Header Ads

SITALIA TENA -20


“Kawaleteni wale watu mahali hapa,” alisema mzee Faraq huku akionekana kuwa na hasira mno, mikononi mwake alikuwa na bastola, alitetemeka mno mno huku kijasho chembamba kikimtoka.
“Mkuu! Ila yule mwanamke amekufa!”
“Amekufa! Kivipi? Yaani mmemuacha mwanamke afe! Kwa nini?” aliuliza mzee Faraq huku akionekana kuwa na hasira.
Kwa haraka sana, vijana wale wakatoka hapo na kwenda katika chumba kile cha Guantanamo ambacho kilikuwa chini kabisa, kwenye handaki. Walipofika kule, wakamkuta Kareem akilia tu, alikuwa amemshika mpenzi wake aliyekuwa hoi kabisa.
Wakawafuata na kuwachukua, wakatoka nao na kuwapeleka kwa mzee yule. Kitendo cha Mzee Faraq kumuona Saida akiwa kwenye hali ile, moyo wake ukashikwa na huzuni ambayo hakuwahi kuihisi kabla, msichana huyo aliyekuwa mbele yake hakufanya kitu chochote kibaya, hakuhusika katika ubaya wowote ule, kwa nini afe mikononi mwake, akasikia moyo wake ukimuhukumu.
Harakaharaka akamuita daktari wa familia na kisha kufika mahali hapo, alichokifanya ni kuanza kumuhudumia msichana huyo. Akamtundikia dripu iliyokuwa na dawa ya metakelfin yenye ujazo wa miligramu 500 ambayo ilisagwa na kuwekwa kwenye dripu hiyo.
Ilikuwa ni dawa kali na yenye ujazo mkubwa, waliyaruhusu matone thelathini yaingie kwa dakika kwani hali ya Saida ilikuwa mbaya mno na kama wangechelewa basi msichana huyo angeweza kufa.
“Ana mimba?” aliuliza daktari.
“Ndiyo! Ana mimba ya mwezi mmoja na nusu,” alijibu Kareem huku akimwangalia mpenzi wake kitandani alipokuwa.
“Pole sana! Sidhani kama mtoto atakuwa hai, dalili zinaonyesha kwamba mimba imeharibika,” alisema daktari huyo maneno yaliyomfanya Kareem kuanza kulia kama mtoto.
Moyo wa Mzee Faraq ulibadilika kabisa kiasi kwamba yeye mwenyewe akabaki akijishangaa. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea moyoni mwake lakini ukweli ni kwamba aliwaonea huruma sana watu hao, alibaki akiwaangalia, alitamani muda urudi nyuma na kuwarudisha nyumbani kwao.
Aliyekuwa akimtaka ni Mzee Abdulaziz, alikuwa amepotea katika ndege iliyopotea na hakuona kama angeweza kumuona tena, kama yeye alikufa, inamaanisha hata kama angemuua Kareem, bado isingesaidia kwani alitamani kufanya hivyo kwa ajili ya kumuumiza mzee Abdulaziz ili ajute kwa alichokifanya, ila kama amekufa, angeumia vipi?
Kareem alikuwa pembeni ya Saida, hakutaka kumuacha, alitaka kufuatilia mwanzo mpaka mwisho. Muda wote alikuwa akimuuliza daktari kuhusu mpenzi wake, angepona au huo ndiyo ungekuwa mwisho wake?
Daktari alimfariji, akafarijika hivyo kuvumilia lakini kila alipokuwa akimwangalia mpenzi wake bado aliumia mno moyoni mwake. Siku iliyofuata, kidogo hali ya Saida ikaanza kutengemaa, dawa alizokuwa amepewa zilianza kumsaidia kwa kiasi kikubwa sana.
Mzee Faraq akafurahi, moyo wake ulikutwa na hali ambayo hakuwahi kuhisi kama alikuwa nayo katika maisha yake, alikuwa na huruma mno na kila alipokuwa akimwangalia Saida, alihisi maumivu makali, mateso aliyokuwa akipitia msichana yule hakika yalimuumiza mno.
Wakati wakiendelea kuishi nyumbani hapo, mzee Faraq akapokea ugeni mkubwa, mgeni aliyekuwa ameingia siku hiyo aliitwa Hamis Al Habsi. Huyu alikuwa miongoni mwa magaidi waliokuwa wakitafutwa kwa kipindi kirefu duniani.
Alikuwa miongoni mwa magaidi waliokuwa na roho mbaya, yeye ndiye aliyemfundisha Osama Bin Laden kuandaa watu, kuwajaza roho ya chuki na visasi kwa ajili ya kujitoa mhanga. Alikuwa akitisha kila kona na kwenye vyombo vya habari alitangazwa kama mtu anayetafutwa mno kuliko watu wote duniani.
Alijificha, alilindwa na watu wengi, kila kona aliogopeka, alikuwa na sura nzuri, alionekana mtu mwema na hata alipokuwa akiongea, aliongea kwa sauti ya upole. Alipenda kuswali na alikuwa mtu wa swala tano aliyekwenda Maka kuhiji kwa kujificha kila mwaka lakini mbali na mambo hayo mazuri, mtu huyo alikuwa katili kuliko mtu yeyote duniani.
Alifika ndani ya nyumba hiyo kwa ajili ya hifadhi ya siku kumi. Alitoka nchini Saudi Arabia, huko, Wamarekani walikaribia kumkamata na kumuua lakini aliwatoka katika hali ambayo hawakuitarajia.
Baada ya kunusurika huko ndipo akaamua kwenda nchini Misri na kuingia katika nyumba ya Mzee Faraq, bilionea aliyekuwa akivifadhiri vikundi vyote vya kigaidi duniani. Yeye ndiye aliyekuwa akiwapa fedha na mambo mengine, kwa kifupi mzee huyo alifanikiwa kuwalinda magaidi mbalimbali.
“Nimekuja,” alisema Hamis huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
“Karibu sana!”
Kila mmoja alifurahi kuona uwepo wa mwanaume huyo ndani ya nyumba hiyo. Katika kipindi hicho kidogo Saida alikuwa amepata nafuu na kwa sababu mzee Faraq hakutaka kabisa msichana huyo aonekane na gaidi huyo, akamtafutia chumba kingine ambacho kilikuwa kama handaki na kumtaka kukaa huko na ni mara chache tu ndiyo alikuwa akitoka.
Kareem alipokutana na Hamis, hakuamini, alimwangalia mwanaume huyo, hakuwa mgeni, alimfahamu vilivyo, alikuwa mtu maarufu aliyekuwa akitafutwa kila kona, alimwangalia, alimhusudu sana, alimpenda kwa sababu alisimama mstari wa mbele kupambana na mataifa ya Magharibi.
Alipomuona, akamsogelea na kisha kumbusu katika mashavu yake yote mawili na kuanza kuzungumza mambo mengi. Hiyo ilikuwa siku ya kwanza kwa Hamis kukaa ndani ya nyumba hiyo, alitakiwa kukaa kwa siku alizopanga kabla ya kuondoka na kuelekea nchini Iraq ambapo huko angepanga watu wake kwa ajili ya kujilipua katika daraja kubwa la Brooklyn lililokuwa nchini Marekani.
Kwa mapambano hayo alitarajia kuua watu wengi kwani daraja hilo lilikuwa kubwa na lililokuwa likipitisha magari zaidi ya milioni moja kwa siku moja tu. Mchoro wa ramani ya tukio hilo ikaanza kuchorwa humo ndani, ilikuwa ni ramani ya kifundi ambapo dakika ishirini kabla ya daraja hilo refu kulipuliwa kulitakiwa kuwe na foleni ambayo itawakusanya watu wengi na kisha magari yao mawili yenye mabomu kulipuka na daraja hilo kuanguka.
“Itawezekana?” aliuliza Mzee Faraq.
“Kwa asilimia mia moja. Nataka niteketeze kizazi chote cha Wazungu,” alisema Hamis huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
“Inshalah! Baada ya hapo?”
“Pia tulipua Hospitali ya Carthbert jijini Washington, na mwisho kabisa tutamalizia katika Chuo cha Yale, yote hayo yatafanyia siku moja, tena kwa wakati mmoja. Nahisi hapo watakuwa wamekoma,” alisema Hamis.
Huo ndiyo ulikuwa mpango wao, usiku huo wakalala huku kila mmoja akiwa na furaha tele. Wakati huohuo wa usiku, Saida akatoka katika chumba kile na kuanza kuzunguka huku na kule, hakukuwa na mtu aliyekuwa akishangaa kwani ilikuwa kawaida kufanya hivyo kila siku usiku.
Kwenye kutembea kwake humo, akakutana na Kareem na kuanza kuzungumza. Ilikuwa ni lazima waondoke kuendelea na safari yao ya kuelekea nchini Tanzania kwani Saida aliwakumbuka wazazi wake na hakutaka tena kuishi huko Uarabuni.
“Haina shida. Nikakuletee matunda ule?” aliuliza Kareem.
“Sawa. Kaniletee nakusubiria hapa kwenye kochi,” alisema Saida huku akikaa sebuleni katika kochi alilopenda kukaa Mzee Faraq.
Harakaharaka Kareem akatoka ndani ya jumba hilo na kwenda kumnunulia matunda mpenzi wake, alikimbia, alitaka kufanya haraka hata kabla Mzee Faraq hajatoka chumbani na kumkuta Saida sebuleni pale.
Alikaa huko kwenye matunda kwa zaidi ya nusu saa kwani muuzaji alikuwa amefunga ila kwa sababu kulikuwa na mteja, ilibidi aamke na kuanza kumuhudumia. Wakati muuzaji akiendelea kumuwekea matunda kadhaa kwenye kikapu alichokuwa nacho, ghafla ukasikika mlio mkubwa wa bomu.
Kila mmoja akashtuka, sehemu mlio huo ulipotoka ndiyo uliomshtua zaidi Kareem. Hakutaka kusubiri, akaacha kapu la matunda na kuanza kurudi nyumbani, alihisi kwamba kulikuwa na tatizo.
Alipokata kona na kuangalia kule nyumba ile ilipokuwa, hakuweza kuiona nyumba hiyo, kulikuwa na mchanga tu, nyumba yote ililipuliwa na ilikuwa vigumu kuamini kama mahali hapo kulikuwa na nyumba.
“Saida...Saida...Saidaaaaaa....” alijikuta akiita Kareem huku akikimbia kule kulipoonekana kuwa tambarare kwani nyumba yote ililipuliwa.
Alipofika katika eneo lile, hakukuwa na kitu kilichosimama, watu wote walikuwa wamekufa huku wakiwa wameunguzwa vibaya kwa moto wa bomu lile na ilikuwa vigumu kugundua huyu alikuwa nani, mwanaume au mwanamke.
“Saida...Saida...Saida mpenzi....” aliita Kareem huku akipekua huku na kule, kila alipopekua alikutana na mwili, katika miili yote hiyo aliyoiona, hakujua Saida alikuwa yupi kutokana na kuteketezwa na moto ule.
“Saida...Saida mpenzi usife...Saida...Saidaaa...” aliendelea kuita Kareem.
Je, nini kitaendelea?
Saida amekufa! Je, Kareem atachukua uamuzi gani?
Tukutane Jumanne mahali hapa.

No comments