Header Ads

Aunt Ezekiel, kama sikusomi vile! ...Umepotelea Wapi?

Nianze kwa kuwashukuru wasomaji wote wa safu hii ambao mara kwa mara wamekuwa pamoja nami kwa kunipa ushauri na nasaha zao kuhusu namna ya kuboresha na kuinogesha.
Nikiri wazi kuwa michango yao ni muhimu sana ili kuifanya sehemu hii kuwa ya wadai wote. Baada ya wiki jana kuzungumza na dada yangu Saida Kalori, wiki hii barua yangu naielekeza kwa mwanafilamu, Aunt Ezekiel Grayson.
Ninamfahamu kidogo huyo muigizaji maana ni mmoja wa wale wanaofanya vizuri. Yuko vizuri na ukitaka kufahamu hicho ninachokisema, cheki filamu zake kama vile Mrembo Kikojozi, Yellow Banana, House Girl and House Boy, Nampenda Mke Wangu, Usiku wa Maajabu na nyingine nyingi.
Juzikati nilipatwa na mshtuko baada ya kumuona katika mahojiano na televisheni moja ya mitandaoni, akizungumzia juu ya nia yake ya kuingia katika Muziki wa Kizazi Kipya, kwani tayari ameshaingia studio na kurekodi wimbo mmoja.

Lakini cha kushangaza, alisema amefanya muziki huo, hata hivyo, siyo kwa sababu ameumbwa kuwa mwanamuziki, bali kwa kushawishiwa na mmoja wa wasanii wenzake, ndiyo maana hata katika kurekodi kwenyewe, alilazimika kufanya kwa siku tatu ili kazi hiyo ikamilike. Aunt anasema yeye hajui kuimba kwa sababu hakuzaliwa kuimba tofauti na vile alivyozaliwa kuwa muigizaji. Dah, lazima niwe mkweli, kauli hii ya staa huyu imenipa mawazo mengi na kujaribu kuona kwa mbali, kiini cha kufa kwa sanaa ya uingizaji katika Tanzania.
Bongo Muvi ambayo inalalamikiwa na wadau kuwa imejaa watu wasio na sifa wala vipaji, inaelekea shimoni, kwani imekosa tena mvuto kwa Watanzania, ambao sasa ni kama wamegoma kununua kazi zao ambazo nyingi, zinakosa uhalisia kwa watazamaji. Na moja ya sababu kubwa iliyosababisha kugoma sokoni kwa kazi zao ni baada ya kujaza watu walioingia kwenye sanaa hiyo kwa sababu za ushkaji, undugu, mapenzi na vitu vingine ambavyo viliweka pembeni vipaji, mafunzo na hata maadili ya sanaa ya uingizaji.
Ni kama ilivyomtokea Aunt Ezekiel, mtu anakutana na msichana mwenye umbo la kuvutia, mwenye sura nzuri na kuamini kuwa kwa muonekano wake, anafaa kuwa muigizaji. Ndiyo maana tukawa na waigizaji wanaoamini katika kuanika miili yao hadharani, kitu ambacho kiliivunjia sana heshima fani hiyo ambayo baada ya waigizaji wenye vipaji kufariki, akiwemo Steven Kanumba, imepoteza mvuto wake.
Sasa Aunt Ezekiel anasema wazi kuwa yeye hana kipaji cha kuimba na wala hawezi kufanya hivyo, kwa nini anaingia studio kujaribu kitu ambacho anajua hana karama nacho? Maana kama amepoteza fedha kwenda studio kujaribu kuimba, ni wazi pia kuwa atatumia ujanjaujanja ili wimbo wake uweze kupata nafasi ya kupigwa katika vituo vya redio na hata televisheni.
Kwa ukubwa wa jina lake na urafiki wake na watu wa maeneo hayo, ni dhahiri kuwa atapewa ‘airtime’, kitu ambacho itakuwa ni kuwanyima haki waimbaji wengine ambao wana vipaji vya kweli, lakini hawana ‘connections’.
Hii haiwezi kuwa sawa, katika vitu vinavyohitaji vipaji, tuache wenye vipaji wafanye, vinginevyo tutaharibu sanaa hizi kama ilivyotokea Bongo Muvi. Kwani amekaa chini na kujiuliza kwa nini hivi sasa filamu zimekwama sokoni? Kama hajajiuliza, basi nimtaarifu dada yangu kuwa watu waliovamia sanaa hiyo, kama yeye anavyotaka kuvamia Bongo Fleva, ndiyo walioipeleka ICU. Iliwaacha wenye vipaji, ikavamiwa na wenye maumbo mazuri ya kuvutia, lakini hawana ABC za filamu. Hili tulipige vita kwa nguvu zote!
BARUA NZITO NA GABRIEL NG’OSHA Maoni & Ushauri: +255 620 744 592 - GPL

No comments