Header Ads

SAMATTA APIGA BONGE LA BAO LAKINI TAIFA STARS YABANWA NA LESOTHO

Licha ya Mbwana Samatta kufunga bao la kiwango cha juu dhidi ya Lesotho bado halikutosha kuipa ushindi timu ya taifa, Taifa Stars katika mchezo baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Taifa Stars ambayo iliweka kambi nchini Misri kwa ajili ya mchezo huo wa kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2019, imeambulia sare ya bao 1-1 katika mchezo huo wa kwanza wa Kundi L.

Ikianza kucheza kwa kasi ndogo, Taifa Stars iliongeza kasi baada ya Samatta kufunga bao dakika ya 27 kwa njia ya faulo baada ya beki Gadiel Michael kuchezewa faulo nje ya eneo la 18.

Mpira aliopiga Samatta ulielekea wavuni moja kwa moja na kuamsha shangwe kwa mashabiki waliohudhuria mchezo huo ulioanza saa 2:00 usiku wa Jumamosi.

Baada ya bao hilo, Lesotho waliongeza kasi na kufanikiwa kusawazisha katika dakika ya 34 baada ya walinzi wa Stars kufanya uzembe wa kumsahau mfungaji.

Kipindi cha pili Stars iliingia kwa kasi na kulishambulia lango la Lesotho lakini hawakuweza kupata bao

Licha ya kufanya mabadiliko ya kuwaingiza Farid Mussa, Mbaraka Yusuph na Abubakar Salum 'Sure Boy' bado milango ya Lesotho ilikuwa migumu.

Matokeo hayo siyo mazuri kwa Stara kwa kuwa sasa itakuwa na mlima mrefu wa kupanda dhidi ya Uganda na Cape Verde ambao wapo kundi moja la L.

No comments