Header Ads

Viongozi wa dini wasisite kuwaeleza ukweli wanasiasa

WAKATI wanasiasa humiliki vyombo vya dola  ambavyo vinajumuisha pingu, bunduki na ‘madege’ ya kijeshi, viongozi wa dini wao wana dhamana ya kumiliki nyoyo za binadamu wenzao kwa kupalilia ndani ya mioyo hiyo upendo, huruma, haki na ukweli ambayo ndiyo misingi ya kuishi kwa amani na kuheshimiana chini ya jua. 
 
Watu wanaofuatilia siasa za nchi hii kubwa iliyopo kusini mwa Jangwa la Sahara,  watabaini kwamba viongozi wa dini nchini wamekuwa wakishindwa kuzipaza sauti zao kwa wanasiasa kama wanavyozipaza kwa ujasiri kwa waumini wao ndani ya nyumba zao za ibada. Katika hali ya kawaida, viongozi wengi wa dini watakaoisoma safu hii, watafanya hivyo wakiwa wamenuna wakidhani haikuwatendea haki. 

Katika hali halisi -- kwa kuogopa au kujikomba -- viongozi wa dini wamekuwa hawataki  kuwaambia ukweli wanasiasa kuhusu tunavyotakiwa kuiendesha nchi yetu kwa misingi ya kuheshimiana na kutooneana.  Badala yake, viongozi hao wamejikita tu katika kusisitiza amani na utulivu tu, bila kuwa na ujasiri angalao kidogo tu wa kuwaambia wanasiasa kwamba amani ni zao la haki na kwamba bila haki hapawezi kuwepo amani. Na katika matukio mengi, viongozi haohao wa dini wamekuwa wakikwepa ukweli na mara nyingi wameungana na propaganda za wanasiasa kuelekeza lawama mahali pasipostahili – hususan kwa vyama vya upinzani.  

Hali hii ndiyo imetawala nchini kila jua linapochomoza mashariki ambapo viongozi wa dini wamejikuta wakinasa kwenye mitego ya wanasiasa kwa hiari yao au kwa kutokujua. Wakati mamilioni ya watu duniani hutegemea zaidi busara za viongozi wa dini na kuyaamini zaidi maneno yao kuliko ya wanasiasa, viongozi wa dini nchini wanaonekana kuusaliti ukweli huo kwa kukosa dira, wasijue pa kwenda na wakashindwa kuchagua kati ya mbingu na nchi.

 Limekuwa ni jambo la nadra sana kwa viongozi wa dini kusimamia ukweli kila inapojitokeza migogoro,
hususan ya kisiasa. Ni wachache sana miongoni mwao ambao wameheshimu kazi zao na wakawa jasiri na kusema ukweli kwa wanasiasa  na kila Mtanzania kila hali ya kutoelewana inapojitokeza katika nchi hii. Ifahamike kwamba migogoro mingi hapa nchini na duniani kote huanzishwa na wanasiasa – si mafundi cherehani, wahandisi au maseremala.  


Uhasama, chuki na kuuana kunakofanyika Syria, Iraq, Libya, Somalia, Congo (DRC) ya Joseph Kabila (pichani) ambayo ni nchi jirani na kadhalika, kulianzishwa na wanasiasa na ukaendelea kwa sababu watu wenye busara katika jamii, wakiwemo viongozi wa dini walishindwa kuwaambia ukweli wanasiasa.  Matokeo yake, mauaji ya maelfu ya watu yanaendelea hadi
leo katika nchi hizo na sehemu mbalimbali duniani wakati Mungu alitupa akili ya kujua jema na baya tangu enzi za Adam! Busara ya kweli duniani, inamtaka mtu aseme ukweli iwapo anataka sauti yake isikike na iheshimiwe. 


 Muungawana husema ukweli --  ukweli usiokuwa na mafumbo --  na akiogopa kufanya hivyo kwa sababu anazojua mwenyewe, hufunga mdomo wake.  Ni heri kufunga mdomo kuliko kusema kitu kitakachokufanya uonekane mpuuzi mbele ya jamii. Ifahamike wazi kabisa kwamba kutosema ukweli kwa ajili ya woga au kujikomba na hivyo kusababisha janga au madhara katika jamii, ni kushiriki moja kwa moja katika kuchochea janga hilo!  Ni vyema kufahamu kwamba majanga ya asili kama vile matetemeko ya ardhi, njaa au mafuriko,  huwa hayachagui mahali pa kufanya uharibifu.  

Vilevile, majanga ya kutengenezwa na kulelewa na binadamu, nayo huwa hayachagui mahali pa kuangukia; yakianza huwakumba walioyaanzisha,  waliokaa kimya na walioogopa kuyazuia wakati yanapangwa!

No comments