Header Ads

Maumivu kabla ya hedhi (Premenstrual Syndrome-PMS)


WANAWAKE wengi wamekuwa na tatizo la kusikia maumivu kabla ya hedhi zao na kuniomba nifafanue kuhusu tatizo hilo, leo nitafanya hivyo. Ni kweli kwamba wanawake wengi hupata matatizo kabla ya kuanza hedhi lakini wapo wanaopata wakati wa hedhi na wengine mara ya baada ya kukoma hedhi.
Ili msomaji uelewe hayo, nitafafanua kila moja ya hayo  na kuona sababu za matatizo hayo na tutashauri jinsi ya kuepuka tatizo hilo. Kwa wale wanaopata maumivu kabla ya hedhi Premenstrual Syndrome kifupi (PSM).
Watambue kuwa hiyo ni hali ambayo humwathiri mwanamke kihisia, afya yake ya mwili na tabia yake katika kipindi fulani cha mzunguko wake wa hedhi, kwa kawaida kabla tu ya kuingia mwezini. Ni kawaida kwa mwanamke kukumbwa na tatizo hili na huathiri karibu asilimia zaidi ya themanini ya wanawake wanaopata hedhi. Maumivu huanza siku tano hadi kumi na mbili kabla hajaanza siku zake za hedhi. Zipo dalili nyingi za tatizo hili kama vile kuwa na msongo wa mawazo au wasiwasi, kuwa na mfadhaiko, kuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya kihisia na hasira, kuwa na matatizo ya kupata usingizi, kujitenga na jamii, kuhangaika na kushindwa kutuliza mawazo.
Lakini pia mwanamke hupata mabadiliko katika maumbile yake ya mwili kama vile kusikia maumivu ya kichwa au kwenye maungio ya mifupa, kuhisi uchovu, kunenepa, kusikia maumivu akiguswa kwenye matiti yake, kutokwa na chunusi nyingi usoni na kukosa choo na kuharisha. Kwa baadhi ya wanawake, mabadiliko haya ya maumivu ya mwili yanaweza kuwa makubwa kiasi cha kuathiri shughuli zake lakini licha ya wengine kuathirika sana, matatizo haya huisha ndani ya siku nne baada ya mwanamke kuanza siku zake za hedhi. Wapo baadhi ya wanawake
ambao husikia maumivu haya ya kabla ya hedhi huwafanya washindwe kabisa kuendelea na shughuli zao za kila siku, na huwatokea kila mwezi (kabla ya hedhi).

Aina hii ya PMS huitwa Premenstrual Dysphoric Disorder (PMDD). Dalili za Premenstrual Dysphoric Disorder ni pamoja na mfadhaiko, hisia za ghafla zinazobadilika, hasira, wasiwasi, kushindwa kufikiri, hasira za ghafla na kuwa na msongo wa mawazo. Wengi wanajiuliza kwa nini hupata maumivu kabla ya kuingia katika siku zao za hedhi? Chanzo kamili hakijathibitika, lakini sababu zifuatazo zimeonyesha kuwa na mchango mkubwa. Kwanza, ni mabadiliko yanayotokea katika mzunguko wa homoni.
DALILI Dalili za maumivu kabla ya mwanamke hajaingia katika hedhi mara nyingi huwa zinabadilika kutokana na mabadiliko ya homoni kwenye mzunguko wa hedhi. Viwango vya homoni ya Estrogen na Progesterone
huongezeka wakati fulani katika mwezi na kusababisha tatizo.

Hii ni kwa sababu muongezeko huu husababisha mabadiliko ya mara kwa mara ya namna mwanamke atakavyojisikia, kuleta wasiwasi na kusababisha hasira za haraka. Vilevile mabadiliko ya viwango vya kemikali katika ubongo yaani mabadiliko katika viwango vya Serotinin katika ubongo vinasababisha Premenstrual Syndrome.
Viwango vya Serotinin huathiri namna mwanamke atakavyojisikia. Serotinin ni nini? Hii ni kemikali katika ubongo inayoamsha namna
ya kujisikia, hisia na mawazo. Kuwa na kiwango kidogo cha Serotinin kunasababisha mfadhaiko, uchovu, kupenda kula sana na kukosa usingizi. Lakini wanawake wengine wanakuwa na mfadhaiko japokuwa huwa siyo sababu za matatizo yote tuliyoyataja hapa.

MAMBO YA KUFANYA KUEPUKA HAYA Mlo
ni kitu cha kwanza cha kufanya. Unaweza kuondokana au kupunguza makali ya tatizo la maumivu kabla ya kupata siku zako za hedhi kwa kufanya mabadiliko ya chakula unachokula, kufanya mazoezi kila siku kwa kufanya haya yafuatayo. Jitahidi kupunguza mlo, punguza chumvi na chakula chenye chumvi nyingi kuzuia tumbo kujaa, kula matunda, mbogamboga za majani na nafaka zisizokobolewa ili kupata complex carbohydrates. Unashauriwa kula chakula chenye uwingi wa calcium na mwanamke mwenye tatizo hili anashauriwa asitumie kahawa na pombe.
MAZOEZI Kila mmoja anashauriwa awe anafanya mazoezi angalau kwa ama ya kukimbia au kutembea angalau kwa dakika 30, kuendesha baiskeli, kuogelea au mazoezi mengine ya kukutoa jasho. Mazoezi ya kila siku yataboresha afya yako na kukuondolea baadhi ya dalili, kama uchovu na mfadhaiko. Pia yeyote mwenye tatizo hilo anatakiwa apate usingizi wa kutosha, afanye mazoezi ya misuli au upumuaji mzito ili kuondoa maumivu ya kichwa, wasiwasi na matatizo ya kukosa usingizi au jaribu kufanya yoga au massage ili kuondoa msongo wa mawazo.
TIBA YAKE NA USHAURI Kabla ya tiba ni vema kumuona daktari  lakini wanawake wenye matatizo haya na hata wasio na matatizo kama haya wanashauriwa kubadili mtindo wa maisha kuweza kuwasaidia kuondokana na tatizo hili. Kulingana na ukubwa wa tatizo, daktari anaweza kukuandikia dawa moja au zaidi za kusaidia kuondoa tatizo hili. Utendaji kazi na msaada wa dawa hizi hutofautiana kutoka mwanamke mmoja hadi mwingine. Dawa ambazo hutolewa ni kama vile Antidepressants, Nonsteroidal anti-inflammatory drugs (NSAIDs) na Diuretics ambazo daktari ataelekeza jinsi ya kutumia. Lakini pia utumiaji wa calcium ya kutosha katika mlo au matumizi ya vidonge vya calcium kunaweza kuondoa dalili za maumivu kabla ya siku za hedhi.
Na Dk. Marise Richard | Simu: 0713 252 394

No comments