Header Ads

KAMATI YA UCHAGUZI YAVUNJWA, YAUNDWA UPYA, AMEBAKI MWENYEKITI TU


Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambayo imekutana leo Jumanne imefanya mabadiliko ya Kamati ya Uchaguzi na kuwaengua Wajumbe wanne walioonyesha kumtetea rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi ambaye kwa sasa yuko rumande kwa tuhuma mbalimbali.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika makao makuu ya shirikisho hilo, Karume jijini Dar na kuongozwa na Kaimu Rais, Wallace Karia.
Wajumbe walioondolewa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti, Wakili Domina Madeli, Juma Lallika, Jeremiah Wambura na Hamim Mahmoud Omar na sasa Mwenyekiti, Wakili Revocatus Kuuli atafanya kazi na Mohamed Mchengerwa, Wakili Malangwe Ally Mchungahela, Wakili Kiomoni Kibamba ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza ma Wakili Thadeus Kalua.
Kabla ya hapo, Mwenyekiti Kuuli alitofautiana na Wajumbe wenzake wote wa Kamati hiyo ya awali juu ya Malinzi kuruhusiwa kuendelea kuogombea katika uchaguzi wa Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma licha ya kwamba hakutokea kwenye usajili.
Malinzi hakutokea kwenye usaili kutokana na kuwa anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kabla ya kufikishwa Mahakamani kusomewa mashitaka 28, ambayo yalimfanya anyimwe dhamana na kupelekwa rumande hadi Julai 17, mwaka huu upelelezi wa kesi uyake utakapokamilika.
Wakili Kuuli alipingana na wenzake waliotaka Malinzi aruhusiwe kuendelea na mchakato japo hakushiriki usaili na kufikia kuvunja kikao, kisha kupeleka taarifa Kamati ya Utendaji ya TFF, ambayo nayo baada ya kikao chake cha leo imefikia uamuzi wa kuiunda upya Kamati ya uchaguzi pamoja na Kamati nyingine.
Kamati nyingine zilizotajwa na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Salum Madadi leo ni Kamati Maadili ambayo inaundwa na Mwenyekiti, Amidou Mbwezeleni, Steven Zangira, Mkuu wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Glorius Luoga, Walter Lungu na Amin Bakhresa.
Kamati ya Rufaa ya Maadili; Wakili Rugemeleza Nshala, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, DCP Mohammed Mpinga, Wakili Benjamin Karume, Dk Lisobine Chisongo, ASP Benedict Nyagabona.
Kamati ya Nidhamu; Tarimba Abbas, Peter Hela, Boniface Lyamwike, Dk Billy Aonga na Kassim Dau.
Kamati ya Rufaa ya Nidhamu; Wakili Rahim Zubeiry Shaaban, Siza Chenga, Abbas Mtemvu, Amani Mulika na Stella Mwakingwe wakati Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi inaundwa na Wakili Abdi Kagomba, Kenneth Mwenda, Rashid Sadallah, Jabir Shekimweri na Mohamed Gombati.
Sasa Kamati mpya ya Uchaguzi inatarajiwa kuendelea na mchakato, ambao ulisimamishwa kwa muda tangu Julai 2 ukiwa katika hatua ya usaili.
Malinzi, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa kwa pamoja na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga wako kwa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam na wanatarajiwa kufikishwa tena Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam Julai 17, mwaka huu.
(HABARI NA MUSA MATEJA/GPL)

No comments