watu hao walijua mahali alipokuwa msichana huyo, waliwapiga huku wakiwataka kusema mahali alipokuwa Saida lakini Ahmed hakufumbua mdomo wake kuwaeleza ukweli.
Walimtafuta ndani ya nyumba nzima, ndani ya vyumba vyote vya siri lakini hawakuweza kumuona msichana huyo, walichanganyikiwa, ni jana tu waliambiwa kwamba msichana huyo alikuwa ndani ya nyumba hiyo lakini cha kushangaza, hakuwepo kitu kilichomchanganya kila mtu.
“Hayupo...” alisema mwanajeshi mmoja huku akiwa ameshika simu.
“Unasemaje?”
“Hayupo mkuu! Tumeangalia kila kona, hakuna msichana huyo!”
“Haiwezekani!”
“Kweli mkuu!”
Upande wa pili, Saida alikuwa akitembea huku akiwa na kikapu chake, jua lilikuwa kali mno, aliungua na juba jeusi alilokuwa amelivaa liliingiza joto mno lakini hakulivua, aliendelea na safari yake kama kawaida.
Alitembea huku akipishana na watu wengi, sehemu kubwa ilikuwa jangwa, hakutaka kurudi nyuma, aliendelea mbele mpaka kufika sehemu ambayo kulikuwa na wanawake wengi na watoto. Hakujua sababu iliyowafanya kuwa mahali hapo, alichokifanya ni kwenda na kusimama pembeni yao.
Mara likatokea gari moja chakavu, lori kubwa, wakawake wote wakalifuata na kupanda kwa nyuma, naye hakutaka kusimama, akalifuata, akapanda na kuanza kuondoka.
Walipokuwa wakielekea hakupajua lakini aliona ni bora aende huko kuliko kuendelea kutembea. Njiani alikuwa akimuomba Mungu kwamba sehemu ambayo gari hilo lilipokuwa likielekea isiwe sehemu ya hatari.
Baada ya dakika kadhaa, gari hilo likasimama sehemu, hakujua palikuwa wapi lakini alichosikia ni sauti ya mwanaume akiwaamuru wanawake hao wateremke kutoka garini. Harakaharaka naye akateremka na kuanza kuelekea kule wanawake wale walipokuwa wakielekea.
“Mawlidu N-Nabiyyi,” (Sikukuu ya Maulidi) alimsikia mwanamke mmoja akisema, si huyo tu, wote walikuwa wakisema hivyohivyo, hapo ndipo akagundua kwamba kipindi hicho kilikuwa ni kipindi Sikukuu ya Maulid, kukumbuka siku ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW)
“Mungu wangu!” alijisemea Saida wakati akiingia ndania ya jumba moja kubwa, humo kulikuwa na watu zaidi ya elfu tatu, wanawake wale walipoingizwa akiwemo yeye mwenyewe, wakachukuliwa na kupelekwa katika chumba kimoja kikubwa na kuambiwa wasubiri humo.
Muda wote aliokuwa humo, moyo wake ulikuwa ukidunda kupita kawaida. Kabla hajajiuliza atafanya nini, wakaletewa Qur-aan (Kitabu Kitakatifu cha Kiislamu) na kupewa, wajiandae kwa ajili ya kusoma aya mbalimbali kwa kichwa huku wakichanganya na zile zilizokuwa ndani ya kitabu hicho kitakatifu.
Je, nini kitaendelea?

No comments