Header Ads

SITALIA TENA-22

Kareem alikuwa akilia, hakuamini alichokuwa akikiona mbele yake, moyo wake ulimuuma mno, alimpenda Saida na alikuwa tayari kufanya kitu chochote kile kwa ajili yake lakini kitendo cha jumba lile kulipuliwa, akaona kwamba mpenzi wake alikuwa amekufa.
Alikuwa akilia, watu walianza kujaa mahali hapo, kila mtu alikuwa akiogopa na watu wote walihisi kwamba ni magaidi ndiyo waliofanya tukio hilo. Kareem akakimbua mpaka pale kulipokuwa na vifusi vya nyumba ile na kuanza kuangalia kuona kama angeweza kumuona Saida.
Miili ilikuwepo lakini hakuweza kugundua ni mwili upi ulikuwa wa msichana wake, miili yote iliunguzwa vibaya kitendo cha kutokugundua mwili wa mpenzi wake ulikuwa upi. Alibaki akilia mpaka baada ya saa moja ambapo gari la wagonjwa likafika na kutoa miili iliyokuwepo mahali hapo.
Kareem akapanda ndani ya gari la wagonjwa na kuelekea hospitali, bado moyo wake haukuridhika, alitaka kujua kuhusu miili ile ya watu kama kulikuwa na mwili wa mpenzi wake.
Haikuwa safari ndefu wakafika huko, miili ilipoteremshwa naye akateremka, hakuacha kulia, moyo wake ulikuwa na majonzi tele na muda mwingi alikuwa akimfikiria mpenzi wake huyo.
“Mpenzi wangu amekufa,” alisema Kareem huku akimwangalia daktari.
“Ni mwanamke?”
“Ndiyo!”
“Mmh!”
“Kuna nini daktari? Niambie, hata kama amekufa, naomba uniambie,” alisema Kareem huku akimbembeleza daktari amwambie ukweli.
“Kwa ile miili iliyoletwa, hakuna hata mwili wa mwanamke! Sasa sijui una uhakika kama naye alikuwepo eneo la tukio au la,” alisema daktari huku akimwangalia Kareem.
“Hakuna mwili wa mwanamke?”
“Ndiyo! Wote wanaume! Tumewachunguza kwa umakini!” alijibu daktari huyo.
Kareem alichanganyikiwa, alipoambiwa kwamba miili ya watu waliokuwa wamekufa katika jengo lile ilikuwa ni ya wanaume tu na hakukuwa na mwanamke, alishindwa kuamini, akawaambia madaktari kwamba na yeye alitaka kwenda kuangalia ili awe na uhakika kama kweli wale walikuwa wanaume tu.
Akaelekea mochwari ambapo baada ya kuingia na majokofu kufunguliwa, akaamini kwamba hakukuwa na mwanamke, wote walikuwa wanaume kitu kilichompa maswali mengi kichwani mwake.
“Saida yupo wapi sasa? Maiti yake imeachwa wapi?” alijiuliza.
Hakutaka kubaki hospitalini hapo, alichokifanya ni kuondoka kuelekea kule nyumbani ambapo baada ya kufika, akaanza kuutafuta mwili wa mpenzi wake. Ulikuwa ni usiku na usiku mzima alibaki akiutafuta lakini akashindwa kitu kilichomchangany zaidi.
Hakuondoka, alibaki hapohapo mpaka asubuhi ambapo magari yakafika na kuanza kutoa vifusi huku waandishi wa habari wengi wakiwa tayari wamekusanyika mahali hapo kuripoti kile kilichokuwa kikiendea kwani bilionea Faraq alikuwa mtu maarufu nchini Misri.
Vifusi vilitolewa, magari yalikusanyika mahali hapo, Kareem alikuwa amesimama pembeni huku macho yake yakiangalia kazi iliyokuwa ikiendelea mahali hapo. Wakati magari hayo yakiwa yamechukua saa moja kutoa vifusi ndipo macho ya waokoaji yakatua katika mwili mmoja, ulikuwa chini ya handaki, wakaitana ili kila mmoja aone kilichokuwa kimetokea.
“Njooni! Kuna mwili huku,” alisema mwanaume mmoja, waokoaji wengine wakasogea kule, hata Kareem naye akaenda huko huku akiwa na hamu ya kuona huyo mtu alikuwa nani.
Alifukiwa na kifusi, alikuwa kimya kabisa, mwili mzima ulijaa vumbi na hata alipotolewa, ilikuwa ngumu kufahamu kama alikuwa Saida. Mapigo yake ya moyo yalikuwa yakidunda kwa shida sana, Kareem alipomfikia, akamwangalia vizuri.
“Ni mpenzi wangu! Ni mpenzi wangu,” alisema maneno ambayo yalimshtua kila mtu.
Wakamchukua Saida na kumpakiza katika gari moja lililokuwa mahali hapo na kumpeleka hospitali. Kareem hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya na yeye ni kuelekea huko huku akiwa pembeni ya mpenzi wake.
Alikuwa akilia, alimwangalia Saida, alionekana kuwa katika hali mbaya kupita kawaida. Kareem alikuwa akilia, kila alipokuwa akimwangalia Saida, moyo wake ulimwambia kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa maisha ya msichana huyo.
“Saida, tafadhali naomba usiniache, usife mpenzi, ninakupenda, nitabaki kwenye hali gani ukifa? Naomba usiniache mpenzi,” alisema Kareem huku akimwangalia Saida, moyo wake ulikuwa na maumivu makali mno.
Walipofika hospitali, Saida akashushwa, akawekwa kwenye machela na kisha kuanza kupelekwa ndani ya hospitali hiyo. Kila mtu alikuwa akimwangalia, alimuonea huruma, alikuwa kwenye hali mbaya huku mwili wake ukiwa na vumbi jingi.
Walipofika katika chumba kilichoandikwa Theatre, Kareem akaambiwa asubiri kwenye viti vilivyokuwa nje ya chumba hicho. Hakutaka kukaa, alisimama huku akizunguka huku na kule, kitu pekee alichokuwa akikitaka ni kuona mpenzi wake akipona na kurudi katika hali kama aliyokuwa zamani.
“Mungu! Hivi kwa nini tunapitia katika maisha haya? Kwa nini kila siku maisha yamekuwa hivi? Mungu, naomba umsaidie Saida apone,” alisema Kareem huku akizunguka huku na kule pale alipokuwa ameachwa.
Matibabu yalichukua saa mbili huku madaktari wakiingia na kutoka kwa zamu. Baada ya muda huo wakamruhusu Kareem aingie ndani ya chumba kile ambapo alimkuta Saida akiwa kitandani huku akipumua kwa msaada wa mashine ya oksijeni.
Moyo wake ulifurahi kumuona akiwa hai kwani kitu alichohisi ni kwamba mpenzi wake huyo angekuwa amefariki kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo saa chache zilizopita. Akajikuta akipiga magoti ndani ya chumba kile na kumshukuru Mungu kwa kazi kubwa aliyokuwa ameifanya.
Hakuacha kulia, kila wakati alimshukuru Mungu huku machozi yakimtoka. Alipata tumaini jipya moyoni mwake, akaona Mungu akimpigania kitu ambacho kwake kilionekana kama muujiza mkubwa.
“Atatakiwa kupumzika. Nafikiri unaweza kwenda nyumbani na kurudi jioni,” alisema daktari huyo.
“Hakuna shida, Nitarudi!” alisema Kareem na kuondoka, alitaka kupumzika kwanza.
****
“Kuna chochote mmekipata?” ilisikika sauti kutoka kwenye simu iliyoshikiliwa na jamaa mmoja aliyevalia kanzu kubwa, kilemba kichwani na alikuwa na mshipi kiunoni mwake, mkono wake wa kushoto alishikilia bunduki kubwa aina ya AK 47.
“Ndiyo mkuu!”
“Kipi?”
“Taarifa za awali zinasema kwamba kabla ya kiongozi kuuawa, ndani ya nyumba ile kulikuwa na wapelelezi wawili, mwanamke na mwanaume ambao walikuwa wakiishi humo, walifika kwa ajili ya kumpeleleza Bwana Faraq,” ilisema jamaa huyo.
“Ilikuwaje mpaka waliingia humo?”
“Hatujui! Sisi wenyewe tumeshangaa na kwa siku mbili walizokaa humo, watu walikuwa wakishangaa sana, hakukuwa na aliyejua kama walikuwa wapelelezi,” alisema jamaa huyo.
“Hao watu wapo wapi?”
“Taarifa zinasema msichana amepelekwa kwenye hospitali moja hapahapa Casablanca baada ya kuangukiwa na kifusi na tunaamini kwamba bado watakuwa huko mkuu.”
“Basi nendeni mkawachukue wote. Sitaki kuwaona, ninachotaka muwateke na kuwatesa, wapelekeni kwenye mapango, huko, wateseni mpaka waseme ni nani aliyewatuma,” alisema kiongozi huyo.
“Hakuna shida mkuu! Ngoja nitume vijana kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo mkuu,” alisema jamaa huyo.
“Sawa. Hakikisheni mnawatesa sana mpaka wawaambie ukweli. Umenielewa?” aliuliza upande wa pili.
“Ndiyo mkuu!”
“Basi sawa. Nataka nipewe taarifa nzuri baada ya saa moja.”
“Hilo ondoa shaka, nitafanya hivyo,” alisema jamaa huyo na kukata simu. Kazi iliyobaki ilikuwa ni kuwateka watu hao tu. Vijana wakaandaliwa na kuanza kwenda huko.

Je, nini kitaendelea?
Je, Saida atapona?
Je, magaidi hao watafanikiwa kuwateka?

No comments