Header Ads

Soko lateketea kwa moto Sumbawanga

SOKO kuu la wakulima la Nelson Mandela lililopo katika Kata ya Mazwi, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa, limeteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana na kusababisha hasara kubwa.


Moto huo uliodumu kwa zaidi ya saa nane, ulilipuka saa moja usiku Jumamosi na kuteketeza maduka na vibanda vya biashara vilivyomo ndani ya soko hilo ambalo ni la pili kwa ukubwa na umaarufu katika mji wa Sumbawanga baada ya soko kuu lililopo Kata ya Mazwi.

Kulipuka kwa moto huo kulizua tafrani kubwa kwa wakazi wa mji huo.
Soko hilo linapakana na Uwanja wa Michezo wa Nelson Mandela ambao haukupata uharibifu wowote.

Baadhi ya mashuhuda walilieleza gazeti hili kuwa, bidhaa nyingi zikiwamo nguo, kuku, majokofu na matunda viliteketea kwa moto, huku idadi kubwa ya waathirika wakidai hawakuwa na bima ya kinga kwenye biashara zao, huku huku mitaji wakiwa wamekopa kutoka taasisi mbalimbali za kifedha.

Akizungumza na gazeti hili kwenye eneo la ajali, Meya wa Manispaa ya Sumbawanga, Justine Malisawa alisema moto huo ulilipuka saa moja usiku na kuendelea kuwaka hadi usiku wa manane na kusababisha hasara kubwa ambapo vijana waliojifanya wasamaria wema walikuwa wakipora mali.

“Soko hili linamilikiwa na Manispaa ya Sumbawanga lilianza rasmi 2011, pia ni chanzo kikubwa cha mapato ya ndani, kuteketea kwake kumeisababishia Manispaa hasara kubwa, kwani kwa siku tulikuwa tunakusanya kati ya Sh 700,000 na Sh milioni moja,” alieleza kuwa Meya, kuwa gari la zimamoto lilichelewa kufika.

“Natoa pongezi za pekee kwa Jeshi la Polisi walivyoweza kuwadhibiti vibaka waliokuwa wakiendelea na uporaji ndani ya soko …chanzo cha moto huo hakijafahamika na kukiri kuwa soko hilo halikuwa na bima yoyote.

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfani Haule alisema Kamati ya Maafa itafanya tathmini ya hasara halisi iliyosababishwa na moto huo, na mipango ya awali ni kuwahamishia wafanyabiashara wa soko hilo kwenye maeneo yaliyotengwa likimoko soko la Majengo, Sabasaba, Sabato na Kizwite.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, George Kyando alisema hakuna mtu aliyekamatwa kutokana na visa vya uporaji vilivyofanyika ndani ya soko hilo usiku huo.

CHANZO: HABARI LEO

No comments