Header Ads

Video: Mrembo Atinga Global Afichua Siri Za ‘Scorpion’


img_20161013_115404
Mrembo aitwaye Talta Msofe (21) akiwa katika pozi baada ya kutinga katika ofisi za Global Publishers kufichua siri za mtuhumiwa huyo, Salum Njwete ‘Scorpion’, mkazi wa Yombo Machimbo jijini Dar es Salaam.
DAR ES SALAAM: Siku chache baada ya kupandishwa kizimbani mara ya pili kwa madai ya kumchoma visu tumboni na kumtoboa macho Said Ally, mrembo aitwaye Talta Msofe (21), amefichua siri za mtuhumiwa huyo, Salum Njwete ‘Scorpion’, mkazi wa Yombo Machimbo jijini Dar es Salaam, Risasi Jumamosi linakupa hatua kwa hatua.
https://www.youtube.com/watch?v=l2Lhf9VYqh0
TALTA NI NANI?
Talta ambaye ni msichana mwenye asili ya Mkoa wa Kilimanjaro lakini mkazi wa Dar, ni meneja uzalishaji katika Kampuni ya Filamu ya Tuesday Entertainment, inayomilikiwa na Mtayarishaji wa Muvi Bongo, Tuesday Kihangala ‘Mr. Chuz’. Licha ya nafasi hiyo, pia ni mwigizaji aliyewahi kufanya mazoezi kwa karibu na Scorpion.
Mrembo huyo alisema yeye amekuwa akifanya mazoezi ya karate na mtuhumiwa huyo.
img_20161013_115417Talta Msofe akiwa katika pozi.
MLIKUTANAJE NA SCORPION?
“Mimi nilikwenda pale ofisini kwa Chuz kufanya kazi ya usekretari. Sasa kufika pale ndiyo baadaye nikawa najifunza mambo mengine ikiwa ni pamoja na uigizaji. Ninakumbuka wakati f’lani tulitaka mtu wa kuigiza filamu za action (matukio), tukatafuta watu, wakapatikana wawili lakini hawakufikia viwango.
“Ndipo siku moja, Chuz akasema kuna jamaa yake anaitwa Samjet atamfuata. Kweli alimpata na kuwa naye. Kwa pale mazoezini alikuwa mtu mzuri. Lakini pia alikuwa mzuri zaidi kwenye karate, anaruka sana juu na ni mtaalamu wa mapigano. Wakati tukifanya mazoezi ya filamu, ndiyo akawa ananifundisha karate mimi.”

ULIPATAJE TAARIFA ZA KUMAKATWA KWA SCORPION?
“Siku hiyo tulikuwa Morogoro kikazi ndiyo zikasambaa zile taarifa kwamba Scorpion amekamatwa kwa madai ya kumtoboa mtu macho. Tulishtuka sana.”
Talta alisema: “Tukapiga simu yake tukiamini ataipokea mwenyewe lakini kilichotokea sasa, simu ilipokelewa na dada yake wa kuzaliwa tumbo moja, tulipomuuliza kama habari tulizosikia ni kweli, akasema ni kweli.”

KAZINI, SCORPION NI MTU NAMNA GANI?
“Mh! Kwa kweli jamaa ni mtu fresh, mcheshi, anaweza akawa anakusikiliza labda unazungumzia stori yako, sasa kabla hujamaliza yeye akaanza kucheka kwelikweli. Mimi nilimuona yuko mwepesi hata kutoa ushauri.”
ALIWAHI KUGOMBANA NA MR. CHUZ?
“Yeah! Nakumbuka siku moja tukiwa Morogoro kikazi, Scorpion alikataa kuingia mitaani kushuti akisema lazima aende kwanza msikitini. Chuz yeye alisema asiende ashuti. Pakatokea kutoelewana kidogo. Lakini mwishowe, Chuz akamruhusu aende msikitini kwanza.”

WEWE AMEWAHI KUKUSHAURI NINI CHA MAANA?
“Mazoezi. Alikuwa ananiambia nifanye mazoezi hata baada ya yale tuliyokuwa tunafanya kwa ajili ya filamu. Ni kitu ambacho nilikubali na nafanya mazoezi mara kwa mara ya kujiweka vizuri kwa ajili ya kazi na mimi mwenyewe pia.”

ALIWAHI KUKUAMBIA NINI WEWE BINAFSI?
“Scorpion aliwahi kuniambia kwamba, angefurahi sana kama siku moja angempata mke mfanya mazoezi kama mimi, alisema anataka mke ambaye yuko vizuri kimwili kwa sababu ya mazoezi.”
img_20161013_115335
ALIWAHI KUKUAMBIA KWA NINI ALIAMUA KUWA MTU WA KARATE?
“Ndiyo. Alisema ilitokana na yeye kuonewa sana wakati akiwa mdogo. Katika vitu ambavyo hapendi, alisema ni kuonewaonewa. Kwa hiyo akaenda kujifunza karate na alipojiona yuko vizuri, akawa anajiamini sasa.”

ALIKUWA KAKA YAKO, USHAENDA KUMCHEKI MAHABUSU?
“Kwa kweli sijapata muda bado wa kwenda kumtembelea, lakini nadhani nikipata muda nitakwenda kumjulia hali.”

UNAFANYA MUVI ZA ACTION, HIZI ZA BABYBABY JE?
“Ninaweza kufanya kwa sababu zote ni kazi, lakini nafurahia zaidi hizi za action, filamu zangu zitatoka hivi karibu na mashabiki wataweza kuona Talta ni nani.”

UNAFANYA MAZOEZI, KWA HIYO VIBAKA WASIKUSOGELEE?
“Siyo kihivyo, lakini nipo vizuri. Huwezi kuniingilia kirahisirahisi.”

ALIYETOBOLEWA MACHO ALIZWA NA DIAMOND
Wakati huohuo, gazeti hili lilipokuwa likienda mitamboni, Said aliyedaiwa kujeruhiwa na Scorpion alikabidhiwa michango mbalimbali kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ aliyetoa shilingi milioni 2 ambazo zilimtoa machozi kutokana na kuguswa kwake na nyimbo za Diamond.
Said alilizwa na mchango huo wa Diamond kwani aliumizwa pia na kitendo cha kutobolewa macho kinachomfanya ashindwe kutazama video mbalimbali za msanii huyo ambaye alikuwa akimkubali uwezo wake.
Makonda alimkabidhi Said, shilingi milioni 10 na kumuahidi nyumba ya kuishi, Bajaj na pikipiki 5 ambazo zitamsaidia katika kuendesha maisha yake.

TUJIKUMBUSHE
Scorpion anadaiwa kumfanyia ukatili huo, Said, wiki chache zilizopita maeneo ya Buguruni Sheli jijini Dar es Salaam. Oktoba 12, mwaka huu, mtuhumiwa huyo alipandishwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa madai hayo. Shauri lake litatajwa tena, Oktoba 19, mwaka huu.
Imeandikwa na Ojuku Abraham na Erick Evarist.

No comments