Header Ads

Kitimtim dakika 2 za Scorpion kizimbani jana DarMTUHUMIWA wa kesi ya unyang`anyi wa kutumia silaha, Salum Njwete (34), maarufu ‘Scopion’, jana alipanda kizimbani kwa dakika mbili kabla ya kesi yake kupigwa kalenda, lakini ulinzi uliimarishwa vikali wakati akiwa kwenye viunga vya Mahakama ya Ilala jijini Dar es Salaam.
 
Hakimu Frola Haule anayesikiliza kesi hiyo, alitumia dakika mbili kusoma na kupangia tarehe nyingine ya kutajwa kuwa Novemba 16.


Wakati mtuhumiwa akiwa kizimbani, kulikuwa na umati wa watu mahakamani hapo waliojazana katika madirisha na katika viunga vya mahakama kushuhudia.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa kwenye viunga vya mahakama hiyo saa 3:38 asubuhi na alipandishwa kizimbani saa 5:49 asubuhi kabla ya kuondolewa dakika mbili baadaye, chini ya ulinzi mkali wa askari ambao walimrudisha rumande.


Nipashe ilishuhudia ulinzi ukiimarishwa mahakamani hapo kabla ya kupandishwa kizimbani. Askari waliokuwa na bunduki walitangulia kufika mahakamani hapo na 'kusafisha' njia, tofauti na ilivyokuwa kwa watuhumiwa wengine.


Baada ya kupandishwa kizimbani, Wakili wa Serikali, Chesensi Gavyole, alisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaiomba mahakama kuipangia tarehe nyingine.
Hakimu Haule aliridhia ombi hilo na kuisogeza mbele hadi Novemba 16 itakapotajwa tena.
Kesi hiyo ilitajwa kwa mara ya kwanza jana tangu mshtakiwa huyo alipobadilishwa shtaka na Hakimu wiki mbili zilizopita, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuiondoa na kuirejesha tena.


Oktoba 19, Scorpion alifutiwa kesi kisha kusomewa upya mashtaka yake kutokana na uamuzi wa DPP aliyeomba kufanya hivyo baada ya hati ya awali kuwa na upungufu wa kisheria.


Mahakama ilikubali na kuifuta kesi hiyo, ambayo ilifikishwa ili kutajwa kwa mara ya tatu, lakini baada ya muda mfupi, Scorpion alifunguliwa mashtaka mapya baada ya DPP kufanya marekebisho ya kisheria na pia kupangiwa kwa Hakimu mwingine kutoka kwa yule wa awali.
Scorpion anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu eneo la Buguruni Sheli, wilaya ya Ilala kwa kuiba mkufu wa rangi ya fedha wenye uzito wa gramu 34, ukiwa na thamani ya Sh. 60,000, bangili na fedha taslimu Sh. 331,000, vyote kwa pamoja vikiwa na thamani ya Sh. 476,000, mali ya Said Ally.


Gavyole alidai kuwa mshtakiwa, kabla na baada ya wizi huo, alimchoma kisu machoni, tumboni na mabegani na kumwacha Ally na majeraha kwa lengo la kujipatia mali hizo.
Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo.


CHANZO: NIPASHE

No comments