Header Ads

SITALIA TENA-17


NYEMO CHILONGANI
Upinzani wa biashara ulikuwa mkubwa, kila siku mabilionea walikuja na mawazo mapya ya biashara, hakukuwa na aliyekuwa radhi kuona akipitwa na mwenzake, kila siku walianzisha biashara kubwa ambazo ziliwafanya kuingiza kiasi kikubwa cha fedha.
Bilionea Bwana Abdulaziz kila siku alipambana kadiri awezavyo ili kuwa na utajiri mkubwa, alikuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wengi wa Kiarabu, kila kona, kuanzia katika nchi za Kiarabu barani Asia mpaka Afrika, alikuwa akijulikana kwa umachachari wake wa kuchangamkia fursa.
Mwaka 2014 wakati Umoja wa Mataifa ukiwataka mabilionea wa Kiarabu kuandika ‘proposal’ kwa ajili ya kusambaza chakula nchini Syria na Afghanistan ambapo kulikuwa na mapigano makubwa, mabilionea wengi wakajitokeza lakini nafasi hiyo ilipatikana kwa bilionea wa Misri, Bwana Sadiq Faraq ambaye alipewa nafasi hiyo iliyotarajiwa kumpa kiasi kikubwa cha fedha kwenye akaunti yake.
Bwana Faraq hakujua ni kitu gani kilitokea lakini tenda ikahamishwa haraka sana mpaka kwa bilionea Abdulaziz kitu kilichomuuma sana. Hilo hakulipenda, uadui ukaanza, hakumpenda kwa sababu alimnyima kiasi kikubwa cha fedha na alipofuatilia, akakuta kulikuwa na mazingira ya hongo yaliyotembea mpaka tenda kutolewa mikononi mwake na kupewa huyo.
Huo ukawa uhasama, moyo wake ukajeruhiwa na hakutaka kukubali kabisa, kama alivyoumia, naye akataka kuumiza moyo wake hivyo alichokifanya ni kuanza kumtafuta ili amuue.
Kazi haikuwa nyepesi, aliwatuma watu kwenda kujitoa mhanga katika sherehe mbalimbali alizokuwa akihudhuria lakini hakuweza kumuua mzee huyo. Moyo wake uliendelea kuwa na maumivu makali mno, alichanganyikiwa, alipoona kumuua ilishindikana, akaanza kumtafuta mtoto wake, Kareem.
Akaanza kumfuatilia, kama ilivyokuwa kwa baba yake, hata kwa mtoto huyo kumpata halikuwa jambo jepesi, alihangaika sana, aliwatuma watu kumpeleleza na kumfuatilia lakini hawakuweza kumpata.
Wakati Kareem alipokwenda nchini Tanzania, vijana wake walimfuata, wakapanda ndege aliyokuwepo, wakashuka ndege wakiwa pamoja, wakatafuta sehemu nzuri ya kumuua, alipopanda teksi na kwenda hotelini, nao walimfuata, kesho yake alipokwenda Magomeni alipokuwa akimfuata Saida, walimfuata lakini hali ya kushangaza, aliwapotea kabisa na hawakujua alikwenda kwa njia ipi kwani gari liliingia katika barabara nyingine za vumbi.
Wakashindwa na kurudi nchini Misri. Mzee Faraq alichanganyikiwa, akawaambia vijana wake wahakikishe kwamba kijana huyo anatekwa na kuuawa, hata alipokwenda nchini Iran, kama kawaida yao walimfuatilia, kuanzia kwenye hoteli aliyofikia mpaka kesho yake alipomchukua Saida na kuanza kuondoka naye.
“Mkuu! Tumempata Kareem, ila yupo na mfanyakazi wa hoteli. Tufanye nini?” aliuliza jamaa mmoja alipokuwa akizungumza na mzee huyo kwenye simu.
“Huyo mhudumu anafanya nini humo?”
“Hatujui! Au tumuachie huyu mhudumu?”
“Hapana. Hilo ni kosa kubwa sana kwani huyo ataweza kutoa siri kwa kuwaambia polisi. Cha msingi wasafirisheni wote. Wachomeni dawa za usingizi, wawekeni kwenye jeneza na kuwaleta huku, ninawataka wote wawili, kama kumuua huyo mwanamke, tutamuua hukuhuku,” alisikika mzee Faraq.
Hilo ndilo lililofanyika, wakawachoma watu hao sindano, japokuwa Kareem alikuwa amezimia, akachomwa sindano hiyo pamoja na mpenzi wake, saa mbili zilizofuata, wakapakizwa ndani ya ndege iliyotakiwa kuelekea nchini Misri.
Wakafanikiwa kuwasafirisha na kuwapeleka huko, walipofika, wakaelekea nyumbani kwa huyo mzee, alipomuona Kareem, moyo wake ukafurahi mno kwa kujiona mshindi, aliuona huo kuwa muda sahihi wa kulipa kisasi kwa mabaya aliyokuwa amefanyiwa.
“Kazi nzuri sana,” alisema mzee huyo huku akikenua na kuyafanya meno yake thelathini na mbili kuonekana.
“Tuwapeleke kwenye banda la nje au ndani ya chumba cha mateso?” aliuliza kijana mmoja.
“Wapelekeni kwenye chumba cha mateso. Kile chenye mateso kama Guantanamo,” alisema mzee Faraq.
Watu hao wakachukuliwa na kupelekwa huko, wakaingizwa ndani ya chumba hicho cha mateso. Kilikuwa na unyevuunyevu kwa chini, kulikuwa na maji machafu yaliyotoa harufu mbaya sana ambayo yalipitishwa kwa kutumia bomba la chooni lililounganishwa mpaka chumbani humo, kulikuwa na giza totoro, mbu pamoja na wadudu wengine wabaya wanaosambaza magonjwa mbalimbali.
Watu hao hawakuwa wakijitambua, walipoingizwa humo, mlango ukafungwa na watu hao kutoka ndani ya chumba hicho. Baada ya saa moja, wakarudiwa na fahamu, hawakujua walikuwa wapi, chumba kilikuwa na joto sana, harufu mbaya na hawakuona kitu chochote kile, kila mmoja akaanza kupapasa.
“Wewe nani?” aliuliza Kareem mara baada ya kumgusa Saida.
“Mpenzi! Ni mimi!”
“Saida mpenzi!” alisema Kareem, akamvuta msichana huyo na kumkumbatia.
Kilikuwa chumba chenye mateso makali, muda wote walikuwa bize kuua mbu, walikuwa kwenye mateso makali mno. Mbali na mbu, kulikuwa na wadudu wengine kama kunguni, waliwauma mno na kutokana na giza kubwa lililokuwepo humo, hawakujua kama muda huo ulikuwa usiku au mchana.
“Hapa ni wapi?” aliuliza Saida.
“Sijui! Ninachokumbuka wale watu walinipiga, nini kiliendelea?” aliuliza Kareem.
“Walituchoma sindano. Baada ya hapo, nikalala pia. Mungu wangu! Tupo wapi hapa?” aliuliza Saida.
Kilichokuwa kikimuogopesha ni ujauzito aliokuwa nao, ulimfanya kuhisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha yake kutokana na mbu wengi waliokuwa ndani ya chumba hicho.
Japokuwa macho yao yalitakiwa kuzoea giza lakini hawakuweza kulizoea, waliendelea kuwa kwenye hali mbaya huku wakiendelea kuumwa kila dakika. Mbali na kuhisi mbu, kunguni na wadudu wengine, pia wakaanza kusikia sauti za panya buku ndani ya chumba hicho, iliwatisha mno, kila wakati Saida alimkumbatia mpenzi wake kwani mara nyingi panga wasiowaona waliwafuata na kuwarukia.
“Mpenzi! Nahisi nitakufa..” alisema Saida.
“Huwezi kufa mpenzi! Utakuwa salama.”
Walikaa humo kwa siku ya kwanza, waliletewa chakula mara moja kwa siku tena jioni, walitakiwa kuteseka hata kabla ya kuuawa. Siku ya pili ilipoingia, Saida akaanza kujisikia vibaya, akaanza kusikia kizunguzungu, akaanza kutapika huku mwili wake ukiwa unachoka sana.
Aliumwa sana na mbu, alikuwa mjauzito na tayari akaanza kupata homa kali kwani damu yake haikuwa na nguvu za kutosha kujikinga na magonjwa mbalimbali. Kazi ikawa kwa Kareem, hakutaka kumuona mpenzi wake akifa, alifanya kila linalowezekana ili amsafirishe na kuelekea nchini Tanzania akiwa salama kabisa lakini kabla hawajafika huko, tayari kulionekana kuwa na tatizo.
“Ninakufa...mpenzi ninakufa,” alisema Saida huku akiwa amekumbatiwa.
Aliendelea kutapika, kwa Kareem hakutaka kujali, alitapikiwa kifuani lakini hakutaka kumuachia msichana huyo, aliendelea kumkumbatia kama kawaida.
“Kareem...nakufa mpenzi! Nakufa mpenzi!” alisema Saida, alizidiwa, aliendelea kutapika, mwili uliendelea kuchoka.
Kareem alichanganyikiwa, hakutaka kuona mpenzi wake akifa, alimpenda kwa sababu alikuwa kila kitu katika maisha yake, hakutaka kumuona akifa tena mbele ya macho yake huku akiwa mikononi mwake, alichokifanya ni kupapasa na kuufuata mlango na kuanza kuugonga huku akihitaji msaada.
Baada ya dakika kumi, mlango ukafunguliwa na wanaume wawili walioshikilia bunduki mikononi mwao. Kareem akaanza kuwaambia kwamba mpenzi wake alizidiwa, alikuwa akifa ndani ya chumba kile, badala ya watu hao kumsaidia, ndiyo kwanza wakaanza kucheka.
“Kwani lengo la nyie kuwaweka humo ni kuyafurahia maisha? Tumewaweka humo ili mfe, mkifa ndiyo ukamilisho wa malengo yetu. Acha afe, na akifa, na wewe unatakiwa ufe. Casmir, kaongeze maji ya chooni yapite katika bomba lake,” alisema mwanaume mmoja, akamsukuma Kareem ndani kisha kuufunga mlango, hakukuwa na mtu yeyote eliyeonekana kujali chochote kile.
Kareem akamrudia Saida pale chini alipokuwa, akampima joto la mwili wake, mwili ulikuwa wa moto mno, mapigo yake ya moyo yalianza kudunda kwa taratibu sana na kadiri muda ulivyokuwa ukizidi kwenda mbele ndivyo alivyoendelea kudhoofika kitu kilichomfanya kuogopa sana, kulikuwa na kila dalili za kumpoteza Saida ndani ya chumba kile.
Wakati akiwa amemshikilia, akahisi mkono wake ukigusa majimaji katika miguu ya msichana huyo, alihisi kwamba inawezekana alikojoa lakini alipozishika vizuri, uzito wake, hakuhisi kama huo ulikuwa mkojo au jasho, jibu alilolipata ni kwamba hizo zilikuwa damu ambazo zilikuwa zikimtoka Saida kuonyesha kwamba alipata tatizo kubwa, hasa mimba kuharibika.
“Saida...naomba usife...Saida, naomba usife...” alisema Kareem huku akilia kama mtoto, alimkumbatia Saida, hakutaka kumpoteza, damu ziliendelea kumtoka sehemu za siri, mimba ilianza kuharibika huku mwenyewe akiwa katika hali mbalia mno.
Wakati akijiuliza nini cha kufanya, Saida akaanza kurusha miguu yake huku na kule, ndiyo alikuwa kwenye hatua za mwisho za kuvuta pumzi ya dunia hii.
“Saida...naomba usife mpenzi...Mungu...Mungu naomba usimuue Saida wangu, ninampenda, Mungu naomba usimuue...” alisema Kareem huku akilia, wakati akisema maneno hayo, naye akaanza kuhisi homa ikimpata, mwili ukaanza kuchoma, ukaanza kumuuma na kwa mbali akahisi kizunguzungu, mbu waliokuwa ndani ya chumba kile waliwaambukiza maralia kali.
“Mungu! Nipo tayari kufa ila naomba umuokoe mpenzi wangu, Saida,” alisema Kareem. Alikata tamaa, alipomgusa Saida, alikuwa ametulia tuli. Hakutingisha kiungo chochote cha mwili wake. Hilo likamtia hofu zaidi na kuhisi kwamba tayari Saida alikuwa amefariki dunia.
“Pumzika kwa amani mpenzi wangu! Imeniuma sana, nimekosa mtoto, mbaya zaidi nimekupoteza wewe pia...pumzika kwa amani mpenzi!” alisema Kareem huku akimkumbatia Saida kwa nguvu zote, kwake, tayari msichana huyo alionekana kuwa marehemu.
Je, nini kitaendelea?
Je, Saida amekufa?
Kama amekufa! Nani amesema hatalia tena?

No comments