Header Ads

Lwandamina Aanza Kazi Rasmi, Awafagilia Wachezaji Yanga
KOCHA mkuu wa Yanga SC George Lwandamina aliyeingia mkataba na Yanga SC hivi karibuni akitokea Zesco United nchini Zambia, leo ameanza kazi rasmi timu yake mpya ya Yanga SC

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Yanga ni kwamba, Lwandamina akiongozana na Mkurugenzi wa Ufundi Hans Van Pluijm walikuwa pembeni katika uwanja wa Polisi – Kilwa Road jijini Dar kushuhudia wachezaji 18 wa timu hiyo waliojitokeza siku ya kwanza leo mazoezini chini ya kocha msaidizi Juma Mwambusi baada ya mapumziko ya mwezi mmoja.

Wachezaji waliokosa mazoezi ya leo ni pamoja na;
1. Donald Ngoma
2. Hassan Kessy
3. Malimi Busungu
4. Yusufu Mhiru
5. Haruna Niyonzima
6. Obrey Chirwa
7. Vicente Bossou
8. Beno Kakolanya

(Wote hao uongozi unataarifa zao)


Lwandamina baada ya mazoezi akiongozana na mwenyeji wake Hans Van Pluijm , walizungumza na wachezaji . Kocha huyo mwenye wingi wa bashasha alisifu morali na ari ya wachezaji kujituma mazoezini .

” Nimeshuhudia hali ya kujituma, nidhamu ya kumsikiliza mwalimu na uelewa mzuri kutekeleza majukumu mliyopewa. Ni mpongeze mwalimu kwa mazoezi mazuri ya ” warm up ” baada ya likizo ndefu . Mkiendelea na morali hii hakika benchi la ufundi tutakuwa na kazi rahisi sana kufikia malengo yetu”

Kikosi kimeanza mazoezi mapema kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu pia kumpa nafasi nzuri mwalimu kuingiza mifumo na falsafa zake ili ligi itakapoanza wachezaji wawe tayari wamemuelewa na ibaki utekelezaji tu.

Naye Hans Van Pluijm mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo ambaye hapo awali alikuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, amewasifu wachezaji kujitokeza kwa wingi siku ya kwanza na kuonesha morali kubwa.

“Mmeonesha morali nzuri na mnaonesha mna stamina nzuri . Hii inaonesha likizo mmeitumia vizuri kwa mazoezi binafsi ” alichombeza Hans Van Pluijm.

Mwalimu Lwandamina anaonekana kuipenda Tanzania pia kuanza kuzoea mazingira ya nchi hii na ameomba kuona viwanja vingine viwili au vitatu tofauti tofauti kwa ajili ya mazoezi ya kikosi hicho cha mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.


Kikosi kitaendelea na mazoezi yake kesho kama kawaida kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo pamoja na mashindano ya klabu bingwa hapo mwakani.

No comments