Header Ads

MBAO FC WAWAPONZA DEUS KASEKE, OBREY CHIRWA WAFUNGIWA NA TFF

SHERIA ni msumeno na ukiuchezea unakukata, nyota wa Yanga, Simon Msuva, Obrey Chirwa na Deus Kaseke kwa pamoja wamesimamishwa kucheza mechi za Ligi Kuu Bara msimu ujao kwa kosa la kumsukuma na kumwangusha mwamuzi Ludovic Charles. 


Wachezaji hao wanadaiwa kutenda kosa hilo katika mchezo wa timu yao dhidi ya Mbao FC, Mei 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambao uliisha kwa Mbao kushinda bao 1-0. Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas alisema, Msuva, Chirwa na Kaseke wamesimamishwa wakisubiri suala lao la kumsukuma na kumwangusha mwamuzi huyo kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya shirikisho hilo. 

“Uamuzi huu wa Kamati umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu, pia Mwamuzi Ludovic Charles amepewa onyo kali kwa kutodhibiti vizuri mchezo kwa mujibu wa Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi,” alisema Lucas. Akizungumzia kitendo hicho, Msuva alisema; “Siyo sawa, mimi sikumgusa mwamuzi lakini hakuna jinsi maana wameshaamua.

” Wakati huohuo, Yanga pia imepigwa faini ya Sh milioni tatu kutokana na makosa matatu iliyofanya katika mchezo huo dhidi ya Mbao. Makosa hayo ni kupita mlango usio rasmi (Sh milioni moja), kutoingia vyumbani (Sh milioni 1.5) na Sh 500,000 kwa kuonyesha vitendo vinavyoashiria ushirikina. 

Pia Yanga imetakiwa kurekebisha uzio wa ndani upande wa magharibi wa Uwanja wa CCM Kirumba baada mashabiki wake kuuvunja na kuingia uwanjani kushangilia ubingwa. Pia Mbao FC imepigwa faini ya Sh 500,000 baada ya mashabiki wake kuingia uwanjani kushangilia ushindi wa timu yao.

No comments