Header Ads

Niyonzima Apewa Jezi no 8, Kazimoto Kwaheri Simba SC


DAR ES SALAAM: BAADA ya kiungo wa zamani wa Yanga, Haruna Niyonzima raia wa Rwanda kutua Simba, imeelezwa kuwa atakuwa akitumia jezi namba nane ambayo ilikuwa ikivaliwa na Mwinyi Kazimoto.

Niyonzima ambaye anajiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Yanga alipomaliza mkataba wake, kwa sasa yupo kwao Rwanda kwa mapumziko huku akitarajiwa kurejea nchini mwezi ujao kujiandaa na msimu mpya.

Jezi hiyo ndiyo imekuwa chaguo sahihi kwa kiungo huyo kwani tangu ajiunge na Yanga mwaka 2011 akitokea APR ya nyumbani kwao, amekuwa akiitumia mpaka ameondoka, na akiwa timu yake ya taifa amekuwa akiitumia pia.

Mmoja wa mabosi kutoka ndani ya Simba, ameliambia Championi Ijumaa kuwa, Niyonzima watampatia jezi hiyo anayoipenda huku wakiwa na mpango wa kuachana na Kazimoto.

“Niyonzima atakuwa akiitumia jezi namba nane ambayo hapa alikuwa akiivaa Kazimoto, tumefikia uamuzi huo baada ya kutokuwa na mpango na Kazimoto ambaye mkataba wake umemalizika, hivyo hatakuwa sehemu ya wachezaji wetu kwa msimu ujao.

“Kikubwa ambacho Wanasimba wanatakiwa kuelewa ni kwamba, tupo katika kuijenga Simba ya kimataifa, hivyo watulie kwani hiki tunachokifanya ni mapendekezo ya benchi letu la ufundi chini ya Joseph Omog,” alisema bosi huyo mwenye nguvu klabuni hapo.
Omary Mdose | CHAMPIONI

No comments