Header Ads

Ndoa Ya Messi Na Funzo Lenye Imani Na Msimamo

Lionel Messi akiwa na mpenzi wake wa muda mrefu, Antonela Roccuzzo wakifanya yao baada ya kufunga ndoa.    
HALIPO na sijaliona neno mbadala la kutumia, zaidi ya ndoto imetimia. Kitendo cha mwanasoka maarufu na mwenye uwezo wa kipekee, Lionel Messi kufunga ndoa na mpenzi wake wa muda mrefu, Antonela Roccuzzo ni matokeo halisi ya Imani na msimamo.

Kwa nini imani na msimamo? Kukutana kwao, chimbuko na ustawi wa penzi lao linaweka na kuacha histori yenye mshibo wa kuigwa na kila kijana mwenye malengo na utoshelezi wa fikra maishani, Messi au ‘Leo’ kama anavyopenda Kutambulishwa, pamoja na mkewe Antonella walifunga ndoa usiku wa kuamkia jana, jijini Rosario nchini Argentina, ndani ya moja ya hoteli za kifahali ya City Center Hotel and Casino.
Akipokea zawadi kutoka kwa mtoto wake.
WALIKUTANA LINI NA WAPI?
Messi alikutana na Antonella Rosario, akiwa na miaka 5 huku mwanamke huyo mrembo akiwa binti wa miaka 4, yapo mambo makubwa mawili yaliyowakutanisha katika umri huo mdogo. Ujirani na urafiki uliokuwepo kati ya Messi na mchezaji Lucas Scagila, ambaye ni binamu wa Antonella, wakiishi na kucheza pamoja kama majirani.
PENZI LA ASILI
Wawili hao, walianza kupendana wakiwa watoto kabisa, kwani walitumia muda mwingi kucheza pamoja, huku Antonella ambaye ni binti wa mmiliki wa duka kubwa la bidhaa mbalimbali (supermarkert), akionekana mkubwa kwani Messi alikuwa na tatizo la ukuaji (Growth efficiency).

PENZI LA KINDAKINDAKI
Messi akiwa na miaka tisa, mwaka 1996 ndipo alianza kugundua hisia kali za kimapenzi zikishamiri moyoni mwake juu ya Antonella, hakuficha jambo hilo akawa anawaambvia marafiki zake. Siku moja alichukua karatasi na kalamu na kisha kuandika maneno ya kujipiza kuwa ni lazima awe mpenzi wa Antonella na kuuahidi moyo wake ilikuwa haikwepeki kumuoa.
Kilichochochea zaidi penzi la wawili hao kuibuka, ni kitendo Antonella kuambatana kwa ukaribu sana na Messi na Lucas, hususan kwenda kupunga upepo kando ya Mto Parana, huko ndiko Messi alipata nafasi nzuri kabisa ya kumuonesha Antonella upendo wa wazi wakati Lucas akiwa bize na michezo ya ufukwe.

DUNIA ILIJARIBU KUWATENGANISHA
Messi akiwa na ndoto za kuwa mchezaji mkubwa duniani, alijiapiza kuyatimiza mambo makubwa mawili, kushinda kwenye soka na kumuoa Antonella, yote kayatimiza na maisha yanaendelea.
Wakiwa katika picha ya pamoja.
Akiwa na miaka 13, ndipo ombi lake la kimapenzi lilikubaliwa na Antonella na kuanzia hapo wakaingia rasmi kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa siri kubwa mno, lakini walitengana baada ya Messi kukubali ofa ya kwenda kucheza kwenye klabu ya Barcelona, kikosi cha watoto maarufu kwa jina la La Masia, nchini Hispania baada ya kuahidiwa matibabu ya tatizo lake la ukuaji  na Antonella kubaki Argentina ambapao alijiunga na Chuo kikuu cha nchi hiyo kijulikanacho kama National University, akisomea selimu ya meno na tiba yake.
Baadaye aliachana na kozi hiyo kisha kuanza kusomea elimu ya mahusiano ya umma (Social Communication).

ANTONELLA ALIZIDIWA NA SHETANI
Akiwa mbali na Messi, Antonella alishindwa kuvumilia na kujikuta akiingia kwenye vishawishi kwa kuanzisha uhusiano na kijana mwingine, ambaye walidumu kwenye mahusiano kwa muda wa miaka mitatu.
MUNGU AWAKUTANISHA KWA NJIA YA UCHUNGU
Antonella, alifiwa na rafiki yake mpenzi, ambaye alijulikana kwa wengi akiwemo Messi, katika ajali ya gari. Messi alilazimika kusafiri kutoka Barcelona wakiwa na miaka kadhaa hawajaonana na wala mawasiliano, Messi alilazimika kuwa bize na mpira ili kujijengea jina huku masomo yakiumeza ubongo wa Antonella.

Kufiatia kufiwa na rafiki, Messi alikwenda kauamfariji Antonella na muda wote wa kuhani msiba walikuwa pamoja na penzi lao kuchipuka upya ingawa  walifanya kwa siri tena hadi lilipoanza kuchipuka wazi mwaka 2007.
WATOTO KABLA YA NDOA
Ilimbidi Antonella kumpokea Messi kwa moyo wake wote kwani upole, ustaarabu , uvumilivu na penzi la dhati alilolionesha vilikuwa silaha na mapigo tosha kabisa kuushinda moyo wa mrembo huyo. Alilazimika kuhamia nchini Hispania kuungana na Messi ambapo walianza kuishi pamoja, tayari jamaa akiwa staa mkubwa wa mpira na dunia nzima ikimjua.
Tarehe 2, Februari mwaka 2012 ni siku ambayo Antonella alinasa mimba ya mwanaye wa kwanza,  Thiago na kumzaa tarehe 2, Novemba mwaka huo, miaka mitatu baadaye alijifungua mtoto wao wa pili, Mateo tarehe 11, Septemba mwaka 2015, wakiwa wanaishi bila ndoa.
ANTONELLA NA MAISHA YA USIRI
Hapendi kabisa maisha ya kujulikana. Miezi kadhaa iliyopita, Messi alitangaza kufunga ndoa na mrembo huyo, kitendo kilichopelekea ugomvi mkubwa kwani hakutaka watu wajue chochote hadi siku ya tukio. Si mtu wa kujumuika sana na watu, anap marafiki wakubwa wawili tu.
Rafiki yake mkubwa zaidi ni Sofia Balbi, mke wa mchezaji wa Barcelona, Luis Suares na mwingine ni Daniella Semaan, ambaye ni mpenzi wa mwanasoka wa timu hiyohiyo ya Barcelona, Sesc Fabrigas.

NDOTO IMETIMIA
Tazama walikotoka, hadi juzi kufunga ndoa. Inagia moyoni mwa Messi na ukague kwa uangalifu na umakini mkubwa furaha aliyonayo, kwa kufuatisha historia yao. Uvumilivu, imani na msimamo vimelipa kwa matokeo chanya.
Ndoa ilihudhuriwa na zaidi ya watu maarufu 260, furaha kubwa ikitanda mioyoni na machoni mwa wahudhuriaji wengi, wanaijua historia ya wawili hao, inavutia kiasi cha kupewa majina ya Ndoa ya Mwaka na Ndoa ya Taifa.

KUNA HILI SOMO
Messi ni mtu maarufu sana duniani. Anpendwa na wengi, wanawake warembo, matajiri na wasomi wanapenda kutoka kimapenzi na Messi, lakini imani yake kwa Antonella tangu akiwa kijana mdogo kabisa, msimamo wake haukumezwa na umaarufu, watu wangapi hula viapo vya kudumu na wapenzi wao wa ujanani lakini wakishapata maisha mengine wanawaacha kwa kuhadaiwa na warembo wengine? Lakini Messi na Antonello wameweka historia njema kabisa, tangu wakiwa na miaka mitano, hadi leo Messi akiwa na miaka 30 na mkewe 29, wametimiza walichoahidiana, ndoa.

CHUKUA HII
Msimamo, imani na na upendo wa dhati havijawahi kushindwa mahali popote maishani. Hakikisha unakipenda kitu/jambo kwa upendo wa dhati na kumaanisha, jiamini na amini kuwa inawezekana kukitimiza na kisha weka msimamo thabiti juu yake, Mungu huweka mikono yake kwa watu kama hao, tazama leo Messi na Antonella, wanafurahia maisha baada ya kuvumiliana kwa miongo kadhaa. Inatia raha, inaleta bashasha, majukumu yalibana, lakini nilidhamiria kuhudhuria sherehe ya ndoa yao, Mungu awabariki na kuwapa maisha marefu na yenye Baraka tele, ndoa yao ina tafsiri moja tu, imani na msimamo.
Habari: Brighton Masalu/ GPL

No comments