Header Ads

Marekani: Mtangazaji Aliyemhoji Trump Afukuzwa Kazi

billy-bush-jpg
Shirika la Utangazaji la NBC nchini Marekani limemfuta kazi mtangazaji Billy Bush (pichani juu) ambaye amekuwa akiendesha kipindi cha Today.
Mgombea urais wa chama cha Republican alikuwa anahojiwa na Bw Bush miaka kumi iliyopita alipotoa matamshi ya kudhalilisha kuhusu wanawake.
Mkanda wa mahojiano hayo yaliyofanyika mwaka 2005 ulifichuliwa majuzi na gazeti la Washington Post.
Baada ya kufichuliwa kwa mkanda huo, viongozi wengi wakuu wa chama cha Republican walijitenga na Trump.
Kwenye video hiyo, Bw Bush anasikika akicheka baada ya matamshi ya Trump.
Billy Bush, 45, ambaye ni mpwa wa rais wa zamani George H W Bush, alikuwa awali amesimamishwa kazi baada ya kufichuliwa kwa video hiyo.
trump-billy
Mtangazaji Billy Bush akiwa na Donald Trump.
Amekuwa mtangazaji wa kipindi cha Today kwa miezi miwili pekee.
“Ingawa alikuwa mgeni tu katika waandaaji wa kipindi cha Today, amekuwa na NBC kwa muda mrefu. Tunamtakia kila la heri,” Shirika la NBC limesema kupitia taarifa yake.
Mke wa Donald Trump, Melania, amemshutumu Bw Bush akisema alimchochea mumewe kusema mambo mabaya kuwahusu wanawake.
Bw Bush mwenyewe aliomba radhi tarehe 7 Oktoba akisema binafsi pia aliaibishwa na tabia yake alipokuwa akifanya mahojiano hayo.
Credit: BBC

No comments