Header Ads

SITALIA TENA - 26 (MWISHO)


NYEMO CHILONGANI

Saida hakutaka kubaki nchini Misri, alichokifanya ni kumwambia balozi kwamba alitaka kuondoka kurudi nchini Tanzania. Mipango ya safari ikaanza kufanyika na usiku huohuo tiketi ya ndege ikapatikana na hivyo Saida kutakiwa kuondoka Misri.
Hilo likamfanya kuwa na amani moyoni mwake, Kwa Kareem, hakuwa na furaha, hakutaka kuona akikaa mbali na mpenzi wake, alimpenda kuliko kitu chochote kile katika maisha yake, kila siku, moyo wake ulikuwa na shauku ya kuishi naye maisha yake yote.
Walikuwa na ndoto ya kupata mtoto, hawakuweza kumpata kwa sababu mimba iliharibika, moyo wake ulimuuma mno na kutokana na matatizo aliyokuwa amepitia na mpenzi wake, Saida, akamuahidi kwamba ni lazima wapate mtoto hata kama ingechukua muda gani.
Wakati wakiendelea kusibiri asubuhi iingie ndipo Kareem akapata taarifa kwamba baba yake alikuwa ndani ya ndege iliyopotea. Moyo wake ulimuuma mno na kulikuwa na tetesi kwamba ndege hiyo ilipotezwa makusudi na abiria wote walikuwa wameuawa.
Alihuzunika mno lakini hakuwa na jinsi kwani kuwa na Saida tu kuliufanya moyo wake kuwa na furaha tele. Asubuhi ilipofika, akaongozana na ulinzi mkubwa wa nyumbani kwa balozi na kwenda benki, akatoa kiasi kikubwa cha fedha, dola laki moja kwa ajili ya Saida, kiasi hicho kikaingizwa katika akaunti ya benki ya Tanzania ya mwanamke huyo.
Siku iliyofuata, wakaagana huku kila mmoja akilia, Saida akapanda ndege na kuanza safari ya kuelekea nchini Tanzania huku ndugu zake wakiwa wamekwishapigiwa simu na kuambiwa kwamba mwanamke huyo alikuwa njiani kuelekea huko.
Ndege ilichukua saa kadhaa mpaka kufika nchini Tanzania. Wazazi wake, ndegu zake, marafiki na watu wengine walifika uwanja wa ndege, hawakuwa hao tu bali hata waandishi wa bahari nao walifika mahali hapo kwa ajili ya kujionea kwa macho yao msichana huyo.
Alipotoka ndani ya jengo la uwanja huo, ndugu zake wakamsogelea na kumkumbatia, walikuwa na furaha mno kwani kila mmoja alijua kwamba tayari alikufa hasa baada ya kuwa mikononi mwa wauza madawa ya kulevya.
“Mungu wangu! Upo hai? Siamini,” alisema rafiki yake, Salama.
“Namshukuru Mungu! Ni safari ndefu sana, bila Mungu, ningekwishakufa kitambo,” alijibu Saida huku akilia, moyo wake ulimuuma mno kila alipokumbuka kule alipopitia kabla ya kurudi nchini humo.
Huo ulikuwa muda wa kuyafurahia maisha, hakutaka kusafiri kuelekea nchi za Kiarabu tena. Mawasiliano yake na Kareem yaliongezeka, alifungua biashara nyingi na kuingiza kiasi kikubwa cha fedha.
Kareem hakutaka kukaa sana Oman, alichokifanya ni kusafiri mpaka Tanzania, alipokelewa na msichana wake na kuishi naye, na hukohuko ndipo akaamua kumuoa Saida, hakutaka kusafiri naye kuelekea Oman kwa kuamini kwamba maisha yake yangekuwa hatarini kwani bado alihitajika sana nchini humo.
Akaishi nchini Tanzania kwa miezi sita, huku tayari akiwa amefanikiwa kumpa ujauzito mke wake, Saida na miezi kadhaa iliyofuata, akajifungua mtoto wa kiume na kumpa jina la Casmir.
Kareem akaipenda familia yake zaidi ya kitu chochote kile. Alikuwa bilionea mkubwa hivyo aliitaka hata familia yake kuishi katika maisha ya kitajiri. Alikumbuka namna alivyopata tabu, alikumbuka namna alivyoteseka kwa ajili ya Saida, hakutaka kumuacha, aliona kwamba yeye ndiye alikuwa mfariji mkubwa kwa mwanamke huyo.
Mapenzi yakanoga, yakawa motomoto, kwa Saida, hakukuwa na majonzi tena, hakulia tena, kila siku kwake ilikuwa ni furaha tele. Ni mara chache sana Kareem alikuwa akiishi Oman, muda mwingi alikuwa nchini Tanzania na familia yake.
Siku zikakatika na kukatika, baada ya miaka miwili, Saida akapata mimba tena na alipojifungua miezi tisa mbele akampa mtoto wa kike na kumpa jina la Aisha.
“Ninakupenda mume wangu,” alisema Saida huku akimwangalia mumewe.
“Ninakupenda pia. Nipo tayari kupoteza kila kitu ila si kukupoteza wewe. Tumetoka mbali sana, unakumbuka?” aliuliza Kareem huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
“Nakumbuka mpenzi! Nashukuru kwa kujitoa. Hakika umekuwa mwanaume bora katika maisha yangu. Ninakupenda, hiyo siyo siri, kila mtu anajua kwamba ninakupenda mno mno mno,” alisema Saida na kumkumbatia mume wake, Kareem.
Utajiri wao ukaendelea kuongezeka, Saida alikuwa na kazi ya kuziendesha biashara zilizokuwa nchini Tanzania. Wakaanzisha kampuni ya kusambaza mafuta Tanzania na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Maisha yake yaliyobaki yakawa ni kuogelea kwenye utajiri mkubwa, hakuishi katika maisha ya kimasikini kama zamani. Na hata kipindi alichoamua kukiandika kitabu cha maisha yake na kukiita SAIDA: SITALIA TENA, kila mtu hakuamini kile alichokisoma.
Huku kila mmoja akijua kwamba safari ya kutoka nchini Oman kwenda Tanzania ilikuwa ni ya kawaida kumbe hawakuwa sahihi. Ilikuwa safari yenye kuumiza, yenye mateso ambayo kwa mtu mwingine angeweza kufa hata kabla ya kufika Tanzania.
Saida alionekana kuwa shujaa mkubwa, aliyefanikiwa kukitoroka kifo wakati kikimuhitaji. Kila mmoja akamsifia na kumpongeza. Kitabu chake kiliingiza mamilioni ya shilingi na fedha zote kuwasaidia watu wasiojiweza, wagonjwa wa magonjwa ya moyo yaliyokuwa yakiwasumbua watu wengi nchini Tanzania.
Historia ya maisha yake kutoka nchini Oman mpaka Tanzania ikaishia hapo. Akasahau kila kitu, akaanza upya na maisha yaliendelea kama kawaida. Moyo wake ukawa na tumaini jipya, hakutaka kulia tena, huo ulikuwa muda mwingine wa kuyafurahia maisha yake.

MWISHO

No comments