Header Ads

Jini Kabula Adata, Alazwa Muhimbili

Staa wa filamu za Kibongo, Miriamu Jolwa ‘Jini Kabula’.
Nasikitisha! Staa wa filamu za Kibongo, Miriamu Jolwa ‘Jini Kabula’ anadaiwa kudata ‘kuchanganyikiwa’ na hivi sasa amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako anapatiwa matibabu, Risasi Mchanganyiko limetonywa.
Chanzo makini kilicho karibu na msanii huyo kililiambia Risasi Mchanganyiko kuwa mwanamama huyo alikuwa kwa rafiki yake ambaye pia ni msanii wa filamu, Esha Buheti kabla ya hali yake kuanza kubadilika na kuzungumza mambo yasiyoeleweka.
“Jini Kabula amechanganyikiwa kabisa yaani, kwani alikuwa kwa rafiki yake huyo, ndipo alipoanzia kuumwa ikabidi ndugu zake wamchukue na kumpeleka Muhimbili ambako mpaka sasa anaendelea na matibabu.
“Ukimuona anakutambua, lakini anayoyaongea hayaeleweki, ni kwamba amedata kabisa licha ya kwamba kama alikuwa anakufahamu awali hata sasa akikuona anakutambua, lakini ndiyo hivyo anaongea vitu mchanganyi-kochan-ganyiko, ukweli anatia huruma sana,” kilisema chanzo hicho.

RISASI LAMSAKA MZAZI MWENZAKE CHUZ!
Ili kuujua ukweli na kujiridhisha zaidi, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta mzazi mwenzake, ambaye pia ni msanii wa filamu, Tuesday Kihangala ‘Chuz’ na kutaka kujua hali ya mwenzake, ambako mkali huyo wa tamthiliya ya Closed Chapter, alikiri Jini Kabula kuugua.
“Nilipata taarifa za Kabula kwamba anaumwa na alikuwa kwa rafiki yake, lakini ndugu zake walimchukua na baadaye kupelekwa Muhimbili ambapo mpaka sasa anaendelea na matibabu, nimeambiwa anaongea vitu ambavyo havieleweki,” alisema Chuz.
Ili kupata ukweli zaidi, Risasi Mchanganyiko halikuchoka na safari hii lilimtafuta rafiki wa muda mrefu wa muigizaji huyo ambaye pia ni msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya akiwa na Kundi la Scorpion, Esha Buheti, ambaye naye alikiri shoga yake kupata matatizo.
“Ni kweli anaumwa, niliwasiliana na ndugu zake wakaja kumchukua kumpeleka Muhimbili, siwezi kusema hasa nini tatizo, lakini anaonekana hayuko sawa, maana kuna maneno anayaongea ambayo si ya kawaida.
“Kuna wakati tukaona tumpeleke kanisani kwa ajili ya maombi, tukaenda pale Kawe akaombewa, lakini hakukuwa na mabadiliko yoyote, ndiyo maana tukawaomba ndugu zake wampeleke hospitali,” alisema Esha.
Alipoulizwa kama ameshakwenda kumtembelea tangu aende huko, alisema hajakwenda kwa vile hali yake ya afya siyo nzuri.
Naye dada wa Jini Kabula aliyejitambulisha kwa jina la Dayness alithibitisha kuwa mdogo wake huyo amelazwa katika chumba cha wagonjwa waliochanganyikiwa kutokana na maleria kupanda kichwani na hali yake bado siyo nzuri.

No comments