Header Ads

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAFANIKIO YA HOSPITALI KWA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA WA AWAMU YA TANO TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MAFANIKIO YA HOSPITALI KWA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA WA AWAMU YA TANO YA UTAWALA WA
MH. RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
DKT. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI

1.0 Utangulizi:
Bodi ya Wadhamini, Menejimenti na Wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wanapenda kumpongeza kwa dhati Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kutimiza mwaka mmoja tangu kuapishwa kwake kuongoza taifa hili. Aidha tunampongeza kwa kazi kubwa anayoifanya ya kujenga uchumi na kuwaletea maendeleo Watanzania katika sekta mbalimbali ikiwamo Sekta ya Afya.

1.1 Ziara ya Mh. Rais katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
Mnamo tarehe 9 Novemba, 2015 ikiwa ni siku nne baada ya Mhe. Rais kuapishwa alifanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kukutana na changamoto kadhaa ambapo alitoa maagizo kwa Uongozi wa Hospitali kwamba, mashini ya Magnetic Resonance Imaging (MRI) na Computerized Tomography Scan (CT-Scan) ambazo zilikuwa zimeharibika ziwe zinafanya kazi katika kipindi cha siku 14, wagonjwa waliolala chini wawe wamepata vitanda pamoja na wagonjwa wote kupata dawa kupitia maduka ya dawa yaliyopo Hospitalini hapa. Na kuagiza Bohari Kuu ya Dawa (Medical Stores Department–MSD), kufungua duka la dawa ndani ya Hospitali ili kuondoa ukosekanaji wa dawa ambao ulikuwa unasababisha wagonjwa walazimike kununua dawa katika maduka binafsi yaliyopo nje ya Hospitali.

1.2 Utekelezaji wa Maagizo ya Mh. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
1.2.1 Matengenezo ya mashini ya MRI
Matengenezo ya mashini hii yalifanyika kikamilifu na hadi hivi sasa mashini hii inaendelea kufanya kazi vizuri ambapo kwa kipindi cha Disemba 2015 hadi Oktoba 25, 2016 wagonjwa 17,951 wamepimwa ukilinganisha na wagonjwa 1,911waliopima Disemba 2014 hadi Oktoba 2015. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 839.35.

1.2.2 Matengenezo ya mashini ya CT-Scan
Mashini hii ilitengenezwa kikamilifu na hadi hivi sasa mashini hii inaendelea kufanya kazi vizuri ambapo kwa kipindi cha Disemba 2015 hadi Oktoba 2016 wagonjwa 10,259 wamepimwa ukilinganisha na wagonjwa 3,319 waliopimwa Disemba 2014 hadi Oktoba 2015. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 209.09.  Tathimini ya vipimo vya radiolojia kwa ujumla wake vinavyojumuisha (MRI, CT-Scan, Utra-Sound na Plain X-Ray) inaonesha kuwa kwa kipindi cha Disemba 2015 hadi Oktoba 2016 wagonjwa 55,073 wamepimwa ukilinganisha na wagonjwa 23,989 waliopima Disemba 2014 hadi Oktoba 2015. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 129.57.

1.2.3 Wagonjwa waliolala chini kupewa vitanda
Agizo hili lilitekelezwa kufuatia kuhama kwa wagonjwa wa Taasisi ya Mifupa (MOI) kutoka wodi za Hospitali ya Taifa Muhimbili walizokuwa wakitumia ambazo ni wodi 17, na 18 zilizoko jengo la Sewahaji pamoja na wodi namba 2 iliyoko jengo la Mwaisela ambayo kwa sasa ni ICU yenye vitanda 15. Aidha Mh. Rais aliipatia Hospitali jengo lililokuwa likitumiwa na Wizara ya Afya kama ofisi ambalo kwa sasa limekuwa wodi na kutupatia nafasi ya vitanda 91.

1.2.4 Upatikanaji wa dawa Hospitalini
Kuhusu upatikanaji wa dawa Hospitalini, kwa sasa wagonjwa wanapata dawa kwa zaidi ya asilimia 96 kutoka kwenye maduka ya dawa ya Hospitali. Tumeboresha mfumo wa Tehama katika utoaji na uagizaji dawa, na wagonjwa wanaokosa katika maduka yetu, Hospitali inanunua haraka ili mgonjwa huyo aweze kupata dawa. Kwa sasa ukosekanaji wa dawa Hospitalini umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kuimarisha utendaji ndani ya Hospitali. Kabla ya hapo upatikanaji wa dawa ulikuwa chini ya asilimia 35 hadi 45.
2.0 Mafanikio ya Hospitali kwa upande wa huduma
2.1 Huduma za Tiba
a.    Hospitali imeendelea kuboresha huduma mbalimbali ambapo kwa upande wa wagonjwa wanaoonwa na kuondoka (OPD) jitihada kubwa imefanyika kwanza kwa kuweka mkakati wa kuanza kliniki saa 03:00 asubuhi.
b.    Tumeanzisha kliniki za jioni ambapo mteja hana haja ya kuja asubuhi anaweza kuja hata saa tisa na tunahudumia hadi saa 12 jioni.  Tumeanzisha pia kliniki za jumamosi pamoja na siku za sikukuu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa tisa mchana ili kutoa fursa kwa mgonjwa kuwa na uamuzi wa muda wa kutibiwa ili kuepusha wagonjwa wote kuja asubuhi na kujikuta wanasubiri muda mrefu.
c.    Kwa upande wa muda wa kusubiri hususani kulipia huduma wakati wowote kuanzia sasa Hospitali itaingia katika mfumo wa kulipia kupitia kadi au simu za mkononi. Hii yote ni jitihada ya kuondoa muda wa kusubiri kabla, wakati na baada ya kupata huduma.
d.    Aidha, Hospitali imejenga wodi ya kisasa kwa ajili ya wagonjwa binafsi (Private) na mashuhuri (VIP) iliyopo wodi 18 kwenye jengo la Sewahaji ili kukidhi kwa kuanzia mahitaji ya wagonjwa hao.

 2.2 Huduma za Upasuaji
a.    Kasi ya kufanya upasuaji imeongezeka ambapo sasa hivi tunafanya upasuaji kila siku wagonjwa kati ya 40 hadi 50 kuanzia jumatatu hadi ijumaa wakati siku za mwisho wa juma jumamosi na jumapili pamoja na siku za sikukuu upasuaji ni kati ya wagonjwa 15 hadi 20. Ambapo kabla ya hapo upasuaji ulikuwa chini ya wagonjwa 10.
b.    Katika kuongeza wigo wa wagonjwa wanaohitaji kufanyiwa upasuaji, Hospitali inaongeza vyumba vya upasuaji saba kutoka 13 vya sasa ili kufikisha 20.
c.    Hospitali inaanzisha vyumba vya uangalizi maalum (ICUs) katika Wodi Na. 2 vitanda 15, Wodi 35 vitanda 5, na step down ya vitanda 5, Neonatal vitanda 10, stepdown neonatal 15, Paed vitanda 15, na step down vitanda 15.
d.    Mkakati huu utaongeza vitanda vya ICU kutoka 21vilivyopo sasa kufikia 101 sawa na ongezeko la vitanda 80. Hii ni sawa na asilimia 67.3 ya takwa la Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linalotaka kila Hospitali kuwa na asilimia 10 ya vitanda vya ICU dhidi ya vitanda ilivyonavyo. MNH ina vitanda karibu 1,500 hivyo inatakiwa kuwa na vitanda 150 vya ICU. Kwa hiyo bado tunahitaji vitanda 49kutimiza sharti hilo.
e.    Hali kadhalika Hospitali inaongeza vyumba vinne vya wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu baada ya wagonjwa kutoka ICU (step-down ICU) na kabla ya kwenda kwenye wodi za kawaida navyo vitakuwa na vitanda 40.
f.    Pia tumeanza kwa muda kufanya upasuaji kwa njia ya hadubini (Endoscopic and Laparascopic Surgeries) hususani kwa magonjwa ya masikio, pua na koo, na katika eneo hili idara ya urolojia inaongoza katika matumizi ya technologia hii mpya.

2.3 Huduma za uchunguzi
2.3.1 Maabara
Kwa upande wa maabara tumeongeza vifaa vipya vya kisasa katika kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa ubora wa hali wa ya juu. Kuna mashini mpya ya Architect Analyzer C4100 ambapo mashini moja inaweza kupima vipimo zaidi ya 1,200 kwa saa moja ili kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri majibu kwa muda mrefu. Hospitali imeweka mashini zote ambazo zifanya kazi kupitia mtandao (automated) eneo moja na zipo karibu na kompyuta ambazo zinatumika kupokea na kuhakiki sampuli zinazotakiwa ndani ya maabara.

2.3.2 Mashini Mpya ya CT-Scan
Kutokana na mahitaji makubwa ya vipimo kupitia mashini za CT-Scan, Hospitali ilinunua mashini mpya ya CT-Scan yenye uwezo wa 126 slices. Uwepo wa mashini hii mpya umeongeza uwezo kwa kiwango kikubwa wa kupima wagonjwa wengi kwa wakati mmoja na tunaweza sasa kumpima mgonjwa mmoja tumbo na kifua kwa sekunde 6. Hivyo, tulikuwa tunapima wagonjwa wastani wa 20 sasa tunapima wagonjwa wastani wa 50 ndani ya saa 24. Baada ya kuwepo kwa mashini hizi mbili za CT-Scan, Hospitali haitegemei tena kukosekana kwa vipimo vinavyohitaji mashini hizi. Aidha mashini hii mpya ambayo ni ya kisasa zaidi na yenye nguvu kubwa imewezesha kufanya vipimo vya kiutalaam zaidi hasa kwa upande wa viungo vya ndani kama moyo, utumbo, ubongo n.k na hivyo kupata uchunguzi sahihi na uhakika.
3.0 Kupunguza Rufaa za Nje
a.    Hospitali ya Taifa Muhimbili inaendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje kwa vitendo ambao mara nyingi walikuwa wakifuata matibabu yasiyopatikana hapa nchini ama kutokana na kutokuwepo wataalamu au ukosefu wa vifaa vya kutolea huduma husika.
b.    Katika kutekeleza hilo, Septemba 25, 2016, Hospitali ilipeleka watalaamu saba nchini India katika Hospitali ya Apollo iliyopo New Delhi ili wakajifunze kwa njia ya vitendo jinsi ya kufanya upasuaji na upandikizaji wa kifaa cha usikivu kwa watu wazima na watoto. Wataalamu hawa wamerudi.  Gharama za kupandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto mmoja ni kati ya shilingi milioni 80 hadi 100 anapopelekwa nje ya nchi. Takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili zinaonyesha kuwa asilimia 95 ya wagonjwa ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa kuwekewa kifaa cha usikivu ni watoto wadogo na kusisitiza kuwa huduma hii itasaidia watoto wengi hapa nchini na pia kujenga uwezo kwa wataalamu wa ndani ya nchi. 
c.    Kuhusu wagonjwa wanaokwenda nje kupata huduma za upandikizaji wa figo ambapo ifikapo mwanzoni mwa mwaka 2017 Hospitali itaweza kupandikiza figo hapa hapa nchini na kupanua huduma za kusafisha figo kutoka uwezo wa kuwa na mashini 23 mpaka kufikia machine 50 na pia kuongeza shift za kuchuja figo kutoka mbili za sasa mpaka kufikia 3 na pia kuchuja figo za wale wenye maambukizi ya ukimwi na hepatitis na kuweka mtambo wa kuchuja maji (water-treatment plant).
d.    Aidha Hospitali ya Taifa Muhimbili imepeleka nchini India wataalamu 18 wa fani mbalimbali kwa ajili ya kujengewa uwezo wa upandikizaji figo kwa watu wenye matatizo ya figo na timu hiyo inatarajia kurejea mwishoni mwaka. Mgonjwa mmoja anayepandikizwa figo nje ya nchi pia hugharimu kiasi cha shilingi milioni 40 hadi 60.
e.    Uwepo wa huduma hizi hapa nchini utawezesha Watanzania wengi kupata huduma hii na kwa gharama nafuu zaidi na kupunguza mzigo kwa Serikali wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwani gharama za matibabu zitapungua kwa zaidi ya asilimia 50 hadi 60.
4.0 Maafanikio mengine
4.1 Kuongezeka kwa Mapato zaidi ya asilimia 100
Baada ya kuongeza kasi ya usimamizi wa wafanyakazi na kupunguza kero za wafanyakazi Hospitali imeongeza uzalishaji wenye tija kwa kiwango kikubwa sana ambapo takwimu zinaonesha kuwa kuanzia Disemba, 2015 hadi Oktoba 2016 Hospitali ilizalisha wastani wa kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kwa mwezi kutoka wastani wa shilingi bilioni 2.3 ilizokuwa ikizalisha kwa kipindi kama hicho cha Disemba 2014 hadi Oktoba 2015. Mwelekeo wa mapato kuanzia Julai 2016 hadi Oktoba 2016 unaonyesha uzalishaji kuwa shilingi bilioni 4.6 kwa mwezi. Haya ni mafanikio makubwa sana kwa upande wa mapato kuwahi kupatikana katika kipindi kifupi sana cha miezi miwili tu. Tumeona Hospitali ina fursa kiasi gani ya kuzalisha kiasi kingi cha fedha na hivyo kuweza kujitosheleza kwa kiwango kikubwa katika uendeshaji wa shughuli zake kutokana na mwelekeo wa mapato yalivyo.

4.2 Kupunguza kero za Wafanyakazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili
Katika kipindi cha mwaka mmoja Hospitali imeweza kulipa wafanyakazi malimbikizo ya madai yao ambayo walikuwa wakidai kwa kipindi kirefu kama malipo ya on call, malipo ya wauguzi ya usiku, malipo ya posho mbalimbali hususani kwa madaktari pamoja na kada nyingine za afya ambazo zinashughulika moja kwa moja na wagonjwa, nauli za likizo pamoja na mambo mengine. Hali hii ilishusha morali kwa kiwango kikubwa sana na hivyo wafanyakazi kupunguza kasi ya ufanyaji kazi kwa kujituma na matokeo yake ni kukosekana kwa tija katika utoaji huduma.

4.3 Kuongezeka kwa Morali ya Kufanya kazi
Hali ilivyo sasa inaonyesha kuwa wafanyakazi wengi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wana hari ya kufanya kazi na ndiyo maana unaweza kuona mapato yameongezeka. Kwa sasa morali ya ufanyaji kazi imeongezeka kama inavyothibitishwa na kuongezeka kwa kliniki za muda wa ziada.

4.4 Usimamizi wa Utendaji Kazi
Baada ya kupunguza kero za wafanyakazi, Menejimenti imeongeza kasi ya kusimamia wafanyakazi ili kuhakisha wanafikia malengo waliyokusudia katika kipindi cha mwaka husika.

4.5 Ulipaji wa Madeni
Hospitali kwa sasa kulingana na uzalishaji unaonekana, inajitahidi kupunguza madeni iliyonayo kwa wazabuni mbalimbali wakiwemo wanaofanya matengenezo kinga ya vifaa tiba vya Hospitali.

4.6 Kupunguza Matumizi
a.    Hospitali pia imejiwekea mikakati wa kupunguza gharama za manunuzi pale inapowezekana na moja ya mikakati hiyo ni kununua dawa na vifaa tiba kutoka viwandani (Manufacturers) moja kwa moja. Kwa mfano, baada ya kupata kibali kutoka TFDA, Hospitali imenunua dawa za figo (immunosuppressant) kutoka nchini India kwa Shilingi milioni 226 wakati hapa nchini zingegharimu Shilingi milioni 500.
b.    Katika mkakati huu huu, Hospitali imeagiza nyuzi za kushonea wagonjwa (sutures) kutoka kiwandani (Ethicon) kwa gharama ya Shilingi 321 milioni wakati hapa ingegharimu Shilingi milioni 668; matumizi haya ni ya robo mwaka.
c.    Aidha Hospitali imeweza kupunguza gharama za uchujaji wa damu (dialysis) kutoka wastani wa TShs. 250,000 kwa kila zamu (session) na kuwa TShs. 171,000/= ambayo inajumuisha pia heparin na huduma.  Zoezi hili limefanya Hospitali kuhudumia wagonjwa 31 ambao hawawezi kulipia gharama hizi. Hii ni hatua kubuwa sana.

4.7 Kuunganisha mashini katika mfumo wa kiiletroniki
Hospitali pia imeweza kuunganisha (integrate) mashini za CT scan, X-Ray na MRI katika mtandao wa TEHAMA ambapo Hospitali katika kuhakikisha picha zote zinazofanyika katika idara hiyo zinaonekana na kupata idadi ya wagonjwa waliofanya vipimo na kulinganisha kiasi cha mapato kilichokusanywa kama kinaendana na picha zilizofanyika kwenye mashini hizo. Katika mpango huu tumeunganisha wodi zote kuweza kuangalia majibu ya picha za CT scan, X-Ray na MRI kupitia kompyuta zilizopo mawodini na Kliniki. Lengo ni kuachana na kutumia picha za film kutoa majibu ambazo ni gharama.

4.8 Kupunguza gharama za uchapishaji
Kupunguza gharama za uchapishaji wa nyaraka za wagonjwa (Paperless electronic System) ambapo Hospitali imeanzisha utaratibu wa ‘paperless’ ikiwa ni Hospitali kutotoa huduma yoyote ya makaratasi na nyaraka za mgonjwa bali kila kitu kuwa katika mfumo wa kompyuta (soft copy) ili kutolewa katika nakala pale tu itakapoonekana ni hitajio la mgonjwa na kwa utaratibu maalum. Hii imepunguza gharama kwa Hospitali kwa kiasi kikubwa hasa upande wa (stationeries) na fedha hizo kuweza kutumika katika matumizi mengine katika kuboresha huduma za Hospitali. Mfano maabara tulikuwa tunanunua karatasi rimu mia moja kwa mwezi kutoa majibu ya wagonjwa, kwa sasa majibu yote yanapatikana kwenye kompyuta online.

4.9 Ukarabati wa Miuondombinu.
a.    Hospitali inaendelea kufanya ukarabati wa majengo na kurekebisha mifumo yake ya maji safi na maji taka. Katika utekelezaji wa mkakati huu, Hospitali imejiwekea utaratibu wa kuelekeza nguvu zake kwenye jengo moja moja kabla ya kuanza ukarabati wa jengo jingine ili kutumia vizuri rasilimali fedha chache zilizopo. Ukarabati wa majengo ulianza na jengo la kina mama lililotolewa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukarabati huo uligharimu T.Shs. 312 milioni. Aidha tumeendelea kuboresha mahali pa wagonjwa kusubiri hususani eneo la idara ya dharura na jengo la wagonjwa wa nje. Tumepanua idara ya magonjwa ya dharura ili kuongeza wigo katika huduma hiyo pamoja upanuzi wa maeneo ya kutolea huduma kwa wateja wa NHIF.
b.    Changamoto za miundo mbinu ya maji machafu jengo la watoto umeshafanyiwa kazi na hivi sasa unaendelea vizuri. Tunategemea kuanza ukarabati wa jengo la kina mama ikiwa ni pamoja na kuweka mfumo wa gesi maeneo mbalimbali.
c.    Ukarabati wa jengo la ofisi za madaktari wa wagonjwa wa akili ya afya ulikamilika mwanzoni wa mwezi wa Julai 2016 na uligharimu T.shs. 65 milioni. 
d.    Ukarabati wa jengo la fiziotherapia ulikamilika nao uligharimu T.Shs. 30 milioni. Aidha Hospitali ilifanya ukarabati mdogo wa barabara uliogharimu T.Shs. 15 milioni.
e.    Hospitali imefufua mashini zote mbili za kuchoma taka kwa gharama ya T.Shs. milioni 60, pamoja na ukarabati mwingine mdogo mdogo unaoendelea kurekebisha mambo ya miundo mbinu.
5.0 Mipango ya Muda Mfupi na Muda Mrefu iliyopo sasa:
a.    Hospitali imeamua kupitia upya mfumo wake na muundo wa kuona wagonjwa katika OPD zote, wagonjwa waliolazwa na mfumo wa wagonjwa wanaohitaji huduma za vipimo na uchunguzi mbalimbali. Lengo ni kuhakikisha mteja anapata huduma katika kiwango na muda unaokubalika.
b.    Hospitali imedhamiria kuendelea kununua vifaa mbalimbali vya kutolea huduma ikiwemo vifaa vya vyumba vya upasuaji, mashini ya Fluoroscopy ili wagonjwa waweze kupata vipimo hapa Hospitalini. Vipimo vinavyopimwa na mashini hii ni pamoja na Barium Meal (kugundua vidonda vya tumbo), urethrogram (kugundua matatizo ya kuziba njia ya mkojo) n.k
c.    Hospitali itahakikisha stahili zote za wafanyakazi zinalipwa kwa wakati na kuongeza wigo wa kutoa motisha ili kuongea morali ya utendaji.
d.    Kuendelea kuboresha huduma kuwa za ubingwa wa hali ya juu katika maeneo mengine ikiwamo mfumo wa ubongo, chakula, ngozi, maskio, pua n.k
e.    Kuhakikisha wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje wanapungua kwa kiwango kikubwa ili kutimiza azma ya uanzishwaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
f.    Hospitali inakusudia kuongeza kasi ya kusomesha watalaam wake ili kuwa na ujuzi zaidi wa kuweza kuendana na kasi ya mabadiliko katika tasnia ya tiba, uchunguzi na utafiti.
g.    Hospitali itaongeza mpango wa kutembelea Hospitali kadhaa hapa nchini ili kutoa mafunzo katika nyanja mbalimbali na kuongeza ujuzi kwa watalaam walioko nje ya Dar Es Salaam waweze kutoa tiba na kufanya uchunguzi huko huko waliko badala ya kuleta wagonjwa wasio wa lazima Hapa.
h.    Kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 4.3 hadi shilingi bilioni 5 kwa mwezi ifikapo Julai 2017.
i.    Kuendelea kuongeza vyumba vya upasuaji, na vyumba vyenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU) ili kupunguza na badaye kuondoa muda wa wagonjwa kusubiri kufanyiwa upasuaji.


Aminiel Buberwa Aligaesha,
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma,
Hospitali ya Taifa Muhimbili,
Novemba 1, 2016.

No comments